Ugaidi ni Nini? Na Magaidi ni Watu Gani Hasa? Sehemu ya Kumi na Tatu: Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), 'tawi' hatari la Al-Qaeda linalosumbua mno Ukanda wa Sahel
Karibu katika mfululizo wa makala kuhusu ugaidi.
Hamasa ya kuandika makala hizi imetokana na mafanikio makubwa ya kitabu cha “Afisa Usalama wa Taifa ni Mtu Gani? Na Anafanya Nini?” ambacho kilitokana na mfululizo wa makala kama huu.
Kadhalika, hivi karibuni mwandishi alichapisha kitabu kingine kilichotokana na mfululizo wa makala kuhusu "UJASUSI (espionage) ni Nini? Na MAJASUSI (spies) Wanafanya Kazi Gani Hasa?"
Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), ambayo inajulikana pia kama “Vuguvugu la Nusra ya Uislamu na Waislamu”, ni muungano wa makundi kadhaa ya jihadi wenye mafungamano na Al-Qaeda katika eneo la Sahel, Afrika Magharibi. Tangu kuundwa kwake mwaka 2017, JNIM imeibuka kuwa tishio kubwa la usalama katika eneo hilo, ikichangia kwa kiasi kikubwa vurugu na ukosefu wa utulivu katika nchi kama Mali, Burkina Faso, na Niger. Kufikia mwaka 2024, kundi hili limeendelea kushiriki katika mashambulizi mbalimbali dhidi ya vikosi vya usalama, serikali, na raia wa ndani ya Sahel.