[Tahadhari Ya Matusi Ya Nguoni] Huu Sio Unaharakati, Haya Ni Matusi Na Udhalilishaji Dhidi Ya Mama Samia.

“Kushindwa kuonya ni dhambi kubwa kabisa katika taaluma ya intelijensia.” Naam, sisi ambao bado tunaendelea kuwa wadau wa taaluma hiyo (hadi tunaingia kaburini) tunawajibika kuepuka dhambi hiyo.

Pia ni muhimu kwetu (maafisa wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa) kutimiza wajibu huu kutokana na ukweli kwamba Idara yetu ya Usalama wa Taifa ipo hoi bin taaban. Miaka 10 ya utawala wa Kikwete uliifanya Idara hiyo kuhangaika zaidi na waliokuwa wanapambana na ufisadi ambao ulishamiri mno katika awamu hiyo.

Na miaka mitano ya marehemu Magufuli ilikuwa kipindi kibaya zaidi kwa Idara hiyo ambapo iligeuzwa kuwa kitengo binafsi cha usalama, ikashirikishwa kwenye unyama mbalimbali dhidi ya Watanzania iliyopaswa kuwatumikia, na pengine baya zaidi, ikajazwa maafisa wapya ambao kigezo chao pekee kujiunga na taasisi hiyo kilikuwa nasaba yako na marehemu Magufuli.

Kwahiyo, sisi wana-Idara wa zamani tunaweza kubaki watazamaji huku taasisi hiyo muhimu ikiangamia au tufanye kilicho stahili; kuingilia kati kuokoa japo kidogo kilichosalia.

Ni katika mantiki hii, nimelazimika kutupia jicho janga linaloweza kuugharimu urais wa Mama Samia Suluhu, janga la matusi mtandaoni. Najua kuna watakaoshauri apuuze tu, lakini ukweli kwamba yeye ni mwanamke, unamuweka katika mazingira magumu kupuuza matusi hayo.

Kuna watakaokwenda mbali na kutetea kuwa “mbona hata Magufuli alitukanwa?” lakini ukweli kwamba Magufuli alikuwa mwanaume, na Mama Samia ni mwanamke unafanya suala hili kuwa tofauti. Kadhalika, ikumbukwe kuwa yeye Magufuli mwenyewe mara kadhaa alitumia lugha isiyo ya kistaarabu ambayo kwa namna flani ilihalalisha matusi dhidi yake, japo ukweli ni kwamba matusi ni kitu kisichokubalika kwa namna yoyote ile.

Kuna mtu mmoja ambaye alianza kumtukana Mama Samia hata kabla hajawa Rais. Kibaya zaidi ni kwamba matusi hayo bado yapo mtandaoni. Ningetamani nisionyeshe hapa lakini sina jinsi.

Na kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, amempachika Mama Samia jina la JUMONG.

Jina hilo lina sababu kuu tatu. Ya kwanza ni kiu ya mtu huyo kuwa “bingwa wa kutunga majina yasiyopendeza kwa viongozi.” Alimuita Magufuli “Meko” na sasa angependa awe mwasisi wa “jina jipya” kwa Mama Samia.

Kuna wanaoweza kutetea kuwa “lakini Magufuli pia aliitwa Jiwe, na watu kadhaa ikiwa ni pamoja na wewe jasusi ulitumia jina hilo.” Ukweli ni kwamba Magufuli mwenyewe alijiita Jiwe.

Pili, jina hilo linatumika kumdhalilisha Mama Samia kwa kumfananisha na mhusika wa tamthilia ya Korea ya Jumong, kama kebehi kwa mavazi ya staha kabisa ya Mama Samia.

Sababu ya tatu inahusiana na nilichokigusia kwenye makala iliyopita kuhusu mkakati hatari wa kumchafua Mama Samia.

Kinachosikitisha kuhusu matusi na udhalilishaji anaofanyiwa Mama Samia ni ukweli kwamba kuna wanawake ambao sio tu wanayaona matusi hayo na udhalilishaji huo bali pia wanaunga mkono. Na baadhi yao walikuwa wahanga wa matusi na udhalilishaji uliokuwa ukifanywa na haramia mkubwa aliyefadhiliwa na utawala wa Magufuli, Musiba.

Lakini huyo mpenda matusi hajaanza kwa Mama Samia au Magufuli pekee. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, nae alikuwa miongoni mwa waliosemewa hovyo kama twiti zifuatazo zinavyoonyesha.

Unfortunately, Chadema “kwa kupenda siasa za harakati” imegeuka mtaji mkubwa wa huyu mtu. Licha ya kuwatusi huko nyuma kama twiti hizo hapo juu zinavyoonyesha, ana sapoti ya kutosha miongoni mwa wafuasi wa chama hicho.

Swali la msingi kwa Watanzania ni kwamba wataruhusu uhuni huu hadi lini? Musiba alipewa uhuru wa kutukana na kuchafua watu apendavyo lakini angalau yeye alikuwa anaungwa mkono na serikali iliyokuwepo madarakani. Kwamba pengine isingekuwa rahisi kuchukua hatua stahili dhidi yake. Lakini huyu mrithi wake ni mtu ambaye “jamii inaweza kummudu ikitaka.”

Hata hivyo, athari za uhalifu wa Musiba haziwezi kulinganishwa na na huyu mrithi wake. Wakati Musiba alikuwa na followers wachache tu mtandaoni kwa hiyo udhalilishaji na matusi yake havikuwafikia watu wengi sana, mrithi wake ana wafuasi takriban nusu milioni huko Twitter, na hiyo inamaanisha kuwa matusi na udhalilishaji anaofanya unafiki mbali sana.

Wakati nikitaraji serikali ya Mama Samia kuchukua hatua stahili dhidi ya “uanaharakati wa matusi” ni wajibu wa kila Mtanzania anayeitakia mema nchi yetu naye kuchukua hatua binafsi kukabiliana na uahalifu huu dhidi ya Rais wetu.