Catch-22 (Pasua Kichwa): Chadema Wakimpuuza Kigogo Atawaliza Lakini Wakimvalia Njuga Watadhihakiwa Wanamjadili Mtu Mmoja Twita. Kwahiyo Wafanyeje?

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kipo katika malumbano makali na Kigogo, ambaye hadi majuzi aliwaaminisha Chadema kuwa ni swahiba wao.

Hata hivyo, kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe, kumepelekea kuvunjika kwa uswahiba huo baada ya ushauri wa Kigogo kwa chama hicho kuwa “kiingie msituni” sio ulikataliwa bali pia ulielezwa na Makamu wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, kuwa ni “ushauri wa kijinga.”

Baada ya kauli hiyo, kama kawaida yake, Kigogo alitumia silaha yake maarufu ya matusi, hali iliyopelekea wafuasi wa Chadema, hususan Martin Maranja, kujibu mashambulizi.

Awali Kigogo alidai kuwa angeendelea kumuunga mkono Mbowe hata kama “ametelekezwa” na Chadema ( kwa kigezo cha chama hicho kukataa ushauri wake wa “kuingia msituni”)

Hata hivyo, hali imebadilika ambapo sasa mtu huyo anaidhihaki Chadema na kuiita “INTERAHAMWE.”

Na kashfa hizo zinaelekewa “kuwakuna” makada wa CCM,

Kwa kifupi hali iko hivyo.

Sasa jana kulikuwa na kipindi cha Clubhouse ya wana-Chadema kujadili suala hilo la ugomvi wao na Kigogo.

Apparently, Kigogo nae alishiriki kwenye “kipindi” hicho pengine bila kufahamika, kwa sababu wakati “kipindi” kinaendelea, yeye alikuwa anajibishana nao kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Na hapa ndio narejea kwenye kichwa cha habari cha makala hii.

Kwa upande mmoja, Chadema wakiendelea kupambana na Kigogo, kunaweza kujengeka hisia kuwa chama hicho “hakina ajenda muhimu hadi kinaparurana na mtu mmoja huko Twita.” Na kuthibitha hilo, tayari makada wa CCM wamedakia hoja hiyo.

Lakini kwa upande mwingine kunaweza kuwa na athari endapo Chadema wakiamua kukalia kimya jitihada za Kigogo kukichafua chama chao. Uongo una tabia moja muhimu: ukiukalia kimya unaweza kuonekana ukweli. Na uongo husambaa kwa kasi sana katika jamii inayoendekeza ubuyu. Na ubuyu ni mtaji muhimu wa Kigogo.

Kwa kiingereza, hali ya “nikifanya A inakuwa ovyo, nikifanya B pia inakuwa ovyo” huitwa “CATCH-22.” Katika hili cha Chadema na Kigogo, chama hicho kikimpuuza itakuwa shida, kikikabiliana nae yaweza pia kuwa shida.

CHADEMA WAFANYEJE?

Katika “catch-22 situations” moja ya options ni ile yenye athari chache kulinganisha na yenye athari kubwa. Ukilinganisha “athari za Chadema kudhihakiwa kuwa haina ajenda endapo itaamua kukabiliana na Kigogo” na “athari zinazoweza kutokana na Kigogo kuachwa afanye atakacho dhidi ya chama hicho” ni dhahiri kuwa kuchukua hatua ni muhimu kuliko kupuuzia.

Na busara hueleza kuwa tatizo haliondoki kwa kulidharau.

Pengine kweli Kigogo si maarufu kihivyo, lakini Chadema wenyewe wameshiriki kikamilifu kumfanya awe mtu wa kuaminika kwenye jamii.

Lakini pia japo watu wengi sasa wanamfahamu yeye ni nani, lakini bado anajificha mtandaoni ilhali Chadema wapo hadharani. Kwahiyo, ni rahisi kwake kusema lolote lile kwa sababu ni “anonymous” ilhali sio rahisi kwa Chadema kufanya hivyo.

Kadhalika, Kigogo kama mtu binafsi hana cha kupoteza akiichafua Chadema, lakini Chadema inaweza kushusha hadhi yake ikiamua, kwa mfano, kuingia kwenye vita ya matusi nae. Na mbinu hii amekuwa akiitumia Kigogo dhidi ya sie tunaojiheshimu mtandaoni. Anatutukana akijua kuwa hatuna uwezo wa kujibu matusi yake.

Hata hivyo, Chadema wanapaswa kufahamu kuwa Kigogo anatumia verified account, na Twitter inafahamu ID yake halisi. Kwahiyo, endapo ataendeleza matusi dhidi yao, kwa mfano hilo la kukiita chama hicho “Interahamwe,” basi wanaweza kuiripoti akaunti hiyo Twitter, na endapo watasiama kidete, basi inaweza kuwa suspended.

Madhara kwa Chadema kupuuzia kashfa hizo za Kigogo kuwa chama hicho ni cha kigaidi yanaweza kuwa makubwa kwa sababu licha ya kupaishwa na MATAGA, yanaweza kuathiri kundi muhimu kwenye siasa za Tanzania, yaani Watanzania wasio na vyama.

Jingine ambalo Chadema wanaweza kufanya ni kutumia raslimali watu. Chadema inaipiku CCM kwa kuwa na vijana smati. Na wengi wao wanamudu matumizi ya mtandao vizuri. Kwa hakika itakuwa ni fedheha kwa chama hicho kupelekeshwa na mtu mmoja, anayeficha ID yake.

Kampeni ya kushawishi wafuasi wa chama hicho wamu-unfolo Kigogo haiwezi kuwa na ufanisi kwa sababu asilimia kubwa ya wafuasi wa chama hicho, kama ilivyo Watanzania wengi, wanapenda ubuyu. Na Kigogo ana unlimited supply ya ubuyu, japo siku hizi anasuasua.

Nihitimishe kwa kuwakumbusha Chadema

Kuna mafunzo mawili muhimu kwa Chadema.

Kwanza, baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho walichekelea pale Kigogo alipofanya unyanyasaji dhidi ya watu wasio na hatia, nami jasusi/mtumishi wako nikiwa miongoni mwa wahanga wengi wa mpenda matusi huyu. Funzo hapa ni kwamba “mwenzio akinyolewa wewe tia maji.”

Pili, baadhi yetu tulitahadharisha kitambo kuhusu uswahiba kati ya chama hicho na “wanaharakati wa mtandaoni.” Kigogo ni mmoja tu wa wanaharakati hao. Japo hatuwezi kukipangia chama hicho nani wa kujiweka karibu nae na nani wa kumkwepa, ukweli ni kwamba hakuna mtu mwenye maslahi sawa na ya chama hicho zaidi ya chama chenyewe na wanachama wake. Ni muhimu sasa chama hicho kitafakari mahusiano yake na “wanaharakati wa mtandaoni” wengineo.

Jummah Mubarak!