Uswahiba Wa Chadema Na "Wanaharakati wa Mtandaoni" Na Mustakabali Wa Chama Hicho

Nianze makala hii kwa kutanabaisha mapema kwamba mimi sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa tangu mwaka 1995 nilipojiunga na utumishi serikalini. Kuanzia hapo sheria ilinikataza kujihusisha na siasa isipokuwa pale tu majukumu ya kikazi yalihitaji iwe hivyo.

Na tangu mahusiano yangu na kitengo yavunjike mwaka 2008, nimebaki Mtanzania tu, japo hadi mwaka 2015 nilikuwa nikiiunga mkono Chadema. In fact, mwaka 2010 nilishiriki kikamilifu kumpigia kampeni mgombea urais wa chama hicho Dkt Willibrord Slaa.

Sababu kuu ya kuiunga mkono Chadema ni ukweli kwamba ilishiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ufisadi, hususan mara tu baada ya serikali ya Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005.

Moja ya mafanikio makubwa kabisa ya Chadema yalikuwa ni kuibua skandali mbalimbali ambazo sio tu zilitikisa taifa bali pia zilipelekea matokeo mazuri. Moja ya mafanikio hayo ni lile la skandali ya Richmond, ambayo ilipelekea kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa.

Kadhalika, mawaziri kadhaa walilazimika kujiuzulu au walitolewa madarakani kutokana na mafanikio ya jitihada za Chadema kuibua ufisadi mbalimbali.

Yayumkinika kutanabaisha bila shaka kuwa mabadiliko makubwa, ambayo baadhi ya wachambuzi wa siasa wanayaona hasi, ni uamuzi wa chama hicho kumpokea Lowassa, mwanasiasa ambaye chama hicho kilimwandama kwa takriban miaka 9 mfulilizo kikimtuhumu kuwa ni “papa la ufisadi,” na kumpitisha kuwa mgombea wake kwenye nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ili kum- “accommodate” Lowassa, Chadema ililazimika kuachana na ajenda yake muhimu ya vita dhidi ya ufisadi. Isingewezekana kwa chama hicho kuendelea kupinga ufisadi ilhali mgombea wake kwenye nafasi ya urais wa JMT ni “mtuhumiwa nambari wani wa ufisadi,” huku chama hicho kikiwa ndicho hasa kilichoanzisha tuhuma hizo.

Chadema pia ililazimika “kulamba matapishi yake” kwa kuzunguka nchi nzima sio tu kumnadi Lowassa kama mgombea wake bali pia kumsafisha dhidi ya tuhuma za ufisadi ambazo kwa asilimia 99 ziliasisiwa na chama hicho.

Na tangu wakati huo, Chadema imeshindwa kuwa na ajenda ya kitaifa ukilinganisha na hiyo ya vita dhidi ya ufisadi ambayo sio tu iligusa nyoyo za Watanzania wengi bali pia iliwaaminisha watu wengi kuwa chama hicho kingeweza kabisa kuwa mbadala wa CCM.

Miaka kadhaa baadaye, Chadema imejikuta “ikirudia kosa ililofanya kwa Lowassa,” la kukumbatia “mtu mwenye maslahi binafsi.” Lowassa alijiunga na Chadema kwa ajili ya kusaka urais tu, na ndio maana muda mfupi baadaye aliamua kurudi CCM.

Hata hivyo, japo Chadema haijawahi kukiri hadharani kuwa ilifanya kosa kumpokea Lowassa na kumfanya mgombea wake katika nafasi ya urais wa JMT mwaka 2015, ukweli mwingine usioongewa ni kwamba mwanasiasa huyo alijiunga kwenye chama hicho akiwa na “lundo la mapandikizi” ambao baadhi yao walikuwa muhimu sana kwenye zoezi la “hamahama” kati ya mwaka 2015 na 2020.

Kosa linalorudiwa na Chadema wakati huu ni “ndoa ya mkeka” (marriage of convenience) kati ya chama hicho na the so-called “wanaharakati wa mtandaoni.”

Japo ni muhimu kwa chama cha siasa kujenga mahusiano na watu na makundi mbalimbali, lakini kigezo muhimu katika mahusiano hayo ni kutambua faida na hasara za mahusiano hayo, na kuangalia mzani unaelemea wapi.

Moja ya faida kwa Chadema kujiweka karibu na “wanaharakati” hao ni kupata sapoti mtandaoni, hasa kwa vile “wanaharakati” hao wana wafuasi wengi mtandaoni. Hata hivyo, wengi wa wafuasi wa wanaharakati hao ni wafuasi pia wa Chama hicho, ikimaanisha kuwa kinaweza kusimama chenyewe bila kuhitaji sapoti ya “wanaharakati” hao.

Lakini kwa upande wa “wanaharakati” hao, uhusiano huo una manufaa makubwa sana kwani unawasaidia kufanya kampeni zao mbalimbali kwa kuwatumia wafuasi wa chama hicho. Hoja zao zimekuwa zikisambazwa zaidi na wafuasi wa chama hicho.

Hata hivyo, moja ya hasara kwa Chadema ni ukweli kwamba hakiwezi kukwepa kuhusishwa na “mabaya” ya “wanaharakati” hao. Kwa mfano, mmoja wa “wanaharakati” hao anayejiita Kigogo amekuwa mstari wa mbele kumtukana Mama Samia Suluhu takriban kila kukicha.

Japo Chadema kama chama hakijawi kumtukana Mama Samia bayana, uswahiba wao na “bingwa huyo wa matusi” unakifanya chama hicho kuwa “guilty by association.”

Hoja ni kwamba, japo chama hicho kinaweza kabisa kumkemea mtu huyo na kumsihi atumie lugha ya kistaarabu, lakini kimeamua kukaa kimya. Kadhalika, chama kingeweza kujiweka kando na “mtu huyo mwenye wasifu wenye walakini” hasa kwa sababu “anguko lake” linaweza pia kukiathiri pia chama hicho.

Ombwe linalotokana na ukosefu wa ajenda limechangia pia kukifanya chama hicho kuwa, kwa upande mmoja, kinachodandia hoja za wanaharakati, na kwa upande mwingine, kuwa “chama cha kiharakati” zaidi kuliko “chama cha siasa.”

Japo si makosa kwa chama cha siasa kujihusisha na harakati mbalimbali, chama kinachogeuka “cha kiuanaharakati” kinajitengenezea nafasi finyu ya kukamata madaraka.

Kibaya zaidi, kwa sasa, ni ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa “wanaharakati wa mtandaoni” ni kama wamepora uongozi wa chama hicho na kukifanya kitumike kunadi hoja za “wanaharakati” hao badala ya sera za chama.

Mfano hai ni katika suala la msanii Diamond Platnumz kuteuliwa kuwania Tuzo za BET 2021. Ushawishi wa “wanaharakati wa mtandaoni” dhidi ya msanii huyo - kwa madai kuwa ni mshirika wa CCM katika ukandamizwaji wa Watanzania - umepelekea viongozi kadhaa waandamizi wa chama hicho kutamka hadharani kuwa hawamuungi mkono msanii huyo anayeiwakilisha Tanzania.

Japo hakuna sheria inayokilazimisha chama hicho kumuunga mkono msanii huyo, ni rahisi kwa “maadui wa Chadema” kutumia suala hilo kama ushahidi kuwa chama hicho ni “cha kibaguzi” na “kinaendekeza visasi na siasa za chuki.”

Kwamba wengi wa “wanaharakati wa mtandaoni” wapo karibu na chama hicho kwa maslahi binafsi sio siri. Baadhi sio tu walishiriki kampeni endelevu za matusi dhidi ya chama hicho bali pia walifanya kampeni dhidi ya chama hicho.

Licha ya udhalilishaji huu wa wazi, “mwanaharakati” huyo sasa anajinasibu kuwa “anaipenda Chadema.”

Nihitimishe makala hii kwa kutanabaisha kuwa “uswahiba huu wa kutumiana” una mwisho mmoja tu: mbaya.

Hilo la baadhi ya viongozi wa Chadema kushirikiana na “wanaharakati wa mtandaoni” dhidi ya Diamond litakiathiri zaidi chama hicho kuliko msanii huyo au hao “wanaharakati” ambao “hawana cha kupoteza” katika kampeni hiyo.

Naam, sio tu kuwa Diamond ana mapungufu yake lakini ni kweli pia kuwa kundi aliloteuliwa kuwania tuzo hizo za BET ni gumu. Japo ni msanii maarufu duniani, lakini bado hajafikia kiwango cha Burna Boy au Wizkid wa Nigeria, kwa mfano, ambao wanachuana nae katika kundi la msanii bora wa kimataifa.

Lakini hata Diamond asipofanikiwa kushinda Tuzo hiyo, bado atakuwa ameiwakilisha vema Tanzania kimataifa. Na ni rahisi kwa Watanzania wengi kutafsiri kuwa “waliompinga waliipinga Tanzania pia” japo kila mtu ana haki ya kumpinga au kumsapoti msanii huyo.

Natambua makala hii itawakera baadhi ya wasomaji lakini huwa sijui kuandika vitu vya kumpendeza kila mtu na badala yake dhamira yangu ni kuhabarisha na/au kuelimisha.