Asante Mheshimiwa Zitto kwa Maoni Yako Kuhusu Sekta ya Umeme, Mjiskie Aibu Mlotumia Lugha Isiyo ya Kistaarabu Kujibu Maoni Hayo.

Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa mchango wa Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa maoni yake kufuatia bandiko langu la jana kwenye kijarida hiki lililokuwa na kichwa cha habari “Tanesco Inahujumiwa. January Makamba Anahujumiwa. Mama Samia Pia Anahujumiwa by Proxy.

Kwa upande mmoja, kwa mwanasiasa mwenye wadhifa mkubwa kitaifa kama yeye kuchukua muda wake kusoma chapisho hilo na hatimaye kutoa maoni yake makes me feel quite privileged.

Kwa upande mwingine, inapendeza kuona wanasiasa kama Mheshimiwa Zitto wakishiriki kwenye mijadala muhimu kwa mustakabali wa taifa letu.

Na kama alivyo Waziri January Makamba huko CCM, kwa upande wa Upinzani, Mheshimiwa Zitto ni the most interactive politician, “anajichanganya” (mingling) na kila mtu bila kubagua. Kwa bahati mbaya, ukaribu aliojenga Mheshimiwa Zitto na takriban kila Mtanzania, hususan mtandaoni, umemfanya kuwa mmoja wa wanasiasa wanaotukanwa sana. Halafu bado tutawalaumu waheshimiwa wakiamua kujiweka mbali nasi?

Kwa bahati mbaya zaidi - pengine makusudi - baadhi ya waliotoa maoni yao kufuatia maoni ya Mheshimiwa Zitto walitumia lugha isiyo ya kistaarabu, ikiwa ni pamoja na matusi.

Matusi ni janga kama ubuyu. Janga hili linaathiri sana maongezi kwenye mitandao ya kijamii. Mara kadhaa nimepokea ujumbe kutoka kwa watu mbalimbali wanaoeleza kuwa japo wameguswa na mada, wanashindwa kutoa maoni yao kwa kuchelewa kutukanwa.

Janga la matusi linachangiwa na sababu kuu mbili. Ya kwanza ni akili duni. Takriban kila mtu anayejihusisha na matusi mtandaoni au hata mtaani, ana mapungufu ya kiakili. Kwao, matusi ni sawa na mkongojo wa kuwawezesha kufikisha ujumbe wao.

Sababu ya pili ni chembechembe za udikteta zinazotawala vichwani mwa baadhi ya Watanzania. Utakuta watu ni wepesi kulaumu “udikteta wa watawala wetu” ilhali nao wanafanya udikteta pindi wakikutana na hoja wasizoafikiana nazo.

Na hawa wapenda matusi huwa wa kwanza kulalamika wanapopigwa bloku.

Nihitimishe kwa kumshukuru tena Mheshimiwa Zitto na mchango wake wa maoni na ninawalaani vikali wote waliomjibu kwa lugha isiyo ya kistaarabu ikiwa ni pamoja na kutumia matusi. Twaweza kutofautiana kimtazamo pasi haja ya kutoboana macho.

Siku njema