Tanesco Inahujumiwa. January Makamba Anahujumiwa. Mama Samia Pia Anahujumiwa "By Proxy."

Kwamba Tanesco inahujumiwa sio suala linalohitaji mjadala. Labda tunachoweza kujadili - na sio hapa - ni upana/ukubwa wa hujuma husika.

Kujadili upana wa hujuma dhidi ya Tanesco kunahitaji makala ndefu, pengine kijitabu kabisa. Hilo linawezekana, lakini kwa faida ya nani? Niwe mkweli, kadri siku zinavyokwenda, nahisi kama hizi kelele zetu wengine kupitia kwenye maandishi ni kama kutwanga maji kwenye kinu. Au kumpigia mbuzi gitaa, ni kupoteza muda na kumuudhi mbuzi.

Kilichobaki kwetu “wapiga kelele wa dhati” (sio hao wanaopaza sauti na kufanya ‘hashtag for pay’ huko mtandaoni) ni kuandika/kuongea pale tu tunapojiskia kuongea/kuandika. Kama hobby vile.

No, sio kukata tamaa bali kuwa realistic. Kwenye stadi za siasa kuna kitu kinaitwa Realpolitik, yaani siasa zinazojikita kwenye uhalisia kuliko maadili au itikadi. Na kwenye diplomasia/mahusiano ya kimataifa (diplomacy/international relations) kuna kitu kinaitwa realism, ambacho kwa tafsiri nyepesi ni kanuni inayojikita kueleza mahusiano ya kimataifa kwa kuzingatia uhalisia. Kwa mantiki hiyohiyo, “wapiga kelele” tunapokubali matokeo kuwa kelele ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu/kumpigia mbuzi gitaa ni kukubali ukweli na sio kukata tamaa. Kuondoka feri baada ya kusubiri “daladala ya kwenda Pemba” (which doesn’t exist) sio kukata tamaa bali ni kuzingatia uhalisia.

Enewei, nisiwachanganye, twende kwenye mada husika.

Nimeshatanabaisha hapo juu kuwa Tanesco inahujumiwa. Na mgao wa umeme au kila linalokukera muda huu kuhusu Tanesco na sekta ya umeme kwa ujumla linachangiwa zaidi na hujuma kuliko sababu za kiunfundi.

Waziri mwenye dhamana kuhusu Tanesco/umeme ni January Makamba, mwanasiasa ambaye yayumkinika kumtaja pasi shaka kuwa ndiye mwenye “haiba kisiasa” kuliko yeyote yule. Kwa bahati mbaya , sifa hii ambayo sio kosa lake pia inamtengenezea lundo la maadui.

Unfortunately, tunaishi katika dunia ambapo mtu akiwa mwema, mwenye utu, msikivu, asiyejikweza…kwa kifupi “mtu kweli kweli,” ni kama kosa la jinai. Ndio maana baadhi ya watu wanaona bora kuwa na roho mbaya kwa sababu “kuwa mwema ni kama kubeba lumbesa la misumari.” Na hii ni moja ya changamoto kwa January. Kuna watu wengi tu wangependa kuona mwanasiasa huyo “akiishi kama mwanasiasa wa Kitanzania,” awe na dharau, ajiweke mbali na watu wasio na faida kwake, asitumie mitandao ya kijamii isipokuwa kwenye kusaka ujiko tu…” Most of watu hao ni wanasiasa wenzie, ndani na nje ya CCM.

Na kumsifia January kuna changamoto zake. Kutokana na utu/wema wake, amezungukwa na mamilioni ya washauri, wa kweli na wanaohangaikia maslahi yao. Na watu hao humtazama kila anyejaribu kumpongeza au kumshauri January kuwa ni adui kwao, kama kwamba ukaribu wa January kwa hao wanaojaribu kumshauri utaathiri maslahi yao. Kwahiyo, sintoshangaa makala hii ikiishia kuhukumiwa kuwani jitihada za kujipendekeza. After all, “sie wengine” hatupaswi kupongeza wanasiasa wa CCM, kwa mujibu wa “wenye chama chao/nchi yao.”

Kama ambavyo kujadili hujuma dhidi ya Tanesco kwahitaji makala nzima au pengine kijitabu kabisa, ndivyo pia ilivyo kwenye “hujuma dhidi ya January.” Hata hivyo, hapa nitajikita zaidi kwenye hujuma dhidi yake baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati.

Ili kuelewa hali ilivyo muda huu, ni vema kurejea hali ilivyokuwa zama za Magufuli, mwanasiasa dhaifu aliyedhani kuwa kila “mwanasiasa anayependwa na watu” ni tishio kwake. Hatupaswi kumsema vibaya marehemu lakini yayumkinika kumtaja kama the most paranoid politician katika historia ya Tanzania.

Magufuli alianza kumhofia January hata kabla hajaapishwa kuwa Rais wa tano wa Tanzania. Sababu kuu ilikuwa kwamba laiti “mahesabu ya kisiasa” yangeenda vema, January na si Magufuli ndiye angekuwa Rais wetu mwaka 2015. Kilichomponza January ni hofu ya Kikwete kwamba mwanasiasa huyo kijana angeweza kutumika “kumrudisha Lowassa kwa mlango wa nyuma.” Ikumbukwe tu kuwa uchaguzi wa 2015 kwa CCM ulikuwa all about Jk vs swahiba wake wa zamani Lowassa. Na Magufuli aliukwaa urais kwenye upenyo huo.

Huku takriban kila mtu akitarajia kuwa Magufuli angemteua January kuwa Waziri Mkuu au Waziri wa Mambo ya Nje kutokana na mchango usiomithilika wa January katika kampeni za Magufuli, kabineti ya Magufuli iliotangazwa ikawa kinyume kabisa na matarajio ya wengi. January akapewa wizara isiyoendana na hadhi yake. Na baadaye Magufuli akamtoa January kwenye kabineti yake baada ya kumtumia “haramia wake Musiba” kujenga taswira kuwa January, pamoja na baba yake Mzee Makamba, Kinana, Ngeleja, Nape na Membe wanamhujumu Magufuli.

Uamuzi wa Mama Samia kumteua January kuwa Waziri wa wizara nyeti ya nishati ulitarajiwa kuwakera mahasimu wa both Mama Samia na hususan mahasimu wa January. Lakini ukweli kwamba aliyeondolewa kwenye uwaziri wa nishati ni Dkt Medard Kalemani, mmoja ya wanasiasa ambao sio tu walikuwa karibu kabisa wa Magufuli, bali pia ni mbunge wa jimbo la Chato, anakotoka Magufuli.

Kwa bahati mbaya, kama ilivyo kwa Mama Samia ambaye amerithi serikali iliyokuwa ikiendeshwa kama taasisi ya mtu binafsi, ndivyo ambavyo January amerithi Wizara ya Nishati. Hujuma dhidi ya Tanesco kati ya 2015 Magufuli alipoingia madarakani hadi mapema mwaka huu Magufuli apofariki ni kubwa kama ilivyo kwenye taasisi nyingine mbalimbali za serikali. Usiri mkubwa uliotawala utawala wa Magufuli, ukiambatana na hatua kali dhidi ya yeyote aliyeonekana tishio kwa utawala huo, ulisaidia sana kuficha lundo na mapungufu ya utawala huo ikiwa ni pamoja na ufisadi mkubwa ambao hopefully Watanzania watapewa haki ya kuufahamu.

Kama kuna kosa January amefanya ni kutomuiga Magufuli “kuonyesha mapungufu aliyoyakuta.” Yes, kama unakumbuka vema hotuba ya Magufuli wakati anazindua Bunge, ilikuwa kama litania ya madudu ya utawala wa Kikwete. Na Watanzania awali waliridhia “hatua za kidikteta” za Magufuli kwa vile zilionekana kama ndio njia pekee ya kuondoa madudu aliyoyakuta.

January alipaswa kuwaeleza Watanzania madudu aliyoyakuta katika Wizara hiyo, na baadaye kuwaeleza Watanzania jinsi gani atasafisha madudu hayo. Kinyume chake ni kwamba madudu aliyoyarithi yanaweza kutafsiriwa kuwa ni mapungufu yake yeye aliyeyarithi.

Ukizunguka mtandaoni unaweza kudhani kuwa “ghafla baada ya January kuingia madarakani, Tanesco imekuwa ovyo kabisa” kwa jinsi kunafanyika jitihada kubwa kumbebesha lawama mwanasiasa huyo kwa makosa ambayo japo yapo lakini hajayasababisha.

Lakini kuna kundi jingine linalomhujumu January. Ni watumishi wasio waadilifu wa shirika hilo ambao wameathiriwa na hatua za awali alizochukua January kuirekebisha Tanesco. Ukipita mtandaoni hutoshindwa kuona mabandiko ya baadhi ya watumishi hao “wakimtisha waziwazi January” kwa “kosa la kuwaondoa kwenye nyadhifa zao.”

Kuna jingine lisilohusiana na Tanesco/sekta ya umeme. Ni urais. Kuna hisia japo si kubwa kwa sasa kuwa “January anaandaliwa kuwa mrithi wa Mama Samia.” Iwe ni mwaka 2025 endapo Mama Samia ataamua kupumzika, au 2030 ambapo mihula yake miwili itakuwa imemalizika.

Kwahiyo kwa “wabaya wa January,” mwanasiasa huyo “akilikoroga huko Wizara ya Nishati/Tanesco, atakuwa hana nafasi tena kwenye kipute cha kuwania urais 2025 au 2030.” Katika hili, baadhi ya wanaotajwa kumhujumu ni pamoja na mawaziri wenzake wenye ndoto za urais.

Hujuma dhidi ya January ni dhidi ya Mama Samia by proxy. Kwa upande mmoja, wenye dhamira ya kuona Mama Samia anakwama “watapata la kusema” endapo “kijana wake” (January) “atalikoroga.” Na ukipita huko na kule, utabaini kuwa “wameshaanza kuongea.” Moja ya mada zinazo-trend kwenye majukwaa mbalimbali ya maongezi ya Watanzania, hususan “wafuasi wa Magufuli” ni “mapungufu ya Mama Samia vs mema ya Magufuli/ mapungufu ya January vs mema ya Kalemani.” Na kuna wanaoshindwa kuficha hisia zao na kutamka bayana wanaombea “Mama Samia na kijana wake January” wafeli mapema.

Nihitimishe kwa kutanabaisha kuwa naamini kwa dhati kuwa January ni mtu sahihi kwenye nafasi hiyo, japo laiti ingekuwa chaguo langu, nafasi mwafaka zaidi kwake ilikuwa kwenye ukurugenzi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa. Kwa sababu moja kuu: ana akili (intelligence) kubwa mno. Na “ana sifa nyingine” zinazotosha kumfanya perfect person kushika wadhifa huo. Kwa sababu what Mama Samia needs most kwa sasa ni intelijensia isiyo na mawaa, ya kuwambia “hapa umekosea Mama,” au “hapa fanya hivi,” lakini pia isiyosita kuafiki mtazamo wake endapo upo sahihi. Wahuni waliopo wanamhujumu mchana kweupe lakini only her knows kwanini hadi muda huu Diwani bado ni DGIS.

Again, nani anajali kuhusu hayo niliyoandika hapo juu? Unfortunately hii ndo Tanzania yetu, na sie ndo watu wake.

Siku njema