Wikiendi ya mwisho kwa mwaka 2019: Ningependa kusikia maoni yako

Leo ni Jumamosi/wikiendi ya mwisho kwa mwaka huu 2019. Pengine ni wakati kama wakati mwingine, lakini moja ya mbinu muhimu katika maisha ni kuuangalia kila wakati kama muujiza flani ambao kamwe hautojirudia. Naam, kamwe hakutokuwa na tarehe 28.12.2019. Never. Ever!

Moja ya mambo nayojivunia kuyafanya mwaka huu ni pamoja na kuendeleza jukumu nililoanza zaidi ya miaka 20 iliyopita, la kuitumikia jamii kupitia maandishi.

Na kinachonipa faraja zaidi sio kuendelea kuandika tu bali pia “kukua kiuandishi.”

Hivi wajua nilianza uandishi kwenye gazeti la kwanza la udaku Tanzania lililokuwa linaitwa SANIFU?

Hiyo ilikuwa mwaka 1997-1998, na aliyenishauri kuwa mwandishi ni mmoja wa waandishi bora kabisa katika historia ya Tanzania, Albert Memba - mmoja wa waandishi wachache kabisa wanaomudu kuandika habari/makala kwa kimombo.

Memba alikuwa mwaka mmoja nyuma yangu pale Mlimani (UDSM). Nilianza kutuma habari za udaku kwenye gazeti hilo la SANIFU ambalo lilikuwa hot cake, enzi hizo hata Shigongo hajaanzisha magazeti yake ya udaku.

Baadaye nikaandikia magazeti mengine mwili ya udaku - KASHESHE na KOMESHA.

And guess what? Safu yangu iliyokuwa maarufu vya kutosha kwenye magazeti hayo ya udaku ilikuwa ya “Ustaadh Bonge” - mnajimu wa nyota za kuchekesha. Kichekesho ni kwamba baadhi ya watu waliamini nyota hizo.

Baadaye nikaamua kuhamia kwenye “uandishi makini,” nikaanza kuandika makala kwenye magazeti ya KULIKONI (nilikuwa mmoja wa wanamakala waasisi), MTANZANIA na baadaye RAIA MWEMA (nikiwa pia mmoja wa wanamakala waasisi wa jarida hilo).

Mwaka 2006 nilianzisha blogu yangu ya KULIKONI UGHAIBUNI ambayo kwa mwaka huu nimekuwa mzembe kui-update.

“Kukua” kwangu kiuandishi ni kutoka kwenye uandishi kwenye magazeti ya udaku hadi kwenye magazeti makini na kublogu, na kutoka kwenye “makelele ya siasa” na kuwekeza nguvu zaidi katika kuwa mtumishi wa watu kupitia uandishi wa mada za kuwajengea watu uwezo - personal development na cybersecurity, maeneo mwili ninayoyapa kipaumbele kikubwa kwa sasa. Sambamba na uandishi wa makala ni uchapishaji vitabu.

Kuwatumikia Watanzania sio kazi rahisi, na hapa simaanishi matusi nayotumiwa kila kukicha na “waungwana” mbalimbali. Jitihada za kuwahamasisha Watanzania wajikite zaidi kwenye masuala muhimu badala ya UBUYU hazijazaa matunda vya kutosha. Na wala sina hakika kama jitihada hizo zitafanikiwa.

Ningependa sana kuendelea watumikia watu wengi mbalimbali na pengine wengi zaidi kupitia uandishi wa makala hasa katika maeneo hayo mawili - personal development na cybersecurity. Lakini kwa vile haikuwa rahisi katika mwaka huu 2019, pengine ni vema kupata ushauri kutoka kwenu. Ningependa kusikia kutoka kwako kuhusu. NIANDIKIE HAPA

(a) Nini kilikukera kutoka kwangu

(b) Nini kifanyike kuboresha utumishi huu

Nimalizie na tangazo la vitabu vyangu (hoping you wouldn't mind)

Nawatakia kila la heri kwa mwaka ujao wa 2020.

Ndimi mtumishi wenu,

Evarist Chahali