Wiki Hii Tunapanua Wigo wa Mada Zaidi ya "Kupiga Politiki"

Tuongee Kuhusu UKIMWI (Tafadhali Usikimbie 😁😁😁)

Majuzi nilipokea pongezi na maoni kutoka kwa mdau mmoja wa #BaruaYaChahali. Alipongeza jitihada zangu kuwatumia kijarida hicho kila wiki hata kama nikichelewa kukituma Jumatatu.

Hata hivyo, alishauri kwamba nipanue wigo wa mada, ambapo badala ya kila wiki kuwa siasa tu, niangalie uwezekano wa kuwawekea mada nyingine zisizohusu siasa.

Nadhani hili ni wazo zuri. Na si kwamba ku-focus kwenye siasa tu ni kosa bali ni ukweli usiofichika kuwa kuna masuala mengine mbalimbali yasiyo ya kisiasa ambayo yanastahili kupewa attention yetu pia.

Lakini kuna sababu nyingine ambayo huko nyuma ilishanifanya "niachane na siasa." Ni silika ya Watanzania takribani wote. Haijalishi mwanaharakati ajitoe kwa kiasi gani kutetea Tanzania yetu au kuwatetea wanyonge, mapokeo ni duni mno kiasi kwamba yayumkinika kuhitimisha kwamba moja ya shughuli zinazoweza kuwa katika daraja la juu kupoteza muda ni "kupiga kelele kuhusu siasa za Tanzania yetu."

Mei mwaka juzi 2017 niliamua kuachana na uandishi wa makala "za kiuanaharakati wa siasa" katika gazeti maarufu la kila wiki la Raia Mwema. Sababu kuu ya kuchukua uamuzi huo ilikuwa usaliti niliofanyiwa na gazeti hilo.

Awali nilibandika "future tweet" hii huko Twitter

na ikazua kasheshe kubwa hadi kufikia hatua ya Waziri Mwakyembe kukanusha nilichoandika.

Tatizo la Mwakyembe na waliomshauri ni kutoelewa maana ya "future tweet," tweet ya kufikirika ambayo japo inaweza kuwa ni ubashiri wa dhati, inalenga zaidi kuburudisha (humorous tweet).

Angalia mifano hii ya "future tweets" zangu ambazo huambatana na alama ya reli #FutureTweet

Kilichonisikitisha kuhusu jamaa wa Raia Mwema ni ukweli kwamba walisumbuliwa na vyombo vya dola kuhusu mie/tweet hiyo lakini sio tu hawakuona umuhimu wa kuandika habari hiyo gazetini mwao bali pia wakapuuzia kunieleza kuhusu tukio hilo. Kanuni muhimu kabisa ya uanahabari ni "ukimbugudhi mmoja wetu umetubugudhi sote." Lakini hao wahuni walipuuzia hilo licha ya kuwa nao tangu gazeti hilo linaanzishwa

Lakini Mungu hamfichi mnafiki, muda mfupi baadaye gazeti hilo lilijikuta lilifungiwa

Agosti mwaka jana, nililazimika kuchukua uamuzi mwingine dhidi ya "utumishi wangu wa hiari kwa Watanzania" kwa kuamua kuchukua mapumziko kwenye "kupiga kelele za siasa."

Uamuzi huu ulichangiwa zaidi na ukweli kwamba sikuwa ninapata sapoti yoyote ile katika "kupiga kelele hizo za siasa" ilhali kelele hizo zilikuwa zikihatarisha zaidi maisha yangu ambayo hata kabla ya hapo yalishakuwa hatarini.

Anyway, wiki hii ninawaletea mada isiyohusiana na siasa. Inahusu masuala ya afya. Lakini kabla ya kuingia kwenye mada hii ngoja nikupe background kidogo.

Sikumbuki ni mwaka gani ila nachokumbuka ni kwamba nilikuwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi, ambapo binamu yangu mmoja aliletwa nyumbani Ifakara kutoka Dar akiwa mahututi. Nakumbuka kila nilipouliza kuhusu maradhi yake nilipewa majibu yasiyoeleweka. Pia nakumbuka nilionywa kuwa nikienda kumuona hospitali nisigusane nae wala kugusa kitu chake chochote.

Licha ya binamu yangu huyo kuwa mwenye mwili mdogo, lakini maradhi hayo yalifanya awe mdogo zaidi kama mtoto. Alikuwa amekongoroka kwelikweli. Na kila kukicha sio tu hali yake ilizidi kuwa mbaya bali pia alizidi kukongoroka.

Hatimaye alifariki japo msiba wake uliambatana na tahadhari kubwa kutogusa kitu chochote kuhusiana na binamu yangu huyo.

Miaka kadhaa baadaye nilikuja kufahamu kuwa binamu yangu huyo alikuwa mwathirika wa ukimwi, maradhi ambayo baadaye yalipelekea kifo chake.

Bado nina kumbukumbu kubwa ya mateso aliyokuwa akiyapata ndugu yangu huyo kabla ya kufariki.

Miaka kadhaa baadaye, nikiwa hapa Uskochi nilipata tenda moja ya usadi ya kufanya kazi na charity moja inayojihusisha na masuala ya ukimwi. Hii ilikuwa fursa nzuri kwangu sio tu kufahamu zaidi kuhusu maradhi hayo bali pia kukutana na waathirika wa ugonjwa huo. Hata hivyo, ni vigumu sana kuongelea ukimwi kwa sababu “waswahili hawapendi kusikia habari mbaya.”

Kuna mambo kadhaa niliyojifunza kupitia usadi wangu kwenye charity hiyo.Baadhi ya mambo hayo ni kama ifuatavyo:

1. Historia ya ukimwi inatisha. Katika siku za mwanzo baada ya kugundulika ugonjwa huo sio tu hakukuwa na dawa bali pia jamii ilitafsiri kuwa ukimwi = kifo. Na jamii ilikuwa na kila sababu ya kutafsiri hivyo kwani ukimwi uliteketeza watu wengi mno.

2. Katika zama hizo, waathirika waliteseka mno. Kwanza, dawa zilizotumika kupunguza makali ya ugonjwa huo zilihitaji mgonjwa anywe lundo la vidonge kwa siku. Lakini pia miongoni mwa dawa hizo zilikuwa na athari kubwa (side effects) ambapo baadhi ziliua waathirika fasta kuliko ukimwi.

3. Kwamba miaka kadhaa baadaye, zama hizi tulizonazo, sio tu kuwa ukimwi haumaanishi "hukumu ya kifo" (kwa maana ya kwamba asilimia kubwa ya ya waathirika wanaishi muda mrefu kama wasioathirika) bali pia maradhi hayo yanadhibitika (sio kupona) kwa kiasi kikubwa na dawa za kisasa za kukabiliana na virusi vya ugonjwa huo.

4. Kwamba jitihada kubwa za wanasayansi zimepelekea hatua tatu muhimu kuhusu ugonjwa huo. Kwanza, ni uwezo wa dawa kudhibiti virusi vya ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa hadi kufikia mahala mgonjwa anakuwa kama hana virusi (vipo lakini havina nguvu), hali ambayo kitabibu inaitwa "undetectable."

Pili, uwezo wa dawa hizo kumfanya mwathirika "kuwa kama hana virusi" (undetectable) unapeleka uwezekano wa mwathirika kufanya tendo la ndoa na mtu ambaye hajaathirika, bila kumuambukiza virusi hivyo.

Tatu, dawa hizo zinaweza kutumiwa na mtu asiyeathirika kuzuwia asiambukizwe pindi akifanya tendo la ndoa na mtu aliyeathirika bila kutumia kinga. Dawa za aina hiyo zinaitwa PrEP.

Hata hivyo, licha ya jitihada kubwa za wanasayansi, bado hakuna tiba ya ukimwi. Na licha ya maradhi hayo kutokuwa "hukumu ya kifo" ukilinganisha na siku za awali, bado ukimwi unaua, hususan katika nchi masikini na kuchangiwa pia na watu wanaodhani kutumia dawa za kupunguza makali ya maradhi hayo ni ruksa ya kufanya ngono zembe.

Kumekuwa na jitihada kubwa za kusaka tiba ya ukimwi. Majuzi, kumetokea maendeleo makubwa zaidi katika jitihada hizo ambapo majaribio ya kisayansi yaliyofanyika nchini Marekani yamefanikiwa kuangamiza virusi vya ugonjwa huo.

Ungana nami wiki ijayo ambapo nitakueleza kwa undani kuhusu majaribio hayo, na -kikubwa zaidi- kwanini yanaleta natumaini kwa mamilioni ya waathirika wa ukimwi duniani. Maradhi haya yana sifa moja kuu, inayoekezeka vema kwa kimombo, "if you are not infected, you are still affected," kwamba hata kama wewe si mwathirika, lazima umeathiriwa na ndugu, jamaa au rafiki anayeumwa au aliyefariki kwa ukimwi (kama huyo marehemu binamu yangu #RIP).

Nakutakia siku na wiki njema. Tukutane Jumatatu ijayo

Mtumishi wako #EvaristChahali