Watu Wasiojulikana Wajitokeza Hadharani

Afisa Usalama Kumtisha Zitto Kabwe Ni Mwanzo Tu wa Yajayo

Je upo kwenye mitandao ya kijamii mingapi? Mie nipo sehemu nyingi lakini ninayoitembelea kila siku (kutoka naotembelea sana to ninaotembelea sio sana) ni Twitter, Insta, Facebook, Jamii Forums, Reddit na Medium. Nipo pia huko LinkedIn, Pinterest, Google+, Blogger, Wordpress, nk japo siendi huko kila siku.

Kwanini Twitter sana? Kwa sababu mtandao huo wa kijamii ni kama chombo cha habari. Na watu mbalimbali wamekuwa wakiutumia kutoa matamko/taarifa mbalimbali.

Na Ijumaa Januari 18, kupitia mtandao huo wa kijamii, Kiongozi Mkuu wa Chadema cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe alitwiti kwamba ametishiwa maisha na Afisa Usalama wa Taifa akiwa Bungeni Dodoma.

Unaweza kudhani hizi ni porojo tu za kisiasa. Hapana. Baadhi yetu tumeshwahi kukumbana na kadhia kama hizi, si mara moja, au mara mbili, bali mara kadhaa kwa miaka kadhaa. Na waweza kupuuzia kuwa “hawawezi kunifanya lolote” kisha “ukapotezwa” kama Ben Saanane. Au wakataka kukuua kama Tundu Lissu. Au wakakubambikia kesi kama Sugu, na sasa Mbowe na Matiko.

Waweza kujidanganya kuwa “mie nani hasa mpaka hao mbwa wa Usalama wa Taifa wanitishie uhai?” Ukweli mchungu ni kwamba, kama wanaweza kumtishia Mbunge kama Zitto ambaye ni sio tu ni mwanasiasa mwenye jina kubwa bali pia ni Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, wewe mwenzangu na mimi ni nani hasa usibughudhiwe?

Hoja yangu hapa ni kwamba, kama wanaweza kufanya hivyo kwa mtu muhimu kama huyo, kwanini washindwe kufanya hivyo kwako?

Ndio hivyo tena, hatimaye “Watu Wasiojulikana” wamejitokeza hadharani. Ama kwa hakika yajayo yanatafakarisha.

Tukutane wiki ijayo.

Take care!

Evarist

Nilikuwa nimemaliza kuandika barua hii kwenu lakini kabla sijaituma kwako, nikakumbana na kituko cha karne. Kituko hiki kitabaki kwenye historia ya taifa letu MILELE.

Naomba nisiongee sana, niweke kiporo hadi wiki ijayo, kwani nahisi kati ya sasa na wiki ijayo kuna mengi ya kujadili.