Upinzani Washinda Urais Malawi. Je Yawezekana Kwa Upinzani Wetu Hapo Oktoba?

Juzi nilitwiti

Bonyeza twiti hiyo ili uweze kusoma maoni ya wadau mbalimbali.

Nawe ukijiksia, wakaribishwa kuchangia maoni yako.

Lakini kabla ya kugusia sehemu ya pili ya kichwa cha habari - “Je Yawezekana Kwa Upinzani Wetu Hapo Oktoba - nikupatie maelezo mafupi kwanini Malawi ililazimika kufanya uchaguzi mwingine licha ya ule wa mwaka jana uliomtangaza Rais aliyekuwepo madarakani, Peter Mutharika kuwa mshindi.

Ni kwamba Malawi ilifanya uchaguzi mkuu Mei 21 mwaka jana, Mutharika alishinda kwa asilimia 38.57 mbele kidogo tu ya Lazarus Chakwera aliyepata asilimia 35.41 na Saulos Chilima asilima 20. Mutharika aliapishwa Mei 27.

Anglican bishop tells Mutharika, Chakwera, Chilima to hold ...

Ushindi huo ulimaanisha muhula wa pili kwa Mutharika baada ya kushinda urais kwa mara ya kwanza mwaka 2014. Kabla ya hapo, aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2009 na kuteuliwa na kaka yake, marehemu Bingu wa Mutharika aliyekuwa rais wakati huo, kuwa Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,. kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwaka 2011.

Mwaka mmoja baadaye, Rais (Bingu) Mutharika alifariki, na nafasi yake kuchukuliwa na Joyce Banda, ambaye alikuwa Makamu wa Rais. Hata hivyo kabla ya kifo cha Mutharika, Banda na Rais huyo waliingia katika mgogoro mkubwa kutokana na tuhuma kuwa Rais huyo alikuwa akimwandaa mdogo wake Peter kuja kubwa Rais badala ya “kuzingatia itifaki” ambapo Banda kama Makamu wa Rais ndiye aliyeonekana “mrithi stahili” wa nafasi hiyo.

Joyce Banda Department for International Development photo crop.jpg

Mgogoro huo ulipelekea Banda kutimuliwa wadhifa wake wa Makamu Mwenyekiti wa chama tawala DPP japo aliendelea na wadhifa wake kama Makamu wa Rais. Na Mutharika alipofariki, mwanamama huyo alimrithi urais kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo. Hatua hiyo ilipelekea lundo la wanachama kuhama chama hicho cha DPP na kujiunga na chama alichoasisi Banda cha DP baada ya kufukuzwa kutoka chama tawala DPP.

Hata hivyo, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2014 ambapo chama cha DPP kilimsimamisha Peter Mutharika, Banda alishindwa vibaya, na safari ya urais wake ikaishia hapo. Wakati Mutharika alipata asilimia 36.4, Banda aliambulia asilimia 27.8. Jitihada za kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi huo ziligonga mwamba.

Kuna mtu mmoja muhimu wa kutajwa kuhusiana na uchaguzi huo, naye ni Saulos Chilima.

Saulos Klaus Chilima, Vice President of Malawi 2017 (cropped).jpg

Huyu alikuwa mgombea mwenza wa Mutharika mwaka 2014 na baada ya ushindi wa Mutharika, Chilima akawa Makamu wa Rais. Hata hivyo, mwaka 2018 alijiondoa kutoka chama tawala DPP na kuunda kikundi cha mabadiliko (transformation movement) cha United Transfmation Movement (UTM) ambacho baadaye kilikuja kuwa chama kamili cha siasa.

Mapema mwaka jana, Chilima na UTM yake iliungana na vyama kadhaa vya upinzani kwa ajili ya kusimamisha wagombea kwenye uchaguzi mkuu ambapo umoja wao ulipelekea Chilima aliyekuwa mgombea wake kushika nafasi ya tatu akipata asilimia 20.24 na wabunge wanne kwenye bunge la nchi hiyo.

Turejee kwa Peter Mutharika. Urais wake ulikumbwa na pigo Februari mwaka huu baada ya Mahakama ya Katiba kutengua matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kuamuru urudiwe upya.

Mwezi mmoja baadaye, Chilima na UTM yake ilifikia makubaliano na chama kingine cha Malawi Congress Party kinachoongozwa na Chakwera, ambaye kwenye uchaguzi wa mwaka jana alishika nafasi ya pili akiwa na asilimia 35.41 nyuma ya Mutharika aliyepata asilimia. Kwahiyo ukiangalia matokeo hayo, laiti Chakwera na Chilima wangeungana dhidi ya Mutharika katika uchaguzi huo, wangeweza kumbwaga Rais huyo.

 Lazarous Chakwera  Saulos Chilima

Na hilo ndilo lililotokea katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumanne iliyopita, ambapo Chakwera ameibuka mshindi kwa kupata asilimia 58.57 ya kura dhidi ya asilimia 39.92 za Mutharika. Chilima ambaye alikuwa mgombea mwenza wa Chakwera atakuwa Makamu wa Rais.

Hili ni funzo muhimu kwa wapinzani wetu kuhusu ushikiano endapo wana nia ya dhati ya kumng’oa madarakani Magufuli na CCM yake iwe ni Oktoba mwaka huu au uchaguzi mkuu ujao mwaka 2025.

Nirejee kwenye swali iwapo Wapinzani wetu wanaweza kufanya kilichotokea Malawi. Kuna tofauti kadhaa kati ya ‘siasa za Malawi’ na ‘siasa za Tanzania,’ kubwa zaidi ikiwa ni kwamba licha ya ‘udogo wake’ (ina jumla ya watu milioni 19 hivi ilhali Tanzania ina jumla ya watu milioni 59 hivi), wenzetu “wamekua kisiasa” kama ulivyoona jinsi Banda alivyoweza kuunda chama chake akiwa Makamu wa Rais kama ambavyo Chilima alivyofanya akiwa katika wadhifa huo.

Lakini kikubwa zaidi ni uhuru wa mahakama. Ikumbukwe kuwa baada Mahakama ya Katiba kutengua matokeo ya uchaguzi Februari mwaka huu, Mutharika alikata rufaa na Tume ya Uchaguzi, lakini licha ya shinikizo kubwa, Mahakama Kuu ya nchi hiyo iliridhia hukumu ya Mahakama ya Katiba na kuamuru uchaguzi urudiwe upya.

Kwa mazingira ya Tanzania yetu, kilichojiri Malawi ni kama miujiza flani. Kwanza kimsingi hatuna Mahakama ya Katiba. Iliyopo ni ‘ya kufikirika zaidi kuliko uhalisia.’ Iliundwa kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 ambayo inahusika tu na masuala yanayohusu Muungano, endapo kutatokea mgogoro kati ya Serikali ya Muungano na SMZ.

Lakini hata Mahakama Kuu iliyopo imejionyesha bayana kuwa ipo mfukoni mwa Magufuli. Na kingine kinachoinyima uhalali mahakama hiyo katika suala lolote linalomhusu Magufuli ni ukweli kwamba mmoja wa majaji ni nduguye.

Hata hivyo, wakati changamoto za kimfumo zinaweza kuwa kikwazo kwa kilichojiri Malawi kutokea Tanzania, pengine tatizo kubwa zaidi ni kwenye uwezekano wa ushirikiano kati ya vyama vya upinzani.

Ilipotokea nafasi bora kabisa kwa upinzani kuing’oa CCM madarakani mwaka 2015, muungano wa wapinzani wa UKAWA ukafanya kosa la kihistoria kwa kumteua mgombea aliyekuwa MAKAPI YA CCM, Edward Lowassa, ambaye kutokana na rekodi ndefu ya tuhuma za ufisadi (zilizokuwa zikipigiwa kelele na wapinzani hao hao tangu 2006) ilikuwa rahisi kwa CCM kushinda uchaguzi huo uliofanyika huku chama hicho tawala kikikabiliwa na orodha ndefu ya tuhuma za ufisadi. Ili kutomuudhi Lowassa, chama kikuu cha upinzani, Chadema, kiliamua kuachana na ajenda yake kuu ya vita dhidi ya ufisadi, na tangu wakati huo chama hicho hakijaweza kuwa na ajenda kuu.

Kama kuna vyama vinavyoweza kumuondoa Magufuli madarakani ni Chadema na ACT-Wazalendo. Chadema kwa sababu licha ya kuwa chama kikuu cha upinzani, ndicho chenye wafuasi wengi zaidi kuliko chama kingine cha upinzani Tanzania. ACT-Wazalendo kwa sababu licha ya kuwa mbadala wa CUF huko Zanzibar, ni chama kinachoongozwa na Zitto Kabwe, mwanasiasa hodari kabisa katika siasa za upinzani Tanzania.

Lakini wakati Zitto na ACT-Wazalendo kwa ujumla wamekuwa wakionyesha kiu ya ushirikiano baina ya Wapinzani, na hususan Chadema, kwa upande wake, Chadema wameonyesha dalili za wazi kuwa hawahitaji ushirikiano huo.

Na pengine uthibitisho kuwa ‘kuna damu mbaya,’ wakati Zitto amekuwa mstari wa mbele kwenye ‘zahma’ dhidi ya Mbowe na Chadema kwa ujumla, mwitikio wa Chadema umekuwa hafifu, uthibitisho wa hivi karibuni ukiwa tukio la kukamatwa kwa Zitto.

Ningependa kuona Chadema na ACT-Wazalendo wakiungana na kusimamisha mgombea mmoja wa nafasi ya urais kumkabili Magufuli. Nafahamu vikwazo mbalimbali vinavyoweza kukwamisha hilo, lakini ni muhimu kwa Chadema kutambua kuwa ikipuuza ushirikiano na ACT-Wazalendo, athari zinaweza kuwa kubwa zaidi kwake kuliko ACT-Wazalendo. Kwanini? Kwa sababu, hadi muda huu ACT-Wazalendo ina mbunge mmoja tu ambaye ni Zitto. Ilhali Chadema ina wabunge kadhaa ukitoa licha ya hao kadhaa waliohama. Katika mazingira yaliyopo, kuna uwezekano mkubwa kwa Chadema kupoteza majimbo kadhaa ilhali ACT-Wazalendo inaweza kuongeza idadi ya wabunge kupitia majimbo ya Zanzibar.

Kwamba japo Magufuli anaweza kuihujumu Chadema isipate jimbo hata moja Bara (haiwezi kupata jimbo Zanzibar) hana ubavu wa kuzuwia ACT-Wazalendo kupata wabunge huko Zanzibar.

Nadhani kikubwa kinachokwaza ushirikiano kati ya Chadema na AC-Wazalendo ni “ishu ndogo tu za kihistoria” ambazo hazipaswi kuendekezwa kwa muda mrefu kiasi hiki. Naam, Zitto na Mbowe walifarakana huko nyuma hadi kupelekea Zitto kufukuzwa katika chama hicho na kuanzisha ACT-Wazalendo. Lakini wakati Zitto ndio angepaswa kulea kinyongo, amekuwa mstari wa mbele kuiunga mkono Chadema katika nyakati ngumu kadhaa kama katika shambulizi la kinyama dhidi ya Tundu Lissu na hata majuzi Mbowe ‘aliposhambuliwa na watu wasiojulikana.’

Nihitimishe kwa kutarajia kuwa labda kilichojiri Malawi kitawashawishi Chadema kuafikiana na ACT-Wazalendo kushirikiana kwenye uchaguzi mkuu ujao hapo Oktoba. Pengine kuna watakaosema kwamba muda uliosalia ni mchache. Hata hivyo, ukweli kwamba Chakwera na Chilima waliungana mwezi Machi na kumudu kumuangusha Mutharika miezi mitatu baadaye, basi huenda yawezekana pia kwa Chadema na ACT-Wazalendo wakiungana Julai maana watakuwa na miezi mitatu pia kabla ya uchaguzi mkuu.

Pongezi za dhati kwa Chakwera na Chilima, na kila la heri kwa Chadema na ACT-Wazalendo nikitaraji kuwa mtajifunza kwa wenzenu wa Malawi. United you stand, divided you fall.

Ndimi jasusi wako,

Evarist Chahali

TANGAZO: niwasumbue na tangazo kuhusu vitabu vyangu viwili, "Jinsi Ya Kuwa Mtu Bora: Toleo la Pili” na “ Mwongozo za Kitabibu wa Jinsi Ya Kuacha Uvutaji wa Sigara.”

Endapo unakwama kwenye kufanya malipo HAPA basi nishtue nikuelekeze.

Twiti hizi zinaeleza jinsi ya kulipia

Karibuni