Ukishangaa Ya Nassari Unakutana na ya Lipumba

Wakati Mwingine Mchawi Wa Upinzani Ni Wapinzani Wenyewe

Nianze barua hii na shukrani nyingi kwa “wageni” zaidi ya 200 mliojisajili ili kutumiwa #BaruaYaChahali Jumatatu kama ya leo kila wiki. Lengo la barua hii ni kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha. Karibuni sana.

Pili, naomba samahani kwa kuchelewa kukutumia barua hii kwa sababu nilitaka kuiandika baada ya kusikia hukumu ya kesi baina ya Lipumba na Maalim Seif iliyotolewa maamuzi leo.

Twende kwenye mada. Wiki iliyopita haikuwa njema kwa siasa za Upinzani nchini Tanzania. Kwa upande mmoja tulishuhudia uhuni wa kisiasa uliohalalishwa na dola chini ya utawala wa Magufuli, ambapo Lipumba alifanikiwa kumtimua Maalim Seif kwa kufanya mkutano mkuu wa kihuni, uliopeleka kupatikana kwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, na hivyo Maalim Seif kutimuliwa kienyeji. Sambamba na hilo, Lipumba aijihalalishia uenyekiti wa chama hicho kikongwe.

Pamoja na tukio hilo la kuudhi, kulikuwa na tumaini japo si kubwa kwamba hukumu kuhusu mgogoro kati ya Lipumba na Maalim Seif leo ingeweza kutenda haki kwa “kumharamisha Lipumba na genge lake” na “kumhalalisha Maalim Seif na kundi lake.” Kwa bahati mbaya, Mahakama imehalalisha uhuni wa Lipumba, na hapohapo kutangaza kifo cha kisiasa cha Maalim Seif na CUF kwa ujumla. Nitafafanua baadaye.

Na katika kinachoweza kutafsiriwa kuwa ni “dalili za kukubali yaishe,” Maalim Seif ametangaza kujiunga na “chama cha Zitto” ACT Wazalendo. Endapo hatua hiyo itakuwa na ufanisi au la, nitaongelea hilo siku nyingine.

Kuna vitu viwili vinavyosikitisha sana kuhusu suala la CUF. Kwanza, ni jinsi ilivyo rahisi kuchezea demokrasia Tanzania. Kinachotokea huko CUF ni mwendelezo tu wa matukio mbalimbali ya ukiukwaji sheria, ambapo serikali kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa na/Au Tume ya Uchaguzi hukaa kimya kama si kuunga mkono upande wenye kuzua chokochoko.

Tatizo hapa sio Msajili au Tume bali ni CCM. Na kimsingi tatizo hasa sio CCM inayozitumia vibaya taasisi hizo mbili za umma bali chanzo ni KATIBA. Pasipo Katiba mpya, upinzani utaendelea kuwa kama unaishi kwa hisani tu.

Pili, janga hilo la CUF linaamsha kumbukumbu ya ukweli mchungu kuhusu takriban vyama vyote vya upinzani: vinaficha na kulea mapungufu yao, na pindi mapungufu hayo yakiviumbua vyama hivyo, kimbilio lao ni kuilaumu CCM. Mfano hai ni skata la Lowassa huko Chadema.

Kwa upande wa CUF, kulikuwa na mapungufu katika Katiba ya chama hicho, mapungufu ambayo Lipumba ameyatumia vema kufanya uhuni aliofanya. Mapungufu hayo yalikuwa ya makusudi, hasa kwa vile CUF imekuwa kama chama cha kisultani ambapo badala ya msingi wake kuwa katika wanachama, chenyewe msingi wake umekuwa “ndoto ya urais wa Maalim Seif.”

Mapungufu haya yaliyoigharimu CUF yanaweza pia kuigharimu Chadema, chama ambacho licha ya jina lake tu kuwa “chama cha DEMOKRASIA na maendeleo” kimekataa katakata kutekeleza demokrasia, kwa kutoitisha uchaguzi mkuu miaka nenda miaka rudi. Ofkoz, Mbowe ni kiongozi mzuri lakini kanuni za demokrasia zinataka viongozi wazuri nao wapatikane kwa njia ya uchaguzi, wahalalishwe kubaki viongozi au waondolewe madarakani.

Kuhusu Nassari, kilichofanyika sio tu ni uhuni wa kisiasa bali pia tusi kwa walalalahoi wa Tanzania ambao watakamuliwa kulipia uchaguzi mdogo kwenye jimbo hilo. Sidhani kama suala la Nassari linahitaji mjadala mrefu hasa kwa vile tetesi kuwa “amenunuliwa na CCM” zilishasikika kitambo.

Uhuni aliofanya ni wa kitoto. Angeweza tu kutangaza anajiuzulu ubunge ili “kumhudumia mkewe,” kuliko kuwapa CCM fursa ya kuonyesha kuwa “upinzani una wababaishaji kama Nassari.” Na si ubabaishaji tu bali pia ni ufisadi, kwa sababu mbunge huyu alikuwa akilipwa mamilioni ya shilingi bila kutimiza wajibu wa kuwakilisha wapigakura wake.

Lakini pia ishu ya Nassari inaonyesha tena mapungufu ya Chadema. Chama hicho kimeshindwa kabisa kuwabaini mamluki wanaokitafuna ndani kwa ndani na badala yake kimekuwa mahiri kuilaumu CCM. Ofkoz, CCM inawahujumu wapinzani. Lakini wapinzani nao wanairahisishia CCM kuwahujumu.

Kwanini Chadema haikuchukua hatua kwa Nassari kabla ya Mtu Mfupi Ndugai kuwa kama “muuza bucha aliyedondokewa na ajali ya mbuzi mbele ya bucha lake”? Kwanini uongozi wa Chadema haukumuweka chini mbunge huyo kijana na kumdadisi kwanini anafanya utoro, kitu ambacho sio tu ni kosa kwa wapigakura bali pia kilitishia kukigharimu chama hichoi kikuu cha upinzani kupoteza jimbo?

Chadema haikuchukua hatua dhidi ya Nassari kwa sababu chama hicho kinaendeshwa kishkaji. Na ukitaka uthibitisho wa chama hicho kuendeshwa kishkaji ni “kukataa katakata kufanya uchaguzi mkuu.”

Naomba ieleweke kuwa mie sina chama. Na kuikosoa Chadema au CUF hakumaanishi kuwa sivipendi vyama hivyo.However, “anayekupenda atakwambia ukweli.” Lakini kwa bahati mbaya - au makusudi - ukitaka kugombana na mswahili, mwambie ukweli. Kwahiyo sintoshangaa ukweli huu kwa Wapinzani ukatafsiriwa kama ni chuki yangu kwa vyama hivyo. Hata hivyo, vyovyote watakavyotafsiri, ukweli huo hautogeuka kuwa uongo bali utabaki ukweli.

Nimalizie barua hii kwa kukushukuru sana kwa kuchukua muda wako kunisoma. Kuna mengi sana ya kuongelea siku zijazo lakini pia ninakaribisha maoni hapo chini au kwa kuniandikia moja kwa moja evarist@criptext.com

Nakutakia siku na wiki njema.Tukutane tena Jumatatu ijayo.