Ukimya wa Lissu Masaa 36 baada ya Mbowe na wenzake kuachiwa huru; mustakabali wa ajenda ya katiba mpya
Hadi wakati makala hii inachapishwa - zaidi ya masaa 36 tangu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe na wenzake watatu waachiwe huru na DPP - Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Mheshimiwa Tundu Lissu hajatwiti chochote kuhusiana na suala hilo.


Kwa upande mmoja baadhi ya wana-Chadema walijitokeza kumtetea Mheshimiwa Lissu wakidai “hawezi kukurupuka kuongelea suala hilo.”

Lazarö E. killu @LazemKillu
@Chahali @freemanmbowetz Anasubiri tumalize point zetu aje kuzungumzia tulizoacha kuzungumzia..
WEMBO OIS IDIAG @DrPycon
@Chahali @freemanmbowetz @TunduALissu ni mtu makini wala hakurupuki ndugu jasusi😏Lakini kama jasusi alivyojibu, hoja kwamba Mheshimiwa Lissu hawezi kukurupuka kuongelea suala hilo haina mashiko kwa sababu sio suala linalohitaji maandalizi makubwa kuliongelea.
Kwa upande mwingine, kuna wanajaribu kutafsiri ukimya huo wa Mheshimiwa Lissu kama “kuchukizwa na hatua ya DDP kumwachia huru na wenzake.”

Jasusi anahisi kuwa huenda Mheshimiwa Lissu amekumbwa na dharura inayomzuwia kuongelea suala hilo na si kwamba amekasirishwa na hatua ya DPP kumfutia mashtaka Mheshimiwa Mbowe na wenzake.
Kuhusu mustakabali wa ajenda kuu ya Chadema kwa sasa ya katiba mpya, kuna “scenarios” kadhaa.

Kwa upande mmoja, hadi muda huu hakuna anayefahamu “walichoafikiana” Mama Samia na Mheshimiwa Mbowe walipokutana juzi baada ya mwenyekiti huyo wa Chadema taifa kufutiwa kesi na kuachiwa huru.
Hata hivyo, yayumkinika kuhisi kuwa “kuna maelekezo” aliyopatiwa Mheshimiwa Mbowe ambayo yanaweza kumfanya “aafikiane na msimamo wa Mama Samia kuwa suala hilo (la katiba mpya) lisubiri kwanza.”
“Maelekezo” hayo yanaweza kuwa yalitolewa kama “ushauri” lakini uwezekano mkubwa ni kwamba yalikuwa katika mfumo wa maagizo yanayohitaji kutelekezwa aka amri.
Huo ni udikteta? Hapana. Hivyo ndivyo siasa za kwenye viambaza vya utawala zinavyofanya kazi. Wakati hadharani watu hushauriwa kufanya/kutofanya hili au lile, kwenye viambazo hivyo lugha huwa katika namna Waingereza wanaita “thinly veiled threat”
Endapo “Mheshimiwa Mbowe atakuwa ameagizwa kuweka kando ajenda ya katiba mpya hadi baadaye,” kuna uwezekano akaingia kwenye mgogoro dhidi ya “wanaharakati wa mtandaoni” ambao wamekuwa mstari wa mbele kuitumia Chadema kama jukwaa la kudai katiba mpya.
Na moja ya changamoto zinazomkabili Mheshimiwa Mbowe ni pamoja na kuiondoa Chadema kutoka mwelekeo wa kuwa genge la harakati badala ya chama kikubwa cha upinzani.
Japo chama hicho kinapaswa kuunga mkono makundi mbalimbali yenye ajenda mtambuka kuhusu mustakabali wa Tanzania, kwa hadhi na historia yake, hakipaswi “kuendeshwa kwa rimoti” na makundi ya nje na hata ndani ya chama hicho.
Ikiamua, Chadema inaweza kurudi zama za “utatu mtakatifu” wa Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa Lissu na Mheshimiwa Zitto Kabwe ambapo chini ya uongozi wa wanasiasa hao, chama hicho kiliweza kuibua lundo la skandali za ufisadi kama vile Richmond (iliyopelekea aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kujiuzulu Februari 2008), Kagoda, EPA, Buzwagi, Tangold, Meremeta, Tegeta Escrow, nk.
Kilichowezesha chama hicho kufahamu kuhusu ufisadi huo mchango mkubwa wa baadhi ya maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa waliojitoa mhanga kuwapatia wanasiasa hao nyaraka za siri, kwa sababu walikuwa na imani nao na chama hicho.
Nihitimishe makala hii kwa kurejea nilichohitimisha kwenye makala iliyopita
kwamba chambuzi hizi kuhusu kuachiwa na Mheshimiwa Mbowe ni endelevu.
Jumapili njema.