Ufisadi Mkubwa Kabisa wa Tsh TRILIONI 2.4

Na Bunge La Mtu Mfupi limewahadaa Watanzania kuwa "hakuna fedha iliyofisadiwa."

Hivi ndivyo Tanzania yetu inavyobakwa mchana kweupe. Usiwe mzembe, soma ripoti hii kwa hatua, ruhusu akili yako itulie, ndipo utaelewa kwanini nchi yetu sio tu inaelekea kubaya bali tayari ipo mahala pabaya mno.

Cha kusikitisha ni kwamba Watanzania wengi wapo bize na UBUYU, na habari hii ya ufisadi mkubwa kabisa inajifia kifo cha asili. Hata hivyo, bado tupo baadhi yetu tunaoumizwa na hali hii, na ndio maana nikachukua muda wangu mwingi kufanya tafsiri hii ya makala hii ndefu ili nawe ufahamu yanayoendelea katika utawala huu wa Magufuli na mpwae Doto James huko Hazina.

Tafsiri hiyo ni hii hapa chini ambayo mwishoni ina ripoti ya uchunguzi wa CAG ambayo Bunge la Mtu Mfupi Ndugai limegoma kuwaonyesha ninyi walipakodi. Hapana Mtu Mfupi hajafanya hivyo kwa vile anampenda sana Magufuli, bali amefanya kitu kama hiki, “unapiga kelele darasani, ghafla mwalimu anaingia na kuuliza nani alikuwa anapiga kelele, kisha adui yako ananyoosha kidole - unatetemeka ukidhani anakutaja - anajitoa mhanga na kudai yeye ndiye alikuwa anapiga kelele.” Ukiona hivyo ujue kuna namna, unawekwa mateka kiaina.

Machi mwaka jana, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mussa Assad aliwasilisha ripoti yake ya mwaka wa fedha 2016/2017. Ilikuwa na mengo yasiyopendeza. Ilionyesha kuwa taasisi mbalimbali zilivyotumia fedha kwenye shughuli hewa huku kanuni za bajeti zikikiukwa.

Kilichogusa hisia za wengi ni sintofahamu ya mapato ya shilingi trilioni 25.3 na jumla ya shilingi trilioni 23.8 zilizotolewa na Hazina kwa ajili ya matumizi ya serikali. Je shilingi trilioni 1.5 ( tofauti kati ya mapato ya sh trilioni 25.3 na matumizi ya shilingi trilioni 23.8) zilienda wapi?

Serikali ilitoa maelezo kadhaa kuhusu tofauti hiyo huku sintofahamu hiyo ikisambaa kutoka bungeni hadi kwenye mitandao ya kijamii. Kisha, katika hafla moja Ikulu, Rais Magufuli alimuuliza CAG Assad, akisema, "CAG yupo hapa...Unaweza kusimama na kutuambia kama kuna fedha yoyote imeibiwa?" Assad alijibu "hapana mheshimiwa, hakuna fedha iliyoibiwa!"

Hata hivyo, hatimaye Bunge lilimwagiza CAG kufanya uchunguzi wa sintofahamu hiyo ya shilingi trilioni 1.5, kazi iliyokamilishwa mwezi uliopita na kuwasilishwa.

Hatua ya pili ilipaswa kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupitia ripoti hiyo. Hatua hiyo iliingiliwa kati baada ya Spika Job Ndugai kumuita CAG bungeni "kujibu tuhuma za utovu wa nidhamu," katika hatua ya kushangaza na inayodaiwa kukiuka katiba. Ndugai pia alisimamisha kwa muda kazi kamati zote za Bunge ikiwa ni pamoja na PAC.

Licha ya hatua hizo, PAC ilimudu kupitia ripoti hiyo ya CAG na, mapema mwezi huu, ikawasilisha ripoti yake yenyewe. Ripoti hiyo, hata hivyo, kwa kiasi kikubwa "ilipuuza" matokeo ya uchunguzi wa CAG, kama ambavyo Mwenyekiti wa Kamati alivyohitimisha, "hakuna upotevu wala wizi."

Wabunge wa Upinzani walipatwa na mshangao.

Mbunge (wa Chadema) Catherine Ruge, mhasibu kitaaluma na mjumbe wa PAC aliishutumu ripoti hiyo ya Kamati ya Bunge. Alieleza kuwa kwa hakika kuna kasoro ya shilingi Trilioni 2.4 iliyoibuliwa na CAG. Naibu Spika alimshurutisha kuondoa kauli hiyo baada ya pingamizi kutoka kwa waziri mmoja.

Kisha Mbunge mwingine wa Upinzani, Zitto Kabwe, aliibua hoja kuhusu shilingi bilioni 976.97 ambazo ripoti ya CAG inaonyesha kuwa zilitumika bila kufuata taratibu za kisheria.

Mwisho, Mbunge (wa Chadema) Halima Mdee alitoa rai ripoti ya CAG iwekwe hadharani ili wabunge wote waweze kuisoma sambamba na ripoti ya PAC. Rai yake ilikataliwa.

Wanahabari na wananchi wengine walihoji kwanini ripoti hizo zifanywe siri wakati mara zote zimekuwa zikiwekwa wazi.Kadhalika, ni utaratibu unaotambulika kimataifa – kupitia matamko kama Azimio la Lima – kwamba ripoti kama hizo shurti ziwekwe hadharani kwa minajili ya udadisi, mijadala na uwazi.

Ndio maana African Argumens inaweka ripoti hiyo hadharani.

Mkanganyiko wa hali ya juu

Ukisoma ripoti ya CAG utabaini vitu kadhaa.

Kwanza, madai ya Mwenyekiti wa PAC kuwa ripoti ya CAG haikukuta ushahidi wowote wa upotevu au wizi, kwa kiasi flani si sawia; inaeleza ndivyo sivyo kuhusu kazi aliyopewa CAG. Uchunguzi wa CAG haukulenga kubaini wizi au ushahidi wa wizi au kumnasa mwizi. Kama ilivyoelezwa kwenye hadidu za rejea, lengo la uchunguzi huo lilikuwa kubaini tofauti ya shilingi Trilioni moja unusu iliyojitokeza.

Hii ilihusisha kwanza kufanya mapitio ya mapato na matumizi ili kuangalia kama kuna mwafaka. Kisha, iliangalia iwapo utoaji fedha ulifanyika kwa mujibu wa sheria na kuangalia kama kuna malipo yaliyofanyika bila kuidhinishwa.

Kwa hakika ripoti ya CAG ilibaini kasoro kadhaa, zinazotosha kuumiza kichwa. Japo hakuna ishara za ujambazi wa kupora benki lakini tunaona kitu kama fedha kutoka kwenye sehemu ya kuhifadhia fedha ikitapakaa sakafuni katika hali inayokanganya kabisa.

Mwanzoni kabisa mwa ripoti hiyo kuna kauli inayogusa hisia kuhusu mwelekeo wa uchunguzi huo. Yapaswa kufanya nukuu kamili: " Uhakiki wetu ulikwazwa na ukosefu wa nyaraka stahili na maelezo yasiyojitosheleza kutoka kwa Utawala (wa Wizara ya Fedha), vitu ambavyo vilikuwa muhimu kupata usahihi na ukweli wa viwango husika. Kwa mfano, Wizara haikuweza kutoa nyaraka kama vile "Cash Book for Consolidated Funds" na "Bank Reconciliation Statements" ambazo hutoa taarifa za msingi kuhusu fedha husika. Taarifa zilizotolewa zilikuwa zimetapakaa katika vipengele kadhaa na zilikuwa zimefanyiwa marekebisho mengi wakati wa uhakiki.

Ikiendelea, ripoti hiyo ilibaini kwamba kiwango cha fedha za mapato na matumizi kilikuwa juu zaidi ya ilivyoripotiwa wali, japo ni muhimu kuzingatia kwamba sio kutokana na sababu zilizotolewa serikali April 2018. Tofauti na kiwango cha awali, inaonekana kuwa fedha za matumizi zilizidi fedha za mapato kwa shilingi bilioni 290.67, japo inatahadharisha kwamba "uthibitisho wa salio kutoka benki kuu hauendani na kiwango hicho."

Kisha uchambuzi katika ripoti hiyo unaangalia kwa kina udhaifu wa mfumo wa usimamizi wa fedha. Ripoti inaeleza kufeli kwa Hazina, na Katibu Mkuu wa Hazina (Mlipaji Mkuu wa Serikali) katika ufuatiliaji mahesabu kwenye akaunti mbalimbali. Pia inakosoa "akaunti zilizotapakaa ovyo na salio lisiloendana na ushahidi kiuhasibu", na kufanya ripoti hiyo kutanabaisha kwamba "utimilifu, uwepo na usahihi wa salio kwenye akaunti husika hauwezi kuthibitishwa."

Shilingi trilioni 2.4 "zimepotea"?

Katika uchambuzi wa fedha zilizotolewa, mapungufu mengi zaidi ya kiusimamizi na kasma yanajidhihirisha. Miongoni mwao ni shilingi bilioni 976.96 zilizotolewa bila idhibi stahili. Wizara kadhaa ziliathirika; hata hivyo, katika kikao na PAC, CAG alieleza kuwa Hazina haikuweza kutoa uthibitisho kuhushu kutolewa kwa fedha hizo, na badala yake Katibu Mkuu wa Hazina alidai kuwa fedha hizo zilipelekwa Ikulu. Ni muhimu kufahamu kuwa Ikulu haikaguliwi na CAG.

Maelezo haya yanapaswa kufuatiliwa na kuthibitishwa, lakini kwa namna yoyote ile, suala la shilingi bilioni 976.96 linaacha alama ya kuuliza, na ripoti inatanabaisha "utoaji wa fedha usiozingatia kanuni unaashiria kuhitajika kwa maboresho katika usambazaji wa fedha za bajeti."

Suala jingine muhimu kuzingatiwa ni kwamba ingawa usimamizi mbovu wa fedha unaweza kufanya majukumu na mamlaka ya CAG kikatiba kuwa magumu, vipi kuhusu zilipo shilingi trilioni moja unusu?

Katika hitimisho, ripoti hiyo inaondoa kiasi hicho cha fedha (shilingi trilioni moja unusu) lakini inazua kiwango kingine kikubwa zaidi cha shilingi triliioni 2.4

Hiki ndicho kiasi ambacho Mbunge (wa Chadema) Ruge alikieleza. Ni jumla ya kasoro za kifedha zilizoonyeshwa kwenye ripoti ya CAG ambazo ni

Shilingi bilioni 976.96 zilizotolewa bila kuidhinishwa (ukurasa 19-23)

Shilingi bilioni 656.6 ambazo ni tofauti kati ya "Exchequer Issues Warrant" na "Exchequer Release Report" (ukurasa wa 29)

Shilingi bilioni 290.67 za "overdraft" isiyo na maelezo  (ukurasa wa 3)

Shilingi bilioni 234.12 za "Exchequer Issues Warrants" zilizotolewa bila maelezo ya kueleweka (ukurasa wa 23-4)

Shilingi bilioni 189.99 zilizochotwa bila idhini kutoka  "Consolidated Fund" (ukurasa wa 19)

Shilingi bilioni 3.45 zinazounganishwa isivyo sahihi na kufutwa kwa  "Exchequer Issue Warrants" (ukurasa wa  26)

Shilingi bilioni 3.26 ambazo ni Exchequer Issue Warrants isivyo halali (ukurasa wa 24)

Mustakabali wa fedha za umma Tanzania ukoje?

Mbunge Ruge anadai kwamba kuna haja ya kufanyia uhakiki kamili, lakini hilo linaonekana kuwa jambo lisilowezekana katika mazingira ya siasa za Tanzania kwa sasa. Ripoti ya CAG inaibua maswali kadhaa, hususan kuhusu Katibu Mkuu wa Hazina, Doto James, anayedaiwa kuwa mpwa wa Rais Magufuli. James alikuwa TANROAD wakati mjomba wake Magufuli alipokuwa Waziri wa Ujenzi. Baadaye alijiunga na timu ya kampeni ya Magufuli, ambaye baada ya kuwa Rais alimteua mpwae huyo kuwa Naibu Katibu Mkuu Hazina, na mwaka mmoja baadaye akateuliwa kuwa Katibu Mkuu kamili akichukua nafasi ya mtu ambaye alikuwepo Hazina kitambo.

Kuhusu mustakabali wa fedha za umma Tanzania, tutarajie hali kama hii iliyopo sasa au pengine mbaya zaidi.

Katika kikao cha Bunge kilichoisha hivi karibuni, taarifa zaidi zimejitokeza hadharani kuhusu utetezi usiokubalika kuhusu fedha zilizotengwa kwa matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Kwa mfano, iliripotiwa kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha, jumla ya shilingi bilioni 8.3 kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi zilikuwa mara saba zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zilizotengwa. Kiwango hicho kilichotolewa kinaweza kuwa kikubwa zaidi, hasa kwa vile ilibainika kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitengewa shilingi bilioni 12.4 mwezi Septemba 2018 kwa ajili ya chaguzi ndogo tatu.

Ripoti ya CAG inaonyesha jinsi usimamizi wa fedha za umma nchini Tanzania ulivyo na mushkeli. Kwa bahati mbaya, uchaguzi mkuu ukiwa takriban mwaka mmoja tu kutoka hivi sasa, kuna kila sababu ya kuamini kuwa hali itakuwa mbaya zaidi.

Kukabiliana na hali hii kunapaswa kuanzia na uwazi, na ndio sababu ya kuchapishwa ripoti hii ya CAG hapa chini. Kiu ya wananchi kujua ukweli sambamba na mijadala vinaweza kusaidia kuleta mwanga kuhusu ripoti hii ya CAG, na pengine kutoa ufuatialiaji usiofungamana na upande wowote kuhusu kazi za Bunge na CAG.

SOMA RIPOTI YA UCHUNGUZI WA CAG HAPA


Tukutane wiki ijayo