Uchunguzi Wa Kiintelijensia Kwa Kanuni Ya Dhana Zinazoshindana (ACH): Nani Aliyepanga Shambulio Dhidi Ya Mheshimiwa Mbowe?

Somo: Shambulizi dhidi ya mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Mheshimiwa Freeman Mbowe

Mahala: Dodoma

Tarehe ya tukio: Jumanne 8 Juni 2020

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Dhana ya kwanza: Mheshimiwa Mbowe alishambuliwa na watu walewale waliomshambulia Mheshimiwa Tundu Lissu Septemba 2017.

Uzito wa dhana: Mwendelezo wa siasa za ukatili na uonevu za Rais Magufuli dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani, vyama vyao na wanachama wa vyama hivyo.

Kwamba labda hawezi kuthubutu kuagiza Mheshimiwa Mbowe “aadhibiwe,” ukweli mchungu ni kwamba kama aliweza kujaribu kwa Mheshimiwa Lissu ambaye laiti angeshambuliwa ingejulikana bayana kuwa ni kutokana na kumkosoa Rais Magufuli mfululizo, kama ambavyo kada Ben Saanane “alivyopotea” baada ya kumkosoa Rais Magufuli mfululizo. Kwahiyo hakuna la ajabu kwa Rais Magufuli kurudia aliyowahi kuyafanya huko nyuma.

Kingine ni ukweli kuwa Rais Magufuli ni mtu mwenye “chuki za kitoto,” mfano hai ukiwa jinsi anavyoendelea kumwandama Dkt Mwele Malecela miaka minne baada ya kumfukuza kazi.

Udhaifu wa dhana: Mwenyekiti wa Taifa wa chama kikuu cha upinzani ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Upinzani kuwa “nje” usiku bila ulinzi inazua shaka. Maelezo kuwa viongozi wa Upinzani wameondolewa ulinzi kwa sababu ya korona hayana mashiko kwa sababu endapo Mheshimiwa Mbowe alikuwa hana ulinzi basi hakupaswa kuwa “nje” muda huo.

Kadhalika, “waliomshambulia” kumwambia aache kumsumbua Rais Magufuli doesn’t really make any sense. Ni kwamba, laiti waliomshambuliwa wangekuwa wanataka kumfikishia ujumbe basi yayumkinika kuhisi kuwa “shambulio hilo lingekuwa kubwa zaidi” (japo simaanishi kuunga mkono shambulio hilo wala simaanishi kuwa ‘ni kiduchu tu.’)

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Dhana ya pili: Mheshimiwa Mbowe alishambuliwa na watu wanaohusiana na Chadema

Uzito wa dhana: Tukio la kuvamiwa Mheshimiwa Mbowe lilitokea ndani ya masaa 24 tangu Mheshimiwa Lissu alipotangaza kuwa anawania urais. Dhana hapa ni kwamba Mheshimiwa Mbowe angekuwa kikwazo dhidi ya safari ya urais ya Mheshimiwa Lissu hivyo ilikuwa lazima ashughulikiwe.

Udhaifu wa dhana: Ili Mheshimiwa Mbowe adhuriwe kwa ajili ya Mheshimiwa Lissu shurti Mheshimiwa Lissu awe Tanzania. Na katika mazingira ya kawaida tu, laiti kungekuwa na nia ovu kama hiyo basi tukio hilo lisingetokea ndani ya masaa 24 tangu Mheshimiwa Lissu atangaze nia.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Dhana ya tatu: Shambulio dhidi ya Mheshimiwa Mbowe halihusiani na siasa bali ni “masuala binafsi.”

Uzito wa dhana: Taarifa ya jeshi la polisi kuwa Mheshimiwa Mbowe alikuwa kwa mzazi mwenzake, Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, Joyce Mukya, inazua utata kidogo. Kwa uelewa wangu, mke wa Mheshimiwa Mbowe anafahamika kwa jina la Lilian Mbowe. Kwamba amezaa nje, tena na Mbunge wa Viti Maalum, inazua maswali. Je shambulio hilo linahusiana na “pembetatu za uhusiano huo” - yaani yeye Mheshimiwa Mbowe, Mkewe Lilian na huyo Joyce Mukya? Au kuna pembe ya nne, kwamba huenda licha ya kuwa na Mheshimiwa Mbowe, Joyce alikuwa na “mtu wake” aliyekerwa na uhisiano wake na Mheshimiwa Mbowe?

Udhaifu wa dhana: Japo “wivu wa mapenzi” huweza kusababisha madhara, tukio hilo haliashirii kuwa hivyo, kwa sababu wahusika wasingeishia kufanya shambulizi tiu dhidi ya Mheshimiwa Mbowe bali huenda wangechukua/wangeacha “ushahidi.”

Kadhalika, “interijensia ya geshi ra porisi” haijawahi kuaminika katika suala lolote linalomhusu mwanasiasa au mwanachama wa Upinzani. Taarifa yao imekaa kisiasa zaidi kuliko wito wao kuwa suala hilo lisigeuzwe kuwa la kisiasa.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Dhana ya nne: Uhusika wa rogue elements.

Uzito wa dhana: Moja ya athari za kuchanganya taaluma ya ushushushu na itikadi za siasa ni kuzaliwa na kushamiri kwa “rogue elements,” yaani watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ambao wanaweza kujichukulia maamuzi mkononi bila hata kuagizwa na mwajiri wao. Nimeshasikia mlolongo wa matukio ya aina hii yakifanywa na watu wa Kitengo.

Lakini Idara ya Usalama wa Taifa yenyewe ni rogue pia kwa sababu kwa mujibu wa taarifa nilizonazo, uongozi wa taasisi hiyo nyeti kwa sasa upo mikononi mwa Rais Magufuli mwenyewe, kinyume na Katiba. Inaelezwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara hiyo, Diwani Athumani yupo yupo tu huku badala ya Idara kumshauri Rais, sasa inapokea maelekezo kutoka kwake licha ya ukweli kuwa Rais Magufuli sio afisa usalama wa Taifa.

Na kwa vile moja ya mapungufu makubwa yanayoikabili taasisi hiyo ni kuwa na MAAFISA WASIO NA INTELLIGENCE, si ajabu kwa akili zao fyongo walidhani kumshambuliwa Mheshimiwa Mbowa masaa machache baada ya Mheshimiwa Lissu kutangaza nia ya urais kunaweza kujenga picha ya vita ya urais ndani ya Chadema. Wanasema “never underestimate power of stupid people in large group.”

Udhaifu wa dhana: hakuna

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Kuondoa dhana dhaifu: Dhana dhaifu zaidi kati ya hizo nne ni ya pili. Kigezo cha udhaifu wa dhana ni udhaifu wake kuwa na nguvu kuliko uzito wake.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Kwahiyo tunabakiwa na dhana tatu

  • Mheshimiwa Mbowe alishambuliwa kwa maagizo ya Rais Magufuli

  • Mheshimiwa Mbowe alishambuliwa kutokana na “masuala binafsi kimahusiano.”

  • Mhehimiwa alishambuliwa na rogue elements za kitengo.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Hitimisho: hebu jaribu kuwa jasusi japo kwa dakika chache na ufikie hitimisho la uchunguzi huu na hatimaye kumbaini mhusika mkuu katika tukio hilo. Ofkoz, jasusi wako nina jawabu lakini naomba nilihifadhi kwa sasa 😊

Ndimi jasusi mstaafu

Evarist Chahali