Uchambuzi wa kiintelijensia kuhusu hotuba ya Mbowe kwa taifa aliyoitoa jana Machi 8, huko Iringa
Utangulizi:
Jana Machi 8, 2022, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe alihutubia taifa kupitia maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake yaliyofanywa na Baraza la Wanawake wa Chadema (BAVICHA) mkoani Iringa.
Hotuba hiyo ilisubiriwa kwa hamu wa watu wengi kwani ilitarajiwa kutoa mwelekeo wa Chadema baada ya kesi iliyokuwa ya ugaidi na uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili Mheshimiwa Mbowe na wenzake watatu kufutwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) Ijumaa iliyopita (Machi 4) na washtakiwa hao kuachiwa huru.
Lakini pia hotuba hiyo ilitarajiwa kutoa mwangaza kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Mheshimiwa Mbowe, endapo atakuwa na kinyongo kutokana na madhila aliyopitia kwa kukaa jela takriban miezi minane na hivyo kuwekeza zaidi kwenye siasa za mapambano (confrontational politics) au kuelemea kwenye siasa za maridhiano (consensual politics) sambamba na kusamehe yaliyopita (reconcialiatory politics) na kutoa fursa ya maslahi ya taifa kuwekwa mbele ya maslahi ya kiitikadi na/au yake binafsi.