Uchambuzi wa kiintelijensia kuhusu hotuba 'kali' ya Rais Samia jana
Jana Rais Samia Suluhu alitoa hotuba ambayo yaweza kutamkwa kuwa ni ‘kali’ kutokana na mazito mengi aliyosema.
Lakini kabla ya kuingia kwenye uchambuzi huu, ni vema kusikiliza hotuba yenyewe kamili
TANGAZO
Matarajio kabla ya hotuba ya Rais Samia
Kulikuwa na matarajio kadhaa kabla ya hotuba ya jana na Rais Samia. Kubwa zaidi lilikuwa mkuu huyo wa nchi kuongelea kuhusu janga la utekaji, mauaji, ubakaji na ulawiti ambalo yayumkinika kutanabaisha kuwa limepamba mot nchini Tanzania.
Katika hilo la utekaji na mauaji, Rais alitarajiwa kuongelea kuuawa kwa kada mwandamizi wa Chadema, marehemu Ali Mohamed Kibao. Matarajio katika hilo yalikuwa kwamba kama mfariji mkuu wa taifa, angewafariji wafiwa na kuwahakikishia usalama wananchi wengine, ilhali kama amiri jeshi mkuu, alitarajiwa kuviamuru vyombo vya ulinzi na usalama kushughulikia kwa bidii zaidi janga na utekaji na mauaji.
Vilevile Rais alitarajiwa kuongelea maandamano ya Chadema, lakini katika lugha ya kidiplomasia, kukisihi chama hicho pinzani kiwe na subira wakati serikali yake inachunguza kifo cha marehemu Kibao.
Kadhalika, ilitarajiwa kuwa Rais Samia angejibu matakwa yaliyowasilishwa kwake na Chadema, ambayo chama hicho kimeweka bayana kuwa yasipotimizwa kufikia Septemba 21, kitaitisha maandamano Septemba 23.