Uchambuzi wa Kiintelijensia Kuhusu Kujiuzulu kwa Spika Ndugai, Mrithi Wake, Na Mustakabali wa CCM. Pia Dondoo Kuhusu Kabineti Mpya
Jana Januari 6, 2022 itaingia kwenye kumbukumbu za historia ya Tanzania kufuatia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, kutangaza kujiuzulu.
Ikumbukwe, mwaka jana, Tanzania ilimpoteza Rais John Magufuli akiwa madarakani, na kuandika historia mpya kwa taifa hilo kupoteza kiongozi aliyekuwa madarakani.
Tangazo la kujiuzulu kwa Ndugai lilipokelewa kwa mshtuko mkubwa, hasa kwa vile awali ilidhaniwa kuwa suala hilo “linaelekea kufa kifo cha asili.” Hata hivyo, kasi ya mashambulizi ya baadhi ya wanasiasa wa CCM dhidi ya Spika huyo, hususan jana, iliashiria kuwa sakata hilo bado “bichi.”
Uchambuzi huu wa kiintelijensia unajikita kwenye kujiuzulu huko na kutoa tafsiri pana, sambamba na kutanabaisha mustakabali wa CCM baada ya tukio hilo zito. Kadhalika, uchambuzi huu utatoa mwanga kuhusu mabadiliko ya baraza la mawaziri la Mama Samia Suluhu linalotarajiwa kutangazwa hivi punde.