Uchambuzi wa kiintelijensia: kauli tete za Jenerali Muhoozi, mtoto wa Rais Museveni wa Uganda ni mzaha tu au ni ishara za mambo yajayo?
Oktoba 3 mwaka huu, mtoto wa Rais Yoweri Museveni, Jeneral Muhoozi Kainerugaba, alititwi kwamba ingechukua wiki 2 tu kwa yeye na jeshi lake kuiteka Nairobi
Japo Jenerali huyo anafahamika kwa kauli zake tete katika mtandao huo wa kijamii, twiti hiyo ya kutishia kuvamia Kenya ilizua taharuki mtandaoni na nje ya mtandaoni.
Lakini kabla ya tishio hilo, Muhoozi alishazua tafaruku nyingine kwa “kumlaumu” Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kwamba alipaswa kubadili katiba ya nchi hiyo ili atawale muhula wa tatu. Na akaenda mbali zaidi na kudhihaki katiba na utawala wa sheria akidai huko Uganda wanajali mapinduzi tu.
Kana kwamba alichofanya kilikuwa tukio la kishujaa, siku chache baadaye, afande huyo aliyekuwa na cheo cha luteni jenerali alipandishwa cheo na baba yake kuwa jenerali kamili. Hata hivyo, kupandishwa cheo huko kuliambatana na Muhoozi kuondolewa kwenye ukamanda wa jeshi la nchi kavu.
Baadaye baba yake, Rais Museveni, aliwaomba radhi Wakenya kwa kauli za mwanae, na baadaye tena Muhoozi mwenyewe alimuomba radhi Rais mpya wa Kenya William Rutto.
Je tukio hilo - na mengineyo kadhaa huko Twitter - ni utani tu wa Muhoozi (huwa pia anafanya “utani” kuhusu mabinti warembo) au ni kiashiria cha “yajayo mbeleni”?
Makala hii inafanya tathmini ya kiintelijensia kwa kutumia mbinu inayofahamika kama “Analysis of Competing Hypotheses” (ACH), mbinu inayoaminika kuwa ni bora zaidi katika kufanya uchambuzi wa kiintelijensia. Mbinu hiyo inashindanisha dhana mbalimbali kabla ya kubaki na dhana moja inayohitimisha uchambuzi.