Uchambuzi Kuhusu Mashinji Kuhama Chadema Na Kujiunga na CCM

Kuna Tatizo Ndani Ya Chadema Lakini Kama Ilivyo Dhambi Kuikosoa CCM Ndivyo Ilivyo Pia Kwa Chadema

Kwamba Mashinji angehama wala halikuwa jambo la “if” (endapo) bali “when” (lini). Na hatimaye jana mwanasiasa huyo aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani, Chadema, alitangaza kuhama rasmi chama hicho na kujiunga na CCM.

Na kama ilivyo kawaida, wafuasi wa Chadema, wakarejea kauli yao maarufu kila mmoja wao anapowakimbia, kudai “Mashinji alikuwa pandikizi la CCM.”

Wengine wakajaribu kugeuza tuio hilo la kuhama kwa Mashinji kuwa ni ushindi kwa Chadema kwa vile hivi karibuni chama hicho kilipata Katibu Mkuu John Mnyika aliyechukua nafasi ya Mashinji. Ndugu yangu Ansbert Ngurumo akaandika haya

Namheshimu sana Bwana Ngurumo lakini ninafadhaika kuona watu wenye uelewa mkubwa kama yeye, na ambao huenda wakitoa ushauri watasikilizwa, nao wanafanya siasa.

Haihitaji akili kubwa kubaini kuwa lolote “baya” litakalosemwa na Chadema muda huu, hata liwe na ukweli mkubwa kiasi gani, litatafsiriwa kuwa ni sawa na simulizi ya “sizitaki mbichi hizi” ya sungura aliyeshindwa kufikia ndizi mkunguni.

Image result for sizitaki mbichi hizi

Kwamba sungura kila alipojaribu kurukia ndizi mkunguni hakuzifikia, na “alipokubali yaishe” akajifanya kusema “sizitaki mbichi hizi.” Stori hii hutumika kueleza kutapatapa kwa mtu aliyekosa kitu flani kisha akaishia kukiponda. Ndio wanachofanya ndugu zetu wa Chadema kila wanapopatwa na pigo la kuondokewa na viongozi/wanachama wao maarufu.

Mtu pekee ambaye hadi leo Chadema wanashindwa kumponda ni Lowassa, na ni kwa sababu za wazi. Aliwaingiza mkenge vibaya. Aliwapa matumaini hewa. Walimgeuza mungu-mtu. Na yayumkinika kuhisi kuna baadhi ya wana-Chadema hawaamini kama kweli Lowassa amewaacha kwenye mataa.

Na japo ni kweli kwamba Chadema kama vyama vingine vya upinzani imekuwa inahujumiwa vya kutosha na CCM kwa kushirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa, kasoro kadhaa ndani ya chama hicho kinarahisisha hujuma hizo.

Kama kuna kosa ambalo linaweza kabisa kugharimu uhai wa Chadema ni uamuzi wake wa kumpokea Lowassa mwaka 2015. Ni hivi, huhitaji kuwa mwelewa wa stadi za siasa kama mie mtumishi wako kubaini kwamba ni ukosefu wa busara wa hali ya juu kwa Chadema kumwandama Lowassa tangu Februari 2006 hadi Julai 2015 - miaka tisa hiyo - huku wakimtaja kama “papa la ufisadi,” kisha kumpokea takriban miezi mitatu tu kabla ya uchaguzi mkuu na kumfanya mgombea wao wa nafasi ya urais.

Kibaya zaidi, Lowassa huyo waliyempokea alikuwa “makapi” ya CCM. Again, haikuhitaji busara kubwa kufahamu kuwa kama hata CCM na ubovu wake ilimwona Lowassa hawafai, sijui Chadema walikuwa wanategemea nini kutoka kwake.

Wanufaika wakubwa wa uamuzi huo mbovu ni

(a) Lowassa mwenyewe: hebu fikiria, watu waliokuandama kwa miaka tisa mfulizo, wanapohangaika kuzunguka nchi nzima kukanusha kilekile walichokuwa wakikutuhumu…Naam, badala ya kusaka urais, kampeni ya Lowassa huko Chadema ilitawaliwa na ajenda moja kuu: Lowassa sio fisadi. Na waliokuwa wakisema hayo ni hao hao waliokuwa wakimuita fisadi. Kwahiyo Chadema walimchafua Lowassa na kisha wakalazimika kumsafisha, tena kwa gharama kubwa, kwani tangu chama hicho kililazimika kuitosa ajenda yake muhimu ya kupinga ufisadi.

(b) CCM: Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa chama hicho aliniambia, namnukuu, “Bwana Chahali, uchaguzi huu ungekuwamgumu sana kwetu kutokana na skandali za miaka 10 tunayomaliza. Lakini jamaa zetu wameturahisishia kwa kukwepa kuzungumzia ufisadi baada ya kumpokea mwanasiasa aliyekuwa kama nembo ya ufisadi kwenye chama chetu…”

Kwa kuitelekeza ajenda ya vita dhidi ya ufisadi, sio tu CCM walipata ahueni bali pia wakaipora ajenda hiyo na kuifanya sera muhimu ya mgombea wao Magufuli.

(c) Kitengo: Idara ya Usalama wa Taifa imekuwa ikivihujumu vyamavya upinzani nonstop. Lakini kwa Lowassa (ambaye kitambo alikuwa na “mahusiano mazuri” na taasisi hiyo) kuhamia Chadema, ilitoa fursa kubwa kwa Idara hiyo kuingiza lundo la watu wao, sambamba na kutengeneza mazingira ya kujenga mtandao wa watoa habari ndani ya chama hicho. Hiindio athari kubwa zaidi ya uamuzi wa kumpokea Lowassa: Chadema imesheheni mapandikizi yanayopigana kufa na kupona kukiangamiza chama hicho kutokea ndani.

Lakini hata tukiamua kusema “yaliyopita si ndwele, tugange yajayo,” bado kuna maswali magumu ambayo Chadema wanapaswa kujiuliza lakini wanayakwepa makusudi kwa sababu hawataki “kumuudhi Mbowe.” Maswali hayo ni pamoja nahilo kubwa zaidi la ujio wa Lowassa. Kwa mfano, ni kweli kwamba Lowassa “alinunua” nafasi hiyo? Ni wazi kuwa kama ni kweli, lazima mtu flani alipaswa kung’oka na Lowassa.

Lakini hata tukiamua kumsahau Lowassa, je nani alimfikisha Mashinji kwenyenafasi ya Ukatibu Mkuu? Je kama tunakubaliana na “sizitaki mbichi hizi” za Chadema kuhusu Mashinji, kwamba ni “pandikizi la CCM,” je ni nani aliyelifikisha “pandikizi hilo” hadi kwenye nafasi nyeti na muhimu wa Ukatibu Mkuu wa chama? Na je kama Mashinji ni pandikizi, huyo “aliyembeba” mpaka kufikia ukatibu mkuu nae sio “pandikizi” pia?

Kitambo, mie nimekuwa nikionyesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa kitengo cha intelijensia cha chama hicho (kama bado kipo hai)

Ni muhimu kukumbuka kuwa moja ya sababu zilizopelekea Chadema kuwa ilipo leo ni kuibua skandali mbalimbali za ufisadi zilizogubika utawala wa Jk, kuanzia Richmond, EPA, Kagoda, Buzwagi, Kiwira, nk. Na kilichowezesha chama hicho kuwa kinara wa kuibua slandali hizi ni intelijensia ya chama hicho ambayo sio tuilikuwa nzuribali pia iliaminiwa na baadhi ya watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa waliofikia hatua ya kujitoa mhanga kukipa chama hicho siri za serikali.

Lakini yaelekea sasa intelijensia pekee iliyobaki ya Chadema ni ramli za “jasusi” Yeriko

Ungetegemea “jasusi” akiwezeshe chama chake kufanya kile majasusi hukifanya: PREEMPTION. Yaani kabla Lowassa hajatangaza kuhama, majasusi wa chama hicho wangeweka hilo hadharani, na pengine kumtimua kabla hajahama. Kabla Waitara, sijui Meya wa Arusha, kabla ya Mr Zero Sumaye hajahama, na jana, kabla Mashinji hajahama, wao ndio wangechukua first step.

Kusubiri mtu atangaze kuhama ndio waje na porojo za “oh ndio maana hatukumpa tena Ukatibu Mkuu,” ni kutufanya - ashakum si matusi - mafala.

Lakini hii hama hama ina atahri zozote kwa Chadema? Well, tofauti na majigambo kuwa hamahama haina athari zozote, kwamba “acha tu waondoke,” ukweli ni kwamba hama hama hiyo ina athari kubwa lakini sio za hapo kwa hapo.

Hebu jiulize katika muda huu, ukimsikia Mbunge flani wa Chadema akidai kuwa kamwe hawezi kuhamia CCM, UTAMWAMINI? Kuwa mkweli. Maana hata akina Lowassa,

Sumaye

na Mashinji

walisema kamwe hawawezi kuhamia CCM, lakini baadaye wakahamia huko.

Kwahiyo moja ya athari za harakaharaka ni kwamba kwa sasa ni vigumu kumwamini mwanasiasa yeyote yule wa Chadema anayedai hatohama chama hicho/hatojiunga na CCM.

Lakini kubwa zaidi ni sintofahamu waliyonayo Watanzania wengi kuhusu mustakabali wa chama hicho kikuu cha upinzani hasa swali hili muhimu: WHO IS NEXT? NANI ANAFUATA (baada yaMashinji)?

In long run, hata wafuasi wa damu wa chama hicho wanaweza kupoteza imani kwa sababu hawajui “kesho nani atatangaza kuunga mkono jitihada.”

Pengine athari kubwa zaidi ya zote ipo kwenye ukweli kwamba kundi muhimu - na kubwa zaidi - la wapiga kura nchini Tanzania ni watu wasio wanachama wa chama chochote. Hawa ndio wanaopaswa kushawishiwa kukisapoti chama husika na/au mgombea wake. Ni hivi, CCM haihitaji kuwashawishi wafuasi wake kukipigia kura chama hicho. Na CCM haihitaji kuwashawishi wafuasi wa upinzani wakipe kura chama hicho. Kadhalika, vyma vya upinzani navyo havihitaji kuwashawishi wana-CCM wavipigie kura. Vilevile havihitaji kuwashawishi wafuasi wao wavipigie kura vyama hivyo. Kundi linalohitaji kushawishiwa kutoa kura ni hilo la wasio na vyama. Na hawa kwa sasa wanaweza kuwa wameanza kupoteza matumaini kwa Chadema. Inafikia mahala watu wanasema “kukipigia kura chama hiki ni kupoteza kura yangu.”

Kadhalika, japo Mashinji amehama akiwa Katibu Mkuu wa zamani, ukweli ni kwamba huyu ni katibu mkuu wa pili wa chama hicho “kukimbia.” Na kibaya zaidi, MASHINJI ANAJUA MENGI. Mark these words: Tutamsikia sana huyu bwana. Na yawezekana akawa mtu hatari kabisa aliyetoka Chadema. Time will tell.

Nimalizie uchambuzi huu kwa kutanabaisha kuwa ni wazi utawakera wahusika kwa sababu kama wenzao wa CCM, hawataki kabisa kukosolewa. Lakini kuuchukia ukweli hakuufanyi kuwa uongo. Sie wengine tutaendelea kusema ukweli hata kama itamaanisha kudhihakiwa na akina Yeriko.

Ushauri wangu kwa Chadema ni kutambua kuwa kuna tatizo la MAPANDIKIZI, na linahitaji kufanyiwa kazi haraka. Maana ili kuweza kutatua tatizo, hatua ya kwanza na ya muhimu kabisa ni kutambua uwepo wa tatizo. Unfortunately hadi muda huu, Chadema hukumbuka tu suala la mapandikizi pindi mmoja wao anapowakimbia. Hakuna anayehangaika kujiuliza WHO IS NEXT?

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali