Wapuuzeni Wanaomdhihaki #ErickKabendera Kwa 'Kukiri Makosa, Kulipa Faini.' Anayestahili Kudhihakiwa Ni JIWE Aliyesalimu Amri Shinikizo La Mabeberu

Jana asubuhi nilitumiwa ujumbe na mdau mtu wangu mmoja wa karibu ambaye mara kwa mara hunirushia breaking news kabla hazijatokea kwenye media. Katika ujumbe huo alinieleza kuwa huenda mwanahabari Erick Kabendera angetolewa jela. Niliandika twiti “Huenda Erick anaweza kuachiwa leo. Tumuweke kwenye sala/dua zetu,” lakini siku-post twiti hiyo kwa kuhofia kuwa endapo taarifa hizo zingekuwa na walakini, zingeishia kumuumiza Erick na watu wengine.

Baadaye nikaona huko Twitter kuwa kuna shtaka limeondolewa kutoka katika mashtaka matatu yaliyokuwa yakimkabili. Na hatimaye ndio zikapatikana habari njema kuwa Erick amechiwa huru.

Hata hivyo, japo wengi wetu tuna furaha kuwa mwenzetu amerudi uraiani, ukweli kwamba kesi yenyewe dhidi yake ilikuwa feki, iliyotungwa kwa sababu za kionevu tu, kwa hakika haya ni maumivu ambayo yatabaki nasi pengine milele.

Erick alikamatwa muda mfupi baada ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya afisa wa Hazina, kitengo cha Umoja wa Ulaya (EU), marehemu Leopold Lwajabe (wa kwanza kulia)

Leopold Lwajabe (right) is seen in this undated

Marehemu Lwajabe ambaye alikuwa mshirika wa Erick, aliuawa kinyama mno.Kabla ya kumuua, watesi wake walimteka, wakamtesa, WAKAMBAKA, kisha wakamuua.

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika, kuuawa kwa Lwajabe kulitokana na maagizo ya Jiwe na mpwa wake huko Hazina, ambapo majahili hao walihisi kuwa marehemu alikuwa na nyaraka zenye uthibitisho wa ufisadi wa kutisha wa fedha za wahisani kwa nchi yetu.

Erick alikamatwa kwa sababu hadi wanamuua marehemu Lwajabe, watesi hawakufanikiwa kupata chochote kwake, na wakahisi tena kuwa huenda nyaraka hizo amekabidhiwa Erick ambaye ana mawasiliano na watu wengi muhimu ndani na nje ya Tanzania.

Kwahiyo, kilichopelekea marehemu Lwajabe atekewe, ateswe, abakwe na hatimaye auwawe ni HISIA tu. Na kilichopelekea Erick akamatwe na kuzushiwa mashtaka mazito na hatimaye kusota jela kwa miezi sita ni HISIA tu.

Na kwa vile leo ni maadhimisho ya miaka miwili tangu mie mtumishi wako na Watanzania wengine kadhaa kutangazwa kuwa ni #WatuHatari, ni vema kugusia jinsi utawala wa Jiwe ulivyogeuza HISIA kuwa FACTS. Na mara nyingi wala sio hisia bali uzushi tu.

Angalia mfano wa huyo mbwa wa Jiwe, Musiba. Tanzania haijawahi kuwa ni kiumbe hatari kabisa kama huyu. Hadi muda huu, exactly miaka miwili baada ya press conference yake ya kwanza ya kuchafua watu, ambayo ilitulenga akina sie, shetani huyo ameendelea nostop kuzusha tuhuma nzito, sambamba na kufanya udhalilishaji mkubwa kwa kila anayeona anafaa kuandamwa. Mie mtumishi wako nimekuwa punching bag la majinuni huyu kwa muda mrefu tu.

Na juzi, kiumbe huyu hatari kuliko virusi vya Corona aliitisha press conference akidai kuwa Zitto anataka kumuua.

Unaweza kujiuliza “sasa mtumishi, ishu ya Musiba inaingia vipi kwenye suala la Kabendera?” Nadhani nimeshatanabaisha hapo juu kuwa masuala haya yanahusiana kwa sababu moja kuu: ukandamizwaji wa haki. Ukandamizwaji wa haki unaoruhusu HISIA kuwa mashtaka. Ukandamizwaji wa haki unaoruhusu uzushi kuwa tuhuma. Ukandamizwaji wa haki unaowezesha utekaji, utesaji, ubakaji na mauaji. Ukandamizwaji wa haki uliopelekea Kabendera sio tu akae jela miezi sita bali pia kulazimishwa kukiri makosa feki, sambamba na kumtwanga faini kubwa kabisa. Huu ni unyama mkubwa kabisa.

Lakini cha kusikitisha sio tu kwamba Kabendera amefanyiwa unyama huo, bali pia kuna Tito Magoti na mwenzie Gyan ambao kama ilivyokuwa kwa mwandishi huyo, wapo jela kwa mashtaka ya kutungwa tu. Lakini pengine kubwa zaidi ni ukweli kwamba wakati tunafahamu kuhusu Kebendera, Magoti na Gyan, inaelezwa kuwa kuna MAMIA ya watu wasio na hatia wanaoozea jela. Licha ya kutokuwa na hatia, bahati mbaya zaidi kwao ni “hawana majina,” kwa maana kwamba “sio watu maarufu” ambao tunaweza kuwapigania kwa alama ya reli #FreeNaniliu

Kitu kimoja kilichonisikitisha sana jana ni kuona baadhi ya watu wakimdhihaki Kabendera kwa “kukiri makosa, kuomba msamaha na kulipa faini.” Siwalaumu. Most of them wanafanya dhihaka hizo huku wamejificha kwenye fake IDs.

Lakini kilichonikera ni kwa hao wanaomdhihaki Kabendera kutojibidiisha kufahamu ukweli uliopelekea mwanahabari huyo kuachiwa jana. Jasusi wako ninakupa exclusive hii: Kabendera ameachiwa baada ya shinikizo zito alilopewa Jiwe na baadhi ya “mabeberu” ambao walitishia kutochangia kwenye bajeti ijayo. Na kwa taarifa tu, licha ya kelele za majigambo “tupo vizuri,” hali ya uchumi huko serikalini ni mbaya, na laiti mabeberu wakigoma kutoa misaada, hali itakuwa mbaya zaidi.

Kwahiyo, kama kuna wa kudhihakiwa basi ni Jiwe, mwanasiasa laghai anayewaaminisha wadanganyika kuwa yupo ngangari dhidi ya mabeberu lakini wakimtikisha kidogo tu anakuwa mdogo kama piritoni. Yaleyale ya mikataba ya madini.

Hizo porojo kuwa sijui Kabendera kalipa milioni 100 na anapaswa kumalizia “deni” ndani yamiezi sita, ni ile Waingereza wanaita “to save a face,” kwa lugha ya mtaani wanasema “kuua soo.”

Nihitimishe kwa kusema haya: POLE SANA ERICK, LAKINI PIA HONGERA KWA UJASIRI WAKO MAANA KUWA JELA KWA MIEZI SITA TENA KWA MASHTAKA FEKI SIO JAMBO RAHISI. MWENYEZI MUNGU YU NAWE, ATAKULIPIA DHIDI YA WATESI WAKO. NA HAO WANAOKUDHIHAKI KUWA WAPUUZE TU.

Ndimi jasusi wenu,

Evarist Chahali