[Tumia VPN Endapo Link Haifunguki] Uchambuzi Wa Kiintelijensia Kuhusu Urais Kwa Tiketi Ya Chadema: Nafasi za Mbowe,Lissu,Msigwa, Nyalandu Zikoje?

Kuna sehemu moja tu inayoweza kukidhi kiu yako ya uchambuzi wa kina kuhusu takriban kila linalohusu Uchaguzi Mkuu ujao, wagombea na nafasi zao, siasa za wazi na za siri ndani ya vyama vyao, mtazamo wa wanachama na wananchi kwa ujumla. Sehemu hiyo ni kijarida hiki cha #BaruaYaChahali.

Kabla ya kuingia kwenye uchambuzi husika, naomba msaada wako katika dhamira yangu hii

Twende kwenye uchambuzi wa Kiitelijensia kuhusu kinyang’anyiro cha Chadema kupata mgombea wake wa nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu ujao hapo Oktoba. Kutokana na kutingwa na majukumu, ninalazimika kufupisha uchambuzi huu.

Somo: Urais Wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Kwa Tiketi Ya Chadema

Lengo: Kubaini nafasi za wagombea waliojitokeza

Walengwa (Subjects):

  • Freeman Mbowe.

  • Tundu Lissu.

  • Peter Msigwa.

  • Lazaro Nyalandu

Mbinu ya uchambuzi: Kutengeneza Maana Katika Taarifa Mchanganyiko (Making Sense in Complex Data)

  • Uchambuzi wa Miendendo (Pattern Analysis)

  • Uchambuzi Linganishi (Comparative Analysis)

Utangulizi: Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani tarehe 25 Oktoba 2020 (kwa kuzingatia chaguzi kuu zilizopita ambapo siku ya uchaguzi huangukia Jumapili ya mwisho ya mwezi Oktoba). Japo inatarajiwa kuwa vyama kadhaa vya siasa vitashiri uchaguzi mkuu huo, vinavypaswa kupewa kipaumbele kiintelijensia ni CCM, Chadema na ACT-Wazalendo. Vyama vingine vitatu ambavyo havina umuhimu kiintelijensia ni NCCR-Mageuzi, CUF na TLP ambavyo kwa upande mmoja vinaisaidia CCM na upande mwingine vinawahujumu Chadema na ACT-Wazalendo.

Hadi wakati uchambuzi huu unafanyika, wanachama wanne wa Chadema wametangaza nia ya kuwania urais. Wanachama hao ni Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho;

Freeman Mbowe.

Tundu Lissu ambaye licha ya kuwahi kuwa mbunge na mnadhimu wa kambi ya upinzani, ni mmoja wa wanasheria wa chama hicho japo kwa sasa yupo Ubelgiji anakopata matibabu;

Tundu Lissu speaks out after loss of Parliamentary seat - The Citizen

Peter Msigwa ambaye ni Mbunge wa chama hicho jimbo la Iringa Mjini;

LIVE: PETER MSIGWA AKITANGAZA NIA YA KUGOMBEA URAIS KUPITIA ...

na Lazaro Nyalandu ambaye licha ya kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kati pia mwanachama mwandamizi wa chama hicho baada ya kujiunga nacho kutoka CCM

Lazaro Nyalandu - Wikipedia

Mantiki ya kutumia mbinu ya uchambuzi wa kiintelijensia ya “Kutengeneza Maana Katika Taarifa mbalimbali” imejikita kwenye ukweli kwamba licha ya uchambuzi kuangalia wagombea wanne, lengo lao lipo ndani ya mafaniko ya chama chao. Kwahiyo ni kama kitu kimoja kilichogawanyika sehemu nne ambazo baadaye zitarudi tena kuwa kitu kimoja (hopefully!)

Mantiki nyingine ya kutumia mbinu hiyo ni ukweli kwamba licha ya wagombea hao kuwa wa chama kimoja, kila mmoja ana turufu na mapungufu yake. Mbinu ya uchambuzi wa mienendo itasaidia katika kubaini turufu na mapungufu ya kila mmoja na hivyo kujenga msingi wa kufahamu nafasi zao kwenye kupatikana mgombea mmoja atakayebeba bendera ya chama hicho kwenye kinyang’anyiro cha urais hapo Oktoba.

Mbinu ya uchambuzi linganifu itasaidia kubaini nguvu na udhaifu wa wagombea hao.

Uchambuzi wa Mienendo (PatternAnalysis):

Mbowe:

Kuingia kwa Mbowe kwenye kinyang’anyiro hicho kumekuja siku chache tu baada ya kupatikana taarifa kuwa ameshambuliwa na watu wasiojulikana. Wakati Watanzania wakisubiri maelezo zaidi kuhusu nini hasa kilimsibu, baada ya jeshi la polisi kudai kuwa “alikuwa amelewa chakari,” ghafla ikatangazwa kuwa nae anataka kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.

Yayumkinika kutanabaisha kuwa “Mbowe ni Chadema, na Chadema ni Mbowe,” kutokana na nafasi yake kama Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho lakini pia kama mwanasiasa mwenye nguvu kuliko wote ndani ya chama hicho.

Mbowe aliwahi kugombea urais mwaka 2005 na kushika nafasi ya tatu. Mwaka 2010 alimpisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Dokta Willbrord Slaa kuwa mgombea na mwaka 2015 alimpisha Edward Lowassa kuwa mgombea kwa tiketi ya muungano wa UKAWA.

Kwamba anaweza kuwa mgombea mwenye nafasi ya kushinda, ni jambo linalojadilika lakini turufu yake ni uzoefu pamoja na nafasi yake ndani ya chama hicho. Kadhalika, ngome kuu ya Chadema ni kanda ya kaskazini, ambapo Mbowe ndiye mgombea pekee minogni mwa wanne hao anayetoka kanda hiyo.

Hata hivyo, kwa kuangalia mwenendo wa “siasa za Chadema,” ilitarajiwa kuwa Mbowe awe kama “mlezi wa wagombea urais,” badala ya yeye nae kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Hitimisho: Mbowe ametangaza kuwania urais kwa sababu kuu mbili. Moja ni “kuua mjadala kuhusu kushambuliwa kwake.” Na pili, uamuzi huo unalenga “kumjengea mazingira mazuri mgombea mmoja.” Nitafafanua.

Lissu:

Unaweza kurejea uchambuzi nilofanya awali kuhusu nafasi ya mwanasiasa huyo. Kwa kifupi, kama nilivyoeleza kwenye uchambuzi huo, nafasi yake kupitishwa kuwa mgombea wa chama hicho ilikuwa ikitegemea endapo hakutokuwa na wanachama wengine “wenye nguvu kama yake au zaidi.”

Hasara kubwa kwa Lissu ni kuwa kwake nje ya nchi kwa muda mrefu. Japo endapo akipitishwa na chama hicho anaweza “kupigiwa kura ya huruma” kutokana na yaliyomsibu katika harakati za siasa za Tanzania, ukweli kwamba wala haijulikani kama ataweza kurudi Tanzania, na endapo atakuwa salama pindi akirudi, inamyima nafasi flani.

Hitimisho: Licha ya kuwa na sifa stahili, intelijensia inabashiri kuwa hatopitishwa kuwa mgombea wa tiketi ya urais wa chama hicho.

Msigwa:

Uchambuzi huu hauoni nafasi kwa mwanasiasa huyo kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kwa sababu zilizo wazi: japo Msigwa ni mmoja wa viongozi waandamizi wa chama hicho, nafasi ya yeye kupitishwa mbele ya Mbowe, Lissu na Nyalandu ni ndogo. In fact, “technically,” nonexistent.

Hitimisho: Intelijensia inabashiri kuwa hatopitishwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho.

Nyalandu:

Alipoamua kuondoka CCM kwa hiari na kijiunga na Chadema Oktoba 2017, nilitanabaisha kwa twiti hii

Japo niliwataja Lowassa na Sumaye, katika twiti zangu kadhaa nilionyesha shaka kuhusu uwepo wao Chadema, na hata kubashiri Lowassa na Sumaye kurudi CCM

Tukiweka kando angalizo hilo, tofauti na wagombea wenzake, yaani Mbowe, Lissu na Msigwa, Nyalandu alikuwa na muda wa kutosha kujianda kwa ajili ya kuwania urais mwaka huu.

Kadhalika, tofauti na wagombea wenzake, Nyalandu alikuwa CCM hadi mwaka 2017 na hilo linaweza kumsaidia kuijua CCM vema zaidi ya wenzie.

Kifedha, yeye ni mgombea anayejimudu zaidi kiuchumi na anaweza “kuiokoa Chadema kwenye gharama za uchaguzi” kwa kutumia fedha zake mwenyewe.

Kadhalika, nafasi yake kama Waziri wa Maliasili na Utalii katika zama za Jk ilimwezesha kufahamiana na wanasiasa wenye nguvu huko Marekani ambao wanaweza pia kuwa na msaada kwake katika azma yake ya kuwania urais.

Hisia kuwa labda ataonekana kama ametumwa na CCM haina uzito sana kwa sababu hisia kama hizo hazikuzuwia Lowassa kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2015.

Swali ambalo Chadema wanaweza kujiuliza kwa minajili ya kujiridhisha tu ni kwanini Nyalandu “hajaguswa na Magufuli” licha ya jitihada za Waziri Kigwangalla kudai Nyalandu alihusika na ufisadi alipokuwa Waziri. Je anaweza kushinda kinyang’anyiro hicho na kuwa mgombea wa Chadema kisha akatangaza kurudi CCM na kuiacha Chadema ikiwa haina mgombea urais? Time will tell

Hitimisho: Intelijensia inabashiri kuwa Nyalandu ndiye atakayepitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema. In fact, Mbowe kutangaza kuwania urais kunalenga “kumfariji Lissu” pindi jina Nyalandu - badala ya yeye Lissu - kupitishwa. It would make sense, kwamba “kama mie Mwenyekiti niliomba dhamana ya kugombea na sikupitishwa, kwanini iwe nongwa kwako Makamu Mwenyekiti wa chama?”

Uchambuzi Linganifu (Comparative Analysis):

Mbowe: Kama intelijensia ilivyotanabaisha hapo juu, ametangaza kugombea kwa minajili ya kuondoa lawama pindi kupitishwa kwa Nyalandu kutamkwaza Lissu. Licha ya kuwa mwanasiasa mwenye nguvu kuliko wote ndani ya Chadema, na mwenye uzoefu wa kugombea urais, intelijensia inabashiri kuwa hatopitishwa au atajitoa pindi Nyalandu akipitishwa.

Lissu: Licha ya kuwa mwanasiasa mwenye wasifu wa kuvutia zaidi ya wagombea wenzie, kwa maana almanusra auwawe kutokana na msimamo wake imara katika kupigania maslahi ya Watanzania, uwepo wake nje ya nchi na kutokuwepo uhakika kama ni salama kwake kurudi Tanzania, “kunamharibia” nafasi yake kwenye kinyang’anyiro hicho.

Msigwa: Intelijensia inamuona kama msindikizaji tu. Huenda pia nae anafahamu hilo ndio maana ametanabaisha kuwa asipopitishwa kuwania urais atarudi kugombea ubunge. Japo si vibaya kuwa na Plan B, “kuwa na jicho kwenye urais na ubunge” kwaweza kumfanya aonekane mwenye tamaa. Lakini kubwa zaidi ni nafasi finyu kwake kupitishwa.

Nyalandu: Intelijensia inamuona kuwa ndiye atapitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema. Hata hivyo, intelijensia inadhani Chadema wanapaswa kujiridhisha ili “wasirudie kosa kama kwa Lowassa.” Ukweli kwamba “Nyalandu amenusurika siasa za chuki za Magufuli” unaweza kuwa “bahati yake tu” lakini pengine “kuna namna.”

Hitimisho kuu:

Intelijensia sio sayansi timilifu (exact science). Uchambuzi huu umetegemea zaidi uelewa wa mchambuzi kuhusu siasa za chadema, uchaguzi na Tanzania kwa ujumla. Katika siasa, siku moja inaweza kuwa sawa na muongo decade) mzima ilhali wiki katika siasa inaweza kuwa sawa na karne. Lolote linaweza kutokea kati ya sasa na wakati Chadema itakapopitisha mgombea wao. Na kubwa zaidi, ukweli kwamba ufanisi wa Chadema katika mchakato huu utategemea kujizatiti kwao kukabiliana na hujuma za CCM na serikali yake (eneo ambalo uchambuzi huu haukuliangalia), haitokuwa jambo la ajabu endapo matokeo ya kinyang’anyiro hicho yatakuwa tofauti.

Ndimi jasusi wako

Evarist Chahali

NB Usisahau kuwakumbusha watu kuhusu umuhimu wa VPN