Tujiulize: Tanzania Yetu Inaelekea Wapi?

Kuna Mambo Ya Ajabu Sana Yanaendelea Katika Nchi Yetu

Kwanza naomba radhi kwa kuchelewa kukufikishia “Barua Ya Chahali.” Hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu, sababu ambazo pia zimechangia kupotea kwangu kwa muda huko Instagram.

Dhamira yangu ni kuhakikisha unakutana na barua hii kwenye inbox yako kila unapoamka Jumatatu asubuhi. Natumaini nitaweza kutekeleza azma hiyo kwa matoleo yajayo ya jarida hili.

Twende kwenye mada ya wiki hii. Ni mambo ya kushangza na kwa hakika ya kusikitisha yanayoendela huko nyumbani. Ijumaa iliyopita, jamaa yangu mmoja alikwenda Benki ya Posta kubadili Dola za Kimarekani 5,000. Ni fedha halali na alikuwa na uthibitisho kuwa ni fedha halali.

Lakini kilichotokea hapo kimenifanya nijiulize mfululizo kuhusu mwelekeo wa Tanzania yetu. Awali wahusika hapo benki walitaka uthibitisho wa kipato cha huyo jamaa yangu, akawaonyesha. Yeye ni mfanyabiashara wa kimataifa, na baadhi ya bidhaa/huduma zake hununuliwa kwa fedha za kigeni.

Awali jamaa yangu alidhani suala hilo ni taratibu za kawaida tu na aidha Benki hiyo itakubali kumbadilishia fedha hizo au itakataa. How wrong! Muda mfupi baadaye akaja Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi

Image result for sabasaba moshingi

Basi huyu Bwana akamuita mwenzie Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Simu TTCL Waziri Kindamba (sijui anahusika vipi)

Image result for waziri kindamba

na matokeo yake huyo kijana amekuwa kizuizini hadi leo, kwa “kosa” la kutaka kubadilisha Dola Za Kimarekani 5000.

Lakini ukidhani labda tatizo ni idadi ya dola hizo, jana nimepewa taarifa kuwa jamaa mmoja amekamatwa alipoenda benki kubadili Dola za Kimarekani 200. Yes, just USD200, na mpaka muda huu yupo rumande.

Pia nimepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kadhaa wanaomiliki maduka ya kubadilishia fedha za kigeni (bureaux de change…angalizo: moja ni “bureau de change,” zaidi ya moja ni “bureaux de change”) wa Arusha na Dar, ambapo wote wanasema kuwa maduka yao yamefungwa huku baadhi yao wakiwa wameporwa vifaa vya ofisini kama vile kompyuta, pia nyaraka, hata simu na baadhi wanasema waliporwa maelfu ya fedha za kigeni.

Mie sio mchochezi lakini kama ikitokea una fedha za kigeni unazotaka kuzibadilisha, ukitia mguu kwenye taasisi ya serikali utakuwa kama umeenda kuvutia bangi kituo cha polisi. Njia pekee ya kupata au kuuza fedha za kigeni ni kwenye “black market.” Na sio kama nahamasisha watu kuvunja sheria, lakini huu uwendawazimu unaoendelea kuhusu suala hili la fedha za kigeni, unalazimisha kuibuka upya kwa “black markets.”

Kwamba ni muhimu kudhibiti biashara ya kubadilisha fedha za kigeni, hilo halina mjadala. Lakini huwezi kudhibiti biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa (a) kufunga maduka yote ya kubadilishia fedha za kigeni (b) kukamata kila mtu anayekwenda benki kubadili fedha za kigeni. Huu ni wendawazimu.

Lakini kuna trend ya kutisha zaidi. Watu kadhaa wamenieleza kuwa katika siku za hivi karibuni wamejikuta wakiitwa benki kuulizwa kuhusu fedha zao. Kwa mfano, akaunti yako ikiwa na shilingi miliono kadhaa basi si ajabu ukipokea wito kutoka benki ili ukawapatie maelezo ya kueleweka kuhusu fedha hizo.

Hatua hizi zinawalenga wanyonge, watu waliovuja jasho na kujipatia kipato halali. Hatua hizi haziwahusu majambazi waliopo Hazina ambao ripoti ya maalum ya CAG ilionyesha “wamepoteza” shilingi TRILIONI 2.4

Mwisho, takriban nusu ya ninaowatumia barua hii kila wiki hawana muda wa kuisoma. Japo simlazimishi mtu kusoma lakini sipendezwi na watu wanaowapotezea muda wenzao: wanajisajili kutumiwa jarida, wakitumiwa wanapuuza jardia husika. Nitaanza kupunguza idadi ya waliojisajili ili nibakiwe na wasomaji wa dhati wa jarida hili.

Tukutane wiki ijayo