Tuhuma Za Ushoga Kama Silaha Ya Wanyanyasaji Mtandaoni: From Musiba To Kigogo.

Moja ya mambo mabaya kabisa kutokea katika Tanzania yetu ni utawala wa kidhalimu wa John Magufuli. Makala hii haiwezi kutosha kuorodhesha kila baya lililofanywa na utawala huo, lakini kwa minajili ya makala hii, ni muhimu kutaja silaha moja muhimu kwa utawala huo katika kampeni zake endelevu dhidi ya Watanzania mbalimbali. Silaha hiyo ni tuhuma za ushoga.

Ushoga kwa upana wake ni mahusiano ya kimwili kati ya mwanaume na mwanaume mwingine. Japo pia neno ushoga hutumiwa kwenye mahusiano ya jinsia moja baina ya wanawake, kwa kawaida mahusiano ya kimwili kati ya mwanamke na mwanamke hufahamika kama usagaji.

Tofauti na hisia kwamba ni kitu kilicholetwa na mitandao, utandawazi au mabeberu, ushoga umekuwepo Tanzania miaka nenda miaka rudi. Nakumbuka wakati nikiwa mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa katikati ya miaka ya 1990s, baa moja maarufu maeneo ya Magomeni, iliyojulikana kwa jina la “Kwa Macheni” ilikuwa ni kama “sehemu huru” kwa mashoga ambapo haikuwa vigumu kuwatambua kutokana na walivyojiremba na hata walivyotembea.

Lakini pia eneo lililokuwa likipendelewa sana na mashoga ni kumbi za muziki za taarabu. Kwa upande wa bendi za muziki wa dansi, takriban kila sehemu kulipokuwa na shoo za “wana Njenje” kulikuwepo idadi kubwa ya mashoga. Kama niliyotanabaisha awali, haikuwa ngumu kuwatambua kutokana na “jinsi walivyo.”

Yayumkinika kusema kuwa maendeleo ya teknolojia nchini Tanzania, hususan matumizi ya mitandao ya kijamii, imechangia kufanya “ushoga kwenda mainstream.” Hapa namaanisha sehemu kama mtandao wa kijamii wa instagram ambapo mashoga mbalimbali wamekuwa wakijitangaza hadharani.

Hata hivyo, kuashiria unafiki wa hali ya juu wa Watanzania, akaunti nyingi za mashoga huko instagram zina maelfu ya followers huku baadhi wakiwa na followers zaidi ya laki moja. Unaweza kujiuliza, “inawezekanaje kwenye nchi yenye watu wanaouchukia ushoga kwa dhati, shoga akawa na followers laki moja mtandaoni?” Jibu ni kwamba baadhi ya wanaopinga ushoga hadharani sio tu wanaounga mkono hali hiyo bali wengine ni wahusika kabisa.

Lakini unafiki huo haupo Tanzania tu. Disemba mwaka jana, Jozsef Szajer, mwanasiasa mmoja maarufu wa Romania - nchi yenye msimamo mkali sana dhidi ya ushoga - alifumwa kwenye pati ya mashoga jijini Brussels, Ubelgiji, na akajaribu kutoroka kwa kuruka ukuta baada ya polisi kuvamia pati hiyo kwa kukiuka kanuni za kujikinga na korona.

Licha ya kuwa kiongozi wa chama cha Fidesz cha Rais wa nchi hiyo Viktor Orban, ambacho kina msimamo mkali dhidi ya ushoga, mwanasiasa huyo pia alishiriki kampeni za wazi dhidi ya mashoga na hakusita kueleza upinzani wake dhidi ya tabia hiyo. Kumbe muda wote huo alikuwa shoga pia.

Tukirejea Tanzania, zama za Magufuli zilishuhudia tuhuma za ushoga zikitumiwa kama silaha ya utawala huo dhalimu dhidi ya watu wasio na hatia lakini waliotazamwa na utawala huo kama wahaini.

Kwa kumtumia mtu hatari kabisa katika historia ya Tanzania, Musiba, Magufuli aliwadhalisha watu mbalimbali kwa kuwatuhumu ni mashoga kwa kutumia magazeti ya Musiba.

Mmoja wa wanasiasa wastaarabu kabisa katika historia ya siasa za Tanzania, marehemu Seif Sharif Hamad (Mola amlaze mahali pema peponi), hakuweza kunusurika kwenye kampeni endelevu ya uadhalilishaji iliyoendeshwa na Magufuli kwa kumtumia Musiba na magazeti yake.

Lakini si Maalim Seif pekee aliyekuwa mhanga wa udhalilishaji huo, mie jasusi/mtumishi wako pia nilikuwa kama “punching bag” la Musiba ambapo aliyatumia magazeti yake kunichafua atakavyo, mfululizo. Na kama ilivyokuwa kwa wahanga wake wengine, alinituhumu ushoga pia.

Sasa kuna tabia mbili muhimu za hizi tuhuma. Kwanza, wakati tuhuma za feki za ushoga zinauma kwa mtu yeyote yule, huumiza zaidi kwa “watu wa mizigo.” Na japo sioni sifa kutamka hili, huku nyuma -kutokana na asili ya kazi ya ujasusi - nilikuwa “mtu wa mizigo.” Takriban asilimia 99 ya watu wa kitengo, JWTZ na polisi ni “watu wa mizigo.” Kwa kitengo ni zaidi kwa sababu kazi hiyo hutegemea zaidi “wanawake warembo kupindukia” kunasa siri mbalimbali.

Tabia nyingine muhimu ya tuhuma za ushoga ni kwamba mara nyingi watu wanaopenda kutoa tuhuma hizo dhidi ya wenzao, wenyewe ndio huwa mashoga.

Hii inafanana na uhusiano kati ya “wanaume wenye wivu sana kwa wenza wao” na tabia ya uzinzi. Mara nyingi wanaume wazinzi huwa mstari wa mbele kurusha tuhuma za kuchepuka dhidi ya wenza wao. Labda “guilty consciousness” huwasuta, lakini pia huenda wanatumia mbinu hiyo kuficha dhambi zao.

Kwa Musiba pia kulikuwa na tuhuma kuwa yeye pia anajihusisha na vitendo vya ushoga na ndio maana tuhuma za ushoga zilikuwa nyenzo yake muhimu katika kuwadhalilisha watu aliotumwa na Magufuli kuwahujumu.

Lakini katika mazingira ya kawaida tu, mwanaume rijali ambaye muda wote yupo bize na maisha ya wanaume wenzie, basi hiyo ni ishara ya wazi kuwa “sio ridhki.”

Kwa bahati mbaya, wakati kifo cha Magufuli kilipelekea “kifo cha Musiba” kwa maana ya anguko lake yeye binafsi na vyombo vyake vya habari, sambamba na kupoteza umaarufu kidogo aliokuwa nao - uliochangiwa na kasumba ya Watanzania kupenda ubuyu - na kubwa zaidi, kuondokewa na ile kinga ya kutukana watu apendavyo, aliibuka mtu mwingine “kumrithi” Musiba.

Huyu ni Kigogo.

Mtu ambaye sio tu amewazushia watu vifo ilhali wapo hai, lakini kama ilivyokuwa kwa Musiba, kila “mbaya wake” ni shoga. Binafsi nimekuwa mhanga wa matusi ya Kigogo tangu mwaka 2018. Sina uhasama nae na wala sijamuingilia kwenye fitna zake.

Pengine moja ya vyanzo vya hasira zake kwangu ni twiti yake hii ya kuniomba nimuondolee bloku (ambayo nilimpa kwa sababu ya matusi yake mfululizo dhidi yangu)

Hata hivyo, plot is thicker than that. Kwa uelewa nilionao, huyu mpenda matusi amekuwa akitumiwa na mtu mmoja wa Kitengo anaitwa NZOWA ambaye nae amekuwa katika kampeni endelevu ya kunidhuru.

Hapa sio mahala mwafaka kuongelea hilo lakini ninafahamu vema uhusiano baina ya wawili hao, na ndio maana mara kadhaa Kigogo amekuwa akifanya dhihaka kuhusu suala hilo. Mtu anayedhihaki janga lako ni zaidi ya haramia.

Na tusi maarufu zaidi la Kigogo dhidi yangu na wengineo anaowachafua ni tuhuma za ushoga. Na anapendelea silaha hiyo kwa sababu mbili. Kwanza, anajua jinsi inavyoumiza ,tu yeyote ambaye hajihusishi na vitendo hivyo.

Lakini pili, kama zilivyokuwepo tuhuma kuwa “Musiba anapenda kuwaita watu mashoga kwa vile yeye mwenyewe ni shoga,” ugomvi unaoendelea kati ya Kigogo na Martin Maranja umetoa “clue” muhimu kuhusu “kwanini Kogogo hupenda kumuita kila mtu shoga.”

Na mara baada ya Martin “kumpiga Kigogo na kitu kizito chenye ncha kali” Kigogo hakujibu tuhuma hizo kuhusu tabia hiyo ambayo amekuiwa akiitumia kwenye udhalilishaji wake dhidi ya watu kadhaa.

Je huu ndio mwisho wa mdhalilishaji huyu? Time will tell. Lakini hakuna marefu yasiyo na ncha. Nani alijua kuwa ipo siku Magufuli angekuwa marehemu? Nani alijua kuwa kuna siku Bashite ataufyata? Nani alijua kuna siku Sabaya “angenyea ndoo” (ashakum si matusi)? Na nani alidhani kuwa kuna siku Musiba angetokea kuwa “mdogo kama piritoni” kwa jinsi alivyo sasa"?

Hata kama hilo jawabu alilotupatia Martini kwenye swali “kwanini Kigogo hupendelea sana kuwatuhumu watu ushoga” (jawabu, kwa mujibu wa Martin, ni kwamba yeye mwenyewe anajihusisha na mchezo huo) haitoweza kumbadili Kigogo aache kuwa mrithi wa Musiba, ipo siku Kigogo atakuwa historia kama ilivyo kwa Musiba, Bashite au Sabaya. Pamoja na ujahili wote alionifanyia, siwezi kusema “ipo siku nae atakuwa kama Magufuli” kwa sababu mtu mwema hupasi kumuombea mwenzio mabaya.

Lakini Kigogo amefikishwa hapa alipo na makundi manne muhimu. La kwanza ni hao “watu wa serikali” waliokuwa wakimtumia kwa maslahi yao binafsi.

Kundi la pili ni baadhi ya wanaharakati ambao wamekuwa wakimtumia Kigogo kama attack dog wao. Yaleyale ya Magufuli kwa Musiba. Kuna dada mmoja aliwahi kunitumia ujumbe huo wa Kigogo akinisihi nim-unblock, na ndio akili ikanifunguka kuwa “kumbe hawa chama kimoja.”

Kundi la tatu ni Chadema. Sijui ni kwa kumbukumbu fupi au kutojielewa, chama hicho kimemsaidia sana Kigogo kufika alipo leo. Mengi ya matusi yake yamesambazwa zaidi na wafuasi wa chama hicho. Kibaya zaidi, baadhi ya viongozi wa chama hicho wamekuwa na uswahiba nae kiasi cha kuritwiti matusi yake.

Hata hivyo, shukrani za kipekee zimwendee Mheshimiwa Tundu Lissu aliyefanikiwa kuzima jaribio la Kigogo kupora uongozi wa chama hicho huku akihamasisha “kiingie mtaani.” Unaweza kusoma msimamo wa Lissu dhidi ya Kigogo HAPA

Na nilipompongeza Lissu kwa kukinusuru chama chake, Kigogo kama kawaida yake akanitukana kwa kutumia silaha yake muhimu ya kutuhumu ushoga.

Kundi la nne ni WATANZANIA WAPENDA UBUYU. Hawa ndio waliowezesha “demand and supply” - wao wana demand ya ubuyu, Kigogo ana unlimited supply ya ubuyu. Kwa bahati mbaya, hata Kigogo “akipotea” wapenda ubuyu hawa “watazalisha Kigogo mwingine.” Unfortunately, hii ndio Tanzania yetu.

Lakini tatizo sio tu hilo la demand and supply ya ubuyu, Watanzania wengi wanajiskia faraja kubwa kuona wenzao wasio na hatia wakidhalilishwa. Ndio maana pamoja na matusi yake mfululizo, hajawahi kujitokeza mtu yeyote wa maana kukemea matusi ya Kigogo. In fact, baadhi ya wafuasi wa matusi yake ni wasomi wanaoheshimika.

Nawatakia Jumapili njema