Toleo Maalum: Ripoti Ya CAG Imethibitisha Tunalokwepa Kusema Kuhusu MAGUFULI

Awamu ya Tano Ya MAGUFULI inaweza kuwa ya kifisadi zaidi kuliko zote zilizotangulia

Hatimaye mkwara wa Mtu Mfupi Ndugai umeshindwa kumzuwia CAG Profesa Mussa Assad kuwasilisha ripoti yake ya ukaguzi na udhibiti wa fedha za serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Hilo dogo.

Kubwa ni (a) yayumkinika kuhitimisha kuwa jitihada za Mtu Mfupi Ndugai dhidi ya Profesa Assad kwamba “Bunge halitafanya kazi na CAG” zilikuwa zinafanywa kwa rimoti na Magufuli mwenyewe kwa sababu (b) ni dhahiri kuwa utawala wake sio tu umegubikwa na ufisadi mkubwa bali pia unaweza kuingia kwenye kumbukumbu za nchi yetu kama utawala wa kifisadi zaidi kuliko yote.

Watanzania wanapaswa kumuomba msamaha Rais Kikwete. Na hata Rais Mkapa. Na pengine hata Rais Mwinyi. Hawa wote - na hasa JK- tuliwaandama mno kuhusu ufisadi. Ikumbukwe kuwa pamoja na mapungufu yao, angalau hawakufanya jitihada za kutunyima access ya habari kuhusu wanavyotuongoza.

Naam, sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari ziliendelea kuwepo/kutumika, lakini hakuna mmoja wao anayefikia kiwango alichofikia Magufuli: sio tu amefanikiwa kuviziba mdomo vyombo vya habari bali pia ameanzisha “toilet papers” kadhaa zinazofanya kazi kuu mbili, kummwagia sifa kila kukicha na kutuandama tunaomkosoa kihalali.

Kwa bahati mbaya - au pengine makusudi - ishu hii nayo itakufa kimya kimya. Kwa upande mmoja, mbinu ya Magufuli kudhibiti vyombo vya habari itamkinga dhidi ya habari hii kuendelea kutawala vichwa vya habari. Kwa upande mwingine, “ukitaka kumficha kitu Mtanzania, kiweke kwenye maandishi. Na ushahidi mwepesi ni huu pichani

Angalia “idadi ya views” kisha linganisha na jitihada kubwa zinazofanyika kuhamaisha “views za YouTube” pindi wasanii wetu wanapotoa video zao. Aliyewaroga Watanzania alihakikisha wanapuuzia vitu vya muhimu na kuendekeza vitu vya ovyo ovyo. Bad news ni kwamba huyo aliyewaroga Watanzania naye alirogwa, akapata uchizi, akagongwa na basi la Skandinavia, akafariki papo hapo. What this means? HAMPONI (wanasema aliyekuroga akifa, huponi).

Lakini lawama hazijengi. Na mabadiliko huanza kwa hatua ndogo ndogo. Unaonaje badala ya kulaumu wengine, wewe binafsi ukawa mfano kwa kuanza kusoma taratibu ripoti hii kisha ukawaelewesha wengine ambao hawajabahatika kuisoma.

Ripoti hii ni muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu ambalo kwa hakika linaelekea kubaya. Magufuli anawahadaa Watanzania kuwa “vyuma vimekaza kwa sababu watu walizowea kupiga dili.”

Lakini ukweli mchungu ni kwamba vyuma vimekaza kwa sababu kuna ufisadi mkubwa kabisa unaoendelea kimyakimya, unaomhusisha Magufuli na genge lake la Kanda ya Ziwa. Na kama unahangaika kutafuta mfano hai, angalia ishu hii ya LUGUMI ambayo ni mtu wa karibu wa Magufuli kama alivyo Bashite.

Kwahiyo wakati Wadanganyika mnakebehiwa kwamba vyuma vimekaza kwa vile nyie ni wapigadili, akina LUGUMI wanazidi kufakamia keki ya taifa.

Na hapa bado hatujui mpwa wa Magufuli pale Hazina safari hii amefisadi kiasi gani, lakini ni muhimu kukumbuka kuwa wakati awali tulidhani pesa iliyopigwa Hazina ni TRILIONI 1.5, baadaye ikabainika kwamba kiwango halisi ni TRILIONI 2.4.

Nimalizie toleo hili maalum kwa kukusihi tena na tena, soma ripoti ya CAG, kisha waelimishe wenzetu ambao kwa sababu moja au nyingine hawawezi kuisoma. Ombi langu jingine kwako ni kutafakari mustakabali wa nchi yetu kwa kuzingatia lindi hili kubwa la ufisadi wa kihistoria. Hatma ya Tanzania yetu ipo mkononi mwako.

Nakutakia siku njema, tukutane Jumatatu ijayo