Toleo Maalum: Ishu ya CAG Chanzo ni Jiwe sio Bunge

Azimio la Bunge Kukataa Kufanya Kazi na CAG Linalenga Kuua Mjadala kuhuru Ripoti ya CAG 2018/2019

Awali nilitaka nisubiri hadi Jumatatu ijayo ndio niwatumie #BaruaYaChahali ikiwa na mada kuhusu azimio la Bunge kuwa halitofanya kazi na CAG.

Hata hivyo, nikakumbuka kuwa Watanzania ni mahiri mno kwa usahaulifu, na kwa vyovyote vile, kufikia Jumatatu watakuwa wameshasahau ishu hii ya CAG na Bunge. Nadhani tatizo sio usahaulifu as such bali kuwa na vipaumbele fyongo, maana kwanini watu haohao wanaosahau haraka mambo ya msingi huwa na kumbukumbu nzuri kwenye ubuyu? Tuliache hilo kwa leo.

Binafsi, licha ya kukasirishwa mno na uhuni uliofanywa na Bunge letu, lakini sikuona kitu cha ajabu kwa sababu kuu mbili. Kwanza, kwa muda mrefu Bunge letu limekuwa taasisi isiyo na umuhimu kwa wananchi hasa kutokana na CCM kutumiwa wingi wa wabunge wake kwa maslahi ya chama hicho na serikali yake hata pale maslahi ya wapigakura wa wabunge hao yanapokuwa hatarini. Hii imepelekea bunge kuwa mhuri wa kupitisha kila jambo linaloletwa na serikali ya chama hicho tawala.

Pili, bunge huru na linalowajibika kwa Watanzania lingemkwamisha sana Magufuli katika utawala wake wa kidikteta. Kwa kutambua hilo, akatumia nguvu za kidola na kichama kuwatisha wabunge wa CCM kwamba “wakorofi wote hawatorudi bungeni mwaka 2020.” Lakini kabla ya kutumia mbinu hii ya vitisho, utawala wa Magufuli ulitumia nguvu ya fedha ambapo inaelezwa kuwa mara kadhaa wabunge wa CCM walikuwa wakipewa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kuitetea serikali bungeni. Mamilioni hayo ni kama rushwa kwa wabunge hao, rushwa iliyokuwa na lengo la kuwafunga mbeleni kwa kigezo cha “si nilikupa hela yangu wewe?” Wanabaki na deni la fadhila.

Baada ya kulidhoofisha Bunge, Magufuli akapata bahati ya “mbuzi kufia kwa muuza bucha” pale Mtu Mfupi alipokumbwa na maradhi ambayo kwa kumtunzia heshima siwezi kuyataja hapa. Magufuli akamlipia gharama Mtu Mfupi akijua bayana kuwa huko mbeleni kibushuti huyo naye atakuwa na deni la fadhila.

Kwahiyo, bila kuzunguka sana, kimsingi uamuzi huo wa bunge dhidi ya CAG sio wa bunge as such bali ni wa Magufuli mwenyewe. Na Magufuli amechukua uamuzi huo kwa sababu kuu mbili.

Kwanza, azimio hilo la bunge kukataa kufanya kazi na CAG limewezesha kuua mjadala muhimu kuhusu kilichotokea kwa ripoti ya CAG kwa mwaka 2018/19 ambayo kwa mara ya kwanza imewasilishwa Ikulu kinyemela.

Magufuli ameua ndege wawili kwa jiwe moja: ameweza kutimiza azma yake ya kulifanya bunge liwe dhaifu lakini papo hapo ameweza kukwepesha mjadala kuhusu ripoti ya CAG. Kwahiyo hatutopata fursa ya kufamu yeye Magufuli na mpaweDoto pale Hazina wamekwapua kiasi gani zaidi ya zile trilion 2.4 tulizoambiwa katika ripoti ya CAG iliyopita.

Kuna angle nyingine katika ishu hii ya CAG. “Kosa” kubwa la CAG Profesa Assad kwa Magufuli ni dini yake. Sio siri kubwa Magufuli ni mdini kama alivyo mkabila na mwendekeza ukanda. Prof Assad ni mcha-Mungu kweli kweli, mtu wa swala tano.

Licha ya “kosa” hilo la dini yake, Profesa Assad ni msomi mwadilifu asiyekubali kuyumbishwa. Kwa profile hiyo anakuwa moja kwa moja tishio kwa Magufuli anayeiendesha nchi kama kampuni yae binafsi. Prof Assad ni kizingiti kwa mpwa wa Magufuli pale Hazina, na kizingiti kwa hiyo miradi ya ajabu ajabu inayoligharimu taifa mabilioni kwa matrilioni ya shilingi pasipo kuzingatia kanuni na taratibu za kisheria.

Yajayo yanatabirika

Tayari kuna mtu wa Kanda ya Ziwa ameshaandaliwa kuwa mrithi wa CAG. Endapo jitihada za kumtoa Prof Assad kwa mizengwe zitashindikana, basi watasubiri hadi Novemba mwaka huu ambapo inaelezwa kuwa muda wake wa kustaafu utakuwa umetimia.

Ukiongea na watu wengi watakwambia “sijui Tanzania yetu inaelekea wapi.” Jibu fupi ni kwamba Tanzania inaelekea kubaya. Magufuli anaipeleka Tanzania kusikofaa. Lakini hilo ni dogo kulinganisha na balaa kubwa linaloisubiri Tanzania yetu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Ni dhahiri kuwa mara baada ya kushinda uchaguzi huo atabadili katiba ili atawale milele.

Kwanini anataka kutawala milele? Kwa sababu pindi akitoka madarakani basi kuna kesi kibao zinamsubiri. Kwa hakika atakuwa rais mstaafu wa kwanza kuburuzwa mahakamani. Kwahiyo, (a) anafanya kila jitihada ashihde uchaguzi mkuu ujao (b) akishinda atabadili katiba ili abaki madarakani milele.

Nimalizie kwa kuwanong’oneza kuwa japo hali ni mbaya na inazidi kuwa mbaya, kuna dalili za matumaini kwa mbali. Mnajua kwanini safari yake ya China imeota mbawa? Ni kwa sababu angelogwa tu kuaondoka, basi asingerudi. Naam, kuna jithada kubwa sana ndani na nje ya chama na serikali kuhakikisha huyu bwana harudi Ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao. Na kwa mbali, kuna uwezekano wa jitihada hizo kufanikiwa.

Awali kulikuwa na hofu kuwa huenda jitihada hizo zisifanikiwe kwa sababu “Magufuli amekikumbatia kitengo,” lakini taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa appeal ya kiongozi huyo imeporomoka sana huko Kitengo na jeshini.

Tukutane Jumatatu.

Mtumishi wako Evarist Chahali