Teua, Tengua, Teua, Tengua ya Magufuli

Tatizo La Msingi Lipo Kwenye Mfumo Fyongo Wa Utawala wa Mtu Mmoja (One-Man Show) wa Jiwe

Awali niliwatumia “audio” ya salamu zangu mtumishi wako kwako kuhusu mabadiliko ya muundo wa kijarida hiki ambacho sasa ni “kimoja katika vitano” (5-in-1) kwa maana ya vijarida vitano kwa wiki

#BaruaYaChahali (kila Jumatatu)

#ChahaliNaTeknolojia (kila Jumatano)

#BaruaYaShushushu (kila Ijumaa)

#YaliyojiriWikiHii (kila Jumamosi)

#MtuHatari (Kila Jumapili)

Baada ya utangulizi huo, naomba niingie kwenye mada ya wiki hii ambayo inahusu mabadiliko ya mara kwa mara wenye safu ya uongozi wa serikali ya Magufuli. Naomba ieleweke mapema kuwa sina tatizo na “mabadiliko” alimradi yawe yanalenga kuleta ufanisi na tija.

Tatizo lipo kwenye ukweli kwamba licha ya “teua, tengu, teua, tengua,nk” ya mfululizo ya Magufuli kuweza kuwa na athari katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali (kila mteuliwa mpya huanza upya), kuna suala la gharama pia ambapo kwa mujibu wa taratibu za utumishi, mshahara uliokuwa ukiupata katika ngazi ya juu utaendelea kulipwa hata ukiwa katika wadhifa wa chini.

Lakini la muhimu zaidi sio hizo gharama maana sie “tupo vizuri na ndio maana tumeshanunua bombadia kadhaa,” ila suala linalonitatiza mtumishi wako ni kwa kuangalia “teua, tengua,teua, tengua,nk” hii kwa jicho la kiusalama.

Kwanza, kwa mujibu wa taratibu, kabla ya Rais kufanya uteuzi hupaswa kuwasilisha jina la mteuliwa mtarajiwa kwa Idara ya Usalama wa Taifa ili afanyiwe kitu kiitwacho “vetting” (yaani uchunguzi wa kiusalama kubaini endapo mhusika anafaa au hafai kwenye nafasi anayopendekezwa kuteuliwa).

Kwa mujibu wa taarifa nilizonazo, Magufuli amekuwa akipuuza utaratibu huu. Na pengine wa nia njema tu kwa sababu ya ubabaishaji wa kupitiliza huko Idara ya Usalama wa Taifa, kwa maana ya kwamba hata vetting zao sio za kuaminika.

Lakini kosa la Jiwe sio kwenye kupuuza utaratibu huo as such bali kupuuza maboresha ya mfumo wa vetting. Kwa sababu pasipo proper vetting, taifa sio tu litaendelea kuingia gharama zinazoweza kuepukika za “teua, tengua, teua, tengua, nk” bali pia kuna hatari kubwa kiusalama, kwani baadhi ya watu wanaotumbuliwa walikuwa katika nyadhifa ambazo zinawawezesha kufahamu masuala nyeti ya taifa letu, na wanaweza kuziweka hatarini taarifa hizo wanapokuwa nje ya nyadhifa zao.

Hapana, simaanishi kwamba kwa sababu A asitumbuliwe kwa vile tu yupo kwenye wadhifa unaomwezesha kujua taarifa nyeti licha ya utendaji kazi wake ni mbovu. Kinachohitajika hapo ni “kinga ni bora kuliko tiba.” Laiti proper vetting ikifanyika, itamsaidia Magufuli kupata timu ya wachapakazi ambao watapeleka Rais kutoona haja ya “teua, tengua, teua, tengua.”

Tukiweka kando huo mtazamo wa kiusalama, wanaomfahamu vema Jiwe wanasema kuwa tatizo lake kubwa lipo kwenye kufanya teuzi kwa upendeleo. Wengi wa anaowateua ni “watu wake” hususan kutoka Kanda ya Ziwa. Sasa, moja ya athari kubwa sana za teuzi za kujuana ni “jeuri” kwamba “hata nikilikoroga, hawezi kunichukulia hatua.” Na hata kama baadaye mhusika atachukuliwa hatua, basi huneda ni baada ya “kulikoroga beyond maelezo.”

Tukiangalia hii latest “teua, tengua, teua, tengua, nk” ya Jiwe, yayumkinika kuhisi kuwa hata huyo mteuliwa mpya nae anaweza kukuta kibarua chake kinaota nyasi, kwa sababu miongoni mwa mapungufu ya Jiwe ni kuwatupia lawama watendaji wake kwa maamuzi yake mabovu. Mfano hai ni ishu ya #Koroshow ambayo bila shaka imechangia kumuondoa huyo Waziri aliyetumbuliwa majuzi.

Serikali haiwezi kuendeshwa kama baba anavyoendesha familia yake kidikteta. Hapan. Serikali ni teamwork.Serikali inapaswa kuzingatia kanuni na taratibu na siokuendesha mambo kwa kukurupuka. Serikali haipaswi kuendeshwa kwa kukomoana au kupendeleana.

Kwahiy, tukiweka kando factors nyingine, “teua, tengua,teua, tengua,nk” ya Jiwe itendelea kutokea endapo hatoachana na aina ya uongozi wake wa mtu mmoja (one-man show). Ni muhimu kuwekeza kwenye mfumo wa uongozi badala ya kuongoza nchi kwa hisia, leo Jiwe akiwa na furaha anafanya hivi, akikasirika anafanya vile. Ikumbukwe kuwa nchi haipaswi kuendeshwa kwa majaribio.

Tukutane wiki ijayo.

Ndimi mtumishi wako

Evarist Chahali