Tamko la Lissu Kuwa Yeye na Lema Watarejea Tanzania Mwezi Machi Linamaanisha Masharti Aliyoipa Serikali Kuhusu Usalama Wake Yametimizwa?
Katika hotuba yake kwa taifa kuaga mwaka 2021 na kuukaribisha mwaka 2022, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, na mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Mheshimiwa Tundu Lissu, alieleza kuwa yeye aliyepo Ubelgiji kwa sasa, na kiongozi mwenzie wa chama hicho, Mheshimiwa Godbless Lema, aliyepo Canada, watarejea Tanzania mwezi Machi mwaka huu.


Hata hivyo, Desemba 8 mwaka jana, mwanasiasa huyo alinukuliwa na gazeti la Mwananchi akitanabaisha kuwa serikali inapaswa kumhakikishia usalama wake ili aweze kurudi nchini Tanzania. Alisisitiza serikali ikitoa kauli ya kuhakikisha usalama wake, yeye hatukuwa na sababu ya kuendelea kuishi Ubelgiji.
Je yawezekana serikali imetoa tamko la siri kwa Mheshimiwa Lissu kumhakikishia usalama wake hadi kufikia hatua ya kutangaza kuwa atarudi Tanzania mwezi Machi, pamoja na Mheshimiwa Lema?
Japo sina shaka na maelezo ya Mheshimiwa Lissu kuwa Kamati Kuu ya chama hicho imewataka yeye na Mheshimiwa Lema kurudi lakini napata shida kuelewa Kamati Kuu hiyo imewezaje kuhakikisha kuwa kurudi kwa viongozi hao wawili hapo mwezi Machi hakutoathiri usalama wao.
Nihitimishe kwa kutanabaisha kuwa sitarajii kama jibu la swali hilo liitapatikana, lakini natumaini litaamsha tafakuri kuhusu “siasa za hadharani” na “siasa za faraghani.”
Heri ya mwaka mpya
Tangazo: Kozi mbalimbali zilizokuwa zinatolewa na chuo changu cha mtandaoni cha AdelPhil Online Academy sasa zitakuwa zinapatikana katika ukurasa huu wa Barua ya Chahali. Karibuni sana 🙏