Tahadhari ya Ubalozi wa Marekani kuhusu tishio la ugaidi Dar: Huku Waziri wa Mambo ya Nje Dkt Tax akizionya balozi za nje "kutozua taharuki", taarifa zadai ISIS walifanya "ukaguzi" Dar hivi karibuni
Jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Stargormena Tax alizionya balozi za kigeni zilizopo Tanzania kufatia taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Marekani wiki iliyopita ikitahadharisha kuhusu uwezekano wa shambulio la kigaidi jijini Dar.
Taarifa kamili kuhusu onyo hilo la Waziri Tax ni hii hapa
Kwa kifupi, taarifa inasema kwamba serikali ya Tanzania inazikumbusha balozi za kigeni kuzingatia milango ya mawasiliano ya kidiplomasia kama ilivyobainishwa kwenye Mkataba wa Vienna kuhusu taarifa zinazoweza kuibua taharuki.
Wito huo ulitolewa na Waziri Tax alipokutana na wakuu wa balozi za nje zilizopo Tanzania na mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini humo, tukio lililojiri jana jijini Dodoma.
Dkt Tax alieleza bayana serikali kusikitishwa na tahadhari iliyotolea hivi karibuni kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi jijini Dar na maeneo mengine ya Tanzania.
Alieleza kuwa tahadhari hiyo ambayo ilirudiwa pia na baadhi ya balozi nyingine ilizua taharuki miongoni mwa Watanzania, raia wa kigeni nchini Tanzania na wasafiri wa shirika la ndege la KLM lililoahirisha baadhi ya safari kutokana na tahadhari hiyo.
Alisema kuwa serikali inatajia kuwa tukio kama hili halitojirudia na kuomba radhi kwa niaba ya serikali kutokana na usumbufu uliojitokeza kutokana na tahadhari hiyo.
Waziri Tax aliziagiza balozi za kigeni kutotoa tahadhari kama hiyo kwani ni kinyume na Mkataba wa Vienna unaoongoza shughuli za kidiplomasia.
Alieleza kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi ya amani, salama na imara huku ikifuatilia masuala ya usalama kitaifa na kimataifa.
Awali, shirika la ndege la KLM lilitoa taarifa ya ufafanuzi kufuatia malalamiko ya Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa baada ya shirika hilo kusitisha baadhi ya safari zake kutokana na ilichoeleza kuwa tishio la ugaidi.
Kwa kifupi, shirika hilo limeomba radhi kwa kutumia neno “civil unrest” linalomaanisha machafuko. Pia shirika hilo limeeleza kuwa taarifa za kiuslama ndizo zilizopelekea kuchua hatua husika. KLM wamesema hawawezi kueleza kwa undani zaidi kuhusu taarifa hizo.
Wakati hayo yakijiri, taarifa za kiintelijensia zimedai kuwa kikundi cha kigaidi cha Islamic State kilifanya “ukaguzi” (dry-runs) jijini Dar kati ya mwezi uliopita na mwezi huu.