Taarifa za Ujio wa Mama @SuluhuSamia Hapa Uingereza: Makada wa CCM Waanza Kushawishi Watu "Kuunga Mkono Jitihada,"Jasusi "Awachomolea."

Kuna taarifa kuwa Mama Samia Suluhu atazuru hapa Uingereza hivi karibuni. Yawezekana ziara hiyo ikahusisha kuhudhuria mkutano wa mazingira unaofahamika kama COP26 unaofanyika katika mji huu ninaoishi wa Glasgow, hapa Uskochi.

Lakini kama ilivyo kawaida ya wana-CCM huko nyumbani na hata huku Ughaibuni, ziara za kitaifa za viongozi wakuu hutekwa na kugeuzwa ziara za kichama.

Jana zilifanyika jitihada za awali za kunishawishi “niunge mkono jitihada” ambapo niliahidiwa kukutanishwa na Mama Samia. Nilitanabaisha kuwa hadi muda huu bado namuunga mkono Mama Samia, japo siridhishwi na handling yake ya kesi ya Mheshimiwa Freeman Mbowe.

Kingine nilichoeleza ni kwamba sihitaji kuwa mwana-CCM kumsapoti Mama Samia au kiongozi mwingine wa kitaifa. Kuwa mwananchi nisiye na chama alimradi naitakia mema nchi yangu kwatosha.

Lakini niwe mkweli. Hisia za kijasusi zilinieleza bayana kuwa mpango wote huo unaweza kuwa mtego tu wa kuwezesha hujuma dhidi yangu. Japo siamini kuwa Mama Samia anaweza kuridhia hujuma dhidi yangu, lakini ni muhimu kuchukua tahadhari.

Kingine nilichotanabaisha ni kwamba mie kama mzalendo sina tatizo kuwa na msaada kwa kiongozi au taifa kwa ujumla. Hata hivyo, iwe kwa matakwa yangu na sio kupangiwa au kushawishiwa. “Endapo huyo Mama au kiongozi mwingine atanihitaji, atalazimika kuwasiliana nami mwenyewe, kisha nifanye maamuzi baada ya thamini ya kina kuhusu usalama wangu,” nilimfahamisha “mjumbe” husika.

Niwasihi viongozi wa jumuiya za Watanzania hapa UK (sijui ziko ngapi) waache ku-politicise ziara za viongozi wa kitafa. I know Rais ni Mwenyekiti wa CCM lakini huo u-CCM wao hauondoi Utanzania wetu. I hope wahusika watafanyia kazi.