Taarifa Ya Kijasusi Kuhusu Vikao Vya CCM Wiki Hii

Ajenda Kuu Ya Vikao Hivyo Ndio Iliyopelekea Hati Ya Dharura Ya Muswada Wa Kukandamiza Haki Za Binadamu

Kabla ya kuingia kwenye mada ya wiki hii naomba kwa masikitiko makubwa kutanabaisha kuwa hili litakuwa toleo la mwisho la #BaruaYaChahali kwa wadau mlioamua kutokuwa wanachama.

Ningetamani sana kuwatumikia nyote lakini ni muhimu nijitendee haki mie mwenyewe pia, kwa kuwekeza nguvu zangu kuwatumia wale tu wenye nia ya dhati ya kutumikiwa nami.

Japo idadi ya waliojisajili uanachama ni ndogo - takriban watu 50 tu - kwangu naona hakuna tatizo kwani ni vema kuwatumikia japo watu 10 wenye uhitaji wa dhati kutumikiwa kuliko watu 1000 ambao hawana nia ya dhati.

Toleo lijalo la kijarida hiki litatoka Julai Mosi, siku ambayo vijarida vitano vinavyounda #BaruaYa Chahali yaani hiki unachosoma muda huu (kinachotoka kila Jumatatu), #ChahaliNaTeknolojia (Jumatano), #BaruaYa Shushushu (Ijumaa), #YaliyojiriWikiHii (Jumamosi) na #MtuHatari (Jumapili) vitaanza kutumwa kwa wanachama tu. Maelezo kuhusu uanachama huo ni haya pichani.

Kwa walio nje ya Tanzania, mnaweza kujiunga kwa KUBONYEZA HAPA.

Mada ya leo inahusu vikao vya CCM vitakavyofanyika wiki hii.

Kwa mujibu wa taarifa za kijasusi nilizonazo, ajenda kuu ya vikao hivyo ni kupitisha msimamo kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais John Magufuli ndio awe mgombea pekee kwenye nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani.

Lengo ni kuweka utaratibu rasmi utakaozuwia mwanachama yeyote yule kutaka kuchuana na Magufuli, ambaye ana hofu kubwa kuhusu hatma ya urais wake kutokana na mwenendo usioridhisha wa utawala wake.

Magufuli anafahamu bayana kuwa endapo atajitokeza mwana-CCM imara kuchuana nae, anaweza kabisa kutoswa, hasa kwa sababu amezungukwa na wanafiki wengi ikiwa ni pamoja na wale wanaomhadaa kuwa wanampenda ilhali wanamwombea kila baya.

Hofu kubwa ya Magufuli ipo kwa Membe, japo binafsi naona ni hofu hewa kwa sababu hakuna uwezekano wowote kwa Membe kuwa Rais. Never. Ever. Nilishaeleza kwa kina kwenye MAKALA HII.

Na nikaeleza kwa kina katika MAKALA HII jinsi akina Rostam “wanavyomzuga” Jiwe. Na so far mkakati huo unafanya kazi vema.

Kwa mujibu wa taarifa, baada ya vikao hivyo kumuidhinisha Magufuli kuwa mgombea pekee (haijafahamika kama uamuzi huo utatangazwa hadharani au utabaki kuwa “siri ya chama”), hatua itakayofuata ni mkakati wa mabadiliko ya katiba yanayolenga kumfanya Magufuli kuwa “Rais wa milele.”

Kwa mujibu wa taarifa, miongoni mwa wahusika muhimu wa mikakati hiyo ya kumfanya Magufuli kuwa mgombea pekee na hatimaye kubadili Katiba ni pamoja na Profesa Kabudi, ambaye taarifa zinadai kuwa tayari ana “kopi ya mabadiliko ya Katiba.” Taarifa zaidi zinadai “katiba hiyo mpya” ni “copya and paste” kutoka Rwanda, nchi ambayo ina maslahi makubwa katika urais wa Magufuli.

Mtu mwingine ambaye ni uthibitisho kwamba mkakati wa akina Rostam umefanikiwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Mzee Cornel Apson, ambaye kama wengi wenu mnavyofahamu, kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mwaka 2015 alikuwa kambi ya Lowassa.

Image result for magufuli apson

Kuibuka upya kwa Mzee Apson kunaweza pia kuwa kumechangiwa na ukweli kwamba uhusiano kati ya Jiwe na Mkurugenzi Mkuu wa sasa wa Idara ya Usalama wa Taifa, Mchungaji Modestus Kipilimba ni wa mashaka, hasa kwa sababu Kipilimba amefika hapo alipo kutokana na sapoti ya Membe. Wajuzi wa mambo wanadai kuwa Jiwe anahangaika jinsi ya kumtoa Kipilimba madarakani lakini inamuwia vigumu kwa sababu sio tu shushushu huyo alikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Jiwe mwaka 2015 lakini pia “amemuweka Jiwe mateka kwa njia za asili.”

Kwa uapnde mwingine, maamuzi ya vikao hivyo vya CCM yametengenezewa mazingira mazuri ya kutokumbana na upinzani mtaani kwa kutumia sheria kandamizi inayoharakishwa huko bungeni kwa kutumia hai ya dharura.

Wananchi wengi hawafahamu kuhusu muswada ya sheria husika, na japo taasisi za kiraia zimekuwa zikipiga kelele, kuna kila dalili kuwa muswada husika utapita na kuwa sheria, na hivyo kusafisha njia kwa safari ya Magufuli kubadili katiba na hatimaye kuwa Rais wa milele.

Jisikie huru kutoamini taarifa hizi, na lengo langu sio kumuaminisha mtu yeyote yule bali kuziripoti kama nilivyozipokea.

Moja ya athari za awali kabisa za muswada huo unaokimbizwa bungeni ni kudhibiti vikali mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na matumizi ya Whatsapp. Kinachosubiriwa na muswada kuwa sheria na si ajabu mkaanza kushuhudia athari zake as early as mwezi ujao.

Bad news ni kwamba kwa Watanzania wengi si suala la mabadiliko ya Katiba ili Jiwe atawale milele wala hilo la sheria kandamizi linalowanyima usingizi. Unfortunately, vipaumbele vya wengi wao vipi kwingineko, na ndio maana hata hizi jitihada tunazofanya baadhi yetu “kuwaamsha waliolala” hazina ufanisi wowote.

Kibaya zaidi, vyama vya upinzani ni kama vimeshakubali kuwa hali iliyopo na ijayo ndio stahili yao na ya Watanzania kwa ujumla. Hata kurudi kwa Lissu mwezi Septemba (kama kweli atarudi) hakutobadili chochote kwa sababu so far watesi wake wameshinda. Wameshinda kwa sababu licha ya serikali kupuuzi tukio la jaribio la kumuua mwanasiasa huyo, chama chake cha Chadema kipokipo tu, na hakijachukua hatua yoyote dhidi ya watesi wa Lissu na viongozi wengine wahanga wa siasa za chuki za Jiwe na mwanae Bashite.

Nimalizie kwa kuwatakia siku na wiki njema, na pia kuwashukuru nyote mliojumuika nami kwa muda mrefu wakati kijarida hiki kikiwa hakina uanachama. Na kunradhi kwa yeyote niliyewahi kumkwaza na maandiko yangu au aliyekwazwa na uamuzi wa kuwa na uanachama wa kijarida hiki.

Ndimi mtumishi wenu,

Evarist Chahali