Taarifa ya Familia ya Mbowe Kuhusu Kauli ya Bashite Kuwa Mtoto wa Mbowe Anaumwa Korona

TAARIFA YA FAMILIA YA FREEMAN AIKAELI MBOWE KWA UMMA WA WATANZANIA NA DUNIA.

KORONA NI JANGA KUBWA KULIKO VIONGOZI NA WATANZANIA WENGI TUNAVYODHANI:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, leo asubuhi ametangazia dunia kuwa mmoja wa Wanafamilia wangu (mtoto) amebainika kuwa na virusi vya Corona na pamoja na mambo mengine anamshukuru Mungu kwa janga hili kutokea kwa familia yangu.

Bila kujali Maadili na upotoshaji ulioambatana na taarifa hizo, ni kweli mwanangu Dudley amethibitika kupatikana na virusi vya Corona baada ya kupata homa za vipindi, kuumwa kichwa mfululizo na kukohoa kwa siku tano.

Mama yake, ambaye ni Daktari alipobaini hali hiyo alizitaarifu mamlaka za Serikali zinazoshughulikia Janga hili nazo zilimtaka kijana apelekwe Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam kwenye vipimo zaidi ambapo ilithibitika rasmi kuwa ana virusi vya Corona.

Aidha, timu ya Serikali imeendelea kutoa ushirikiano na ufuatiliaji wa karibu kwa familia yote ikiwemo ushauri nasaha kwa wanafamilia na marafiki wengine waliokutana na Dudley katika mikusanyiko mbalimbali ikiwemo kuweka wengine in Isolation au karantini.

Familia yangu inakiri kupokea ushirikiano wa kiwango kilichowezekana kutoka kwa Mamlaka husika za Serikali wakiongozwa na Waziri Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu wake, Mganga Mkuu wa Serikali na Wataalam wao wote nikimaanisha Madaktari, Wauguzi nk.

Hali ya Dudley sasa imeimarika. Homa zimekwisha. Kichwa kimepona. Bado anakohoa kiasi na yuko chini ya uangalizi maalum kwenye “isolation”.

Dudley hajasafiri nje ya nchi mwaka huu. Maambukizi haya kayapata ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Ugonjwa huu haupaswi kuwa siri japo kuna miiko inayoongoza utaji wa taarifa za wagonjwa. Tatizo ni kubwa kuliko tulivyojiandaa na tunavyojiandaa.

Wengi wameitafuta familia kutaka kujua ukweli na undani wa jambo hili. Pengine kupitia ushuhuda wangu, tutaweza kuokoa wengi katika nchi yetu. Hakika leo kila mmoja anastahili kujua janga hili liko mlangoni mwake!

Nimekiri kupata ushirikiano “kwa kiwango kilichowezekana”. Sina uhakika ni wangapi watapata “bahati” hiyo. Nimejifunza mengi. Nazungumza kwa mamlaka ya kuwa mhanga na shuhuda wa hali halisi tuliyo nayo. Tuna mlima mrefu wa kupanda. Hakika Serikali inahitaji msaada. Mlipuko hauko mbali. Tuelezane ukweli tusijechelewa.

Njia mojawapo muhimu ya kulishinda tatizo ni kulikubali na kulikabili kwa nguvu zote na kwa Umoja wetu.

Hatustahili kuchefuliwa na kejeli za Paul Makonda kipindi hiki. Tusiiachie serikali pekee. Tutajuta. Tusiilaumu tu, tuishauri nayo iwe tayari kuupokea ushauri na ishirikishe. Ni janga la Dunia na hakika tutaumizwa kuliko tunavyowaza.

Rai kwa Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli: Unda timu ya kukusaidia na ushirikishe wadau wengine nje ya Serikali yako. Yako mengi ya kufanya nje ya mikakati ya kitabibu inayosimamiwa na Waziri Mkuu na Waziri Ummy Mwalimu.

Katika maisha maandalizi hayajawahi kuwa hasara, bali hasara iliyo

majuto ni kutokujiandaa na kupuuza yanayofanywa na walioyapitia kama

Ilivyo nchi za wenzetu zilizoendelea na hata nahitaji zetu!

Wengi wako tayari kukusaidia. Chadema tuko tayari kukusaidia na kulisaidia Taifa. Siyo wakati wa kulumbana huu.

Freeman Aikaeli Mbowe

Mkuu wa Familia na Shuhuda wa Janga