Sophia Mjema: Baada ya kupata mwanamke wa kwanza kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama chao - Mama @SuluhuSamia huyo - CCM waandika historia nyingine kuwa na Mwenezi wa kwanza wa kike
Kwanza naomba nitanabaishe kuwa hii ni mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 7 kwa mie kuipongeza CCM. Naamini watu wengi wanaonifahamu wanaelewa bayana msimamo wangu kuhusu chama hicho.
Kwahiyo, kabla msomaji hujaanza kuhisi “Jasusi kanunuliwa” au “Jasusi anataka u-DC” (japo u-DC sio dhambi), ieleweke kuwa Jasusi ni mzalendo anayekosoa panapostahili na kupongeza panapostahili. Jasusi hana chama isipokuwa mapenzi yake kwa Tanzania. Na hiyo inamsaidia kuangalia mambo bila kutumia miwani ya mbao ya ukada inayopofusha Watanzania wengi.
Ni muhimu kutoacha kuzungumzia matukio yanayoandika historia mpya. Tukiacha kuzungumzia au kuweka kumbukumbu, vizazi vijavyo vitapata shida sana kuelewa mambo mbalimbali huko mbeleni.
Na moja ya mambo ambayo Jasusi amejifunza katika maisha yake huku ughaibuni ni jinsi wenzetu wanavyojibidiisha kuhusu vizazi vijavyo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu, Bi Sophia Mjema aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu Mwenezi wa CCM, anakuwa mwanamke wa kwanza kabisa kushika wadhifa huo.
Kwanza Jasusi alilazimika kuuliza kuhusu rekodi hiyo

Na bahati nzuri mdau mmoja akasaidia kupata jawabu

Japo kwa moyo mgumu, lakini Jasusi analazimika kuipongeza CCM kwa kuweka historia nyingine. Awali chama hicho tawala kiliweka historia kwa kupata mwenyekiti wake wa taifa wa kwanza mwanamke, Rais Samia Suluhu, na sasa kimeweka rekodi nyingine kwa Bi Mjema.
Japo Jasusi hamfahamu vizuri Bi Mjema, lakini mambo matatu yanamfanya Jasusi adhani kuwa Bi Mjema nae anaweza kuandika historia kwa utendaji kazi bora pengine kuliko watangulizi wake wote.
Jambo la kwanza ni hilo la yeye kama mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo ndani ya chama hicho kikongwe. Kama ambavyo Jasusi anaamini uanamke wa Rais Samia ambao ni historia kwa chama chake na nchi yetu unavyoweza kuwa chachu ya yeye kuacha alama katika uongozi wake, ndivyo Bi Mjema nae anavyoweza kufanya “maajabu”.
Pili, Bi Mjema amekuwa kwenye uongozi serikalini kwa muda mrefu. Hiyo itamsaidia kujenga uwiano kati ya wajibu wa kiitikadi kwa chama na kusimamia utendaji wa serikali (kwa vile chama hicho tawala ndio kilichounda serikali iliyopo madarakani).
Tatu, mtangulizi wa Bi Mjema, Bwana Shaka, alikuwa Mzanzibari kama Mama Samia. Japo vikao ndio viliamua kumtoa Shaka na badala yake kumteua Bi Mjema, huhitaji uelewa mkubwa wa siasa kubaini kuwa both - kuondolewa Shaka na kuteuliwa Bi Mjema - kuna baraka za Mama Samia. Sasa ukiaminiwa na kiongozi wako inamaanisha una mtaji muhimu katika utekelezaji wa majukumu yako.
Jasusi anachukua nafasi hii kumpongeza Bi Mjema kwa matumaini kuwa ataweza kukisaidia chama hicho tawala kiondoke katika nafasi yake ya sasa ambapo kinabebeshwa lawama zote kuhusiana na changamoto zinazoikabili Tanzania, hususan rushwa na ufisadi, na kukirejesha chama hicho katika asili yake ya kuwatumikia wanyonge.
Kadhalika, Jasusi anatarajia kuwa Bi Mjema ataepuka siasa za mipasho na badala yake atajikita katika kuhakikisha kuwa chama hicho kinawatumikia Watanzania kwa uadilifu mkubwa.
MENGINEYO
I think CCM now need concrete message. Instead of propaganda and the chawa strategy. Tanzanians are not stupid or ignorant of what is going on. I wonder what Sophia’s strategy will be about educating the people of Tanzanians. All in all we have a long way to go. In my opinion this Chawa phenomenon is silly and ignorant. I can’t stand young people who have turned to praise teams. I don’t know why ccm thinks it is a good thing.