Siasa Kidogo, Kisha Nikupe "Maujanja"

Kwanza naomba radhi kwa kuchelewa kuwatumia #BaruaYaChahali. Hiyo ikitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Pili naomba kutumia fursa hii kuwatakia swaum njema nyote mnaoendelea na mfungo katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.

Twende kwenye mada. Wiki hii kijarida hiki kina sehemu mbili. Kwanza ni siasa kidogo, kisha sehemu ya pili ni darasa fupi mbinu flani muhimu kwako.

Kwenye siasa ni habari njema ya kupatikana kwa kada maarufu wa Chadema, Mdude Nyagali almaaruf “Mdude Chadema.”

Ilikuwa faraja kubwa kwa baadhi yetu tuliopiga kelele kwa nguvu zote kumsisitiza Magufuli amuachie mwanaharakati huyo akiwa hai.

Kuna mengi ya kujifunza kutoka katika tukio hili la Mdude lakini matatu ya msingi ni, kwanza, kutekwa kwa Mdude ni uthibitisho mwingine wa udikteta wa Magufuli.

Pili, kelele dhidi ya maovu zinaweza kupelekea mabadiliko chanya kama ambavyo kelele za #BringBackMdudeAlive zilivyochangia kurejeshwa hai kwa mwanaharakati huyo.

Tatu, pamoja na Mdude kurejea, bado kuna wingu zito lililotanda kuhusu “kupotea” kwa kada wa Chadema Ben Saanane, mwanahabari Azory Gwanda na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye.

Sambamba na “kupotea” huko, bado kuna wingu zito kuhusu #WatuWasiojulikana

Sio tu kuwa bado #WatuWasiojulikana ni tishio kubwa bali pia uhusika wao kwenye matukio mbalimbali kama vile jaribio la kumuua Tundu Lissu, kutekwa kwa mfanyabiashara Mo Dewji na msanii Roma Mkatoliki na wenzie, kuuawa kwa Diwani Luena wa Chadema na Katibu wa chama hicho Kata ya Hananasif Daniel, na wengineo kadhaa.

Kwa bahati mbaya - au makusudi - tayari tukio la kutekwa kwa Mdude limeshasahaulika, kama ambavyo matukio mengine yaliyojiri huko nyuma yalivyosahaulika.

Kama kuna kitu kimoja “aliyeiroga Tanzania” alihakikisha hakiponi ni huo USAHAULIFU. Na niwe mkweli, sina hakika kama ni usahaulifu kweli au ni uzembe tu.

Na pengine cha kuvunja moyo zaidi ni ukweli kwamba kama katika kadhia ya mgao wa umeme ambayo imedumu kwa takriban miaka, 20 sasa, watu huitukana Tanesco kila aina ya matusi na kuimwagia kila aina ya laana, only for watu hao kusahau kabisa kuhusu kadhia hiyo mara tu umeme unaporudi, kwanini basi matukio ya “mara moja moja” kama hilo la Mdude, yasisahaulike kirahisi tu?

Enewei, tuachane na siasa kwa sasa. Twende kwenye sehemu ya pili ya toleo hili ambayo inahusu “maujanja flani.”

Kabla ya kukupatia “maujanja” husika, naomba kukiri kuwa moja ya mambo yanayonipa wakati mgumu sana ni kusimama kwangu kutoa mada mbalimbali huko Instagram, hatua iliyotokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu.

Ninajiskia kama ninawanyima watu mbalimbali vitu mbalimbali ambavyo huenda vingekuwa na msaada kwao.

Hata hivyo, ni matarajio yangu kuwa pindi mazingira yatakapokaa vema, nitaendelea kuwaletea mada hizo, ambazo zilijikitika kwenye “jinsi ya kuwa mtu bora/jinsi ya kuboresha ubora wa mtu husika.”

“Maujanja” ninayokupatia leo ni ya kukusaidia kukumbuka vitu. Tunaishi dunia “ya mwendokasi” ambapo sio tu vitu vinatokea na kupotea haraka bali pia vinatokea kwa wingi kiasi kwamba inaweza kukuwia vigumu kukumbuka vitu muhimu kwako.

Kuna njia (ndo hayo naita “maujanja”) kadhaa kukusaidia kukumbuka vitu kirahisi. Kwa leo tugusie njia tano muhimu.

Ya kwanza ni kurudiarudia kitu husika.

Uzoefu unaonyesha kwamba kukirudiarudia kitu unachotaka kukikumbuka husaidia kukikumbuka.

Ya pili ni kusoma.

Kwa bahati mbaya, kusoma ni kama adhabu kwa Watanzania wengi. Kuna msemo kwamba ukitaka kuficha kitu Mtanzania basi kiweke kwenye maandishi. Hata hivyo, nadhani unafahamu kuwa kama kuna kitu unahitaji kukikumbuka baadaye, ukikiandika na kukisoma baadaye kitarejea kwenye kumbukumbu zako kirahisi.

Ya tatu ni kufundisha.

Najua si kila mtu ana uwezo wa kufundisha, lakini sie ambao tumekuwa tukijihusisha na ufundishaji tunafahamu kuwa vitu tunavyofundisha wengine hukaa kichwani kwa muda mrefu na huwa rahisi kukikumbuka.

Ya nne ni kujadili.

Vitu tunavyojadili na wenzetu hukaa nasi muda mrefu na pia huwa rahisi kuvikumbuka. Kwa mfano kama ulijadiliana nami kuhusu siasa, ukikutana nami siku nyingine kuna uwezekano mkubwa kukumbuka kuhusu tulichojadiliana mara ya mwisho tulipokutana.

Ya tano na mwisho (kwa leo) ni kufanya mdahalo.

Mdahalo ni kama hiyo mbinu ya nne ya kujadili ila tofauti hapa ni ile hali ya kama “mashindano ya hoja.”

Tukutane wiki ijayo.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali