Sehemu ya Kwanza ya Mfululizo wa Makala Kuhusu Mmomonyoko wa Uzalendo Tanzania (Nilituma kwa Gazeti la Raia Mwema Lakini Haikuchapishwa)

MAKALA YA RAIA MWEMA

Evarist Chahali

Nianze makala hii kwa kuwataka radhi wasomaji kutokana na kuadimika kidogo. Hali hiyo ilisababishwa na sababu zilizo nje ya uwezo wangu.

Moja ya changamoto za uandishi wa makala kwenye gazeti kubwa kama hili la Raia Mwema ni ukweli kwamba matarajio ya wasomaji yapo juu sana. Kwa mantiki hiyo, mimi kama mwana-makala (columnist) ninakuwa na wajibu mkubwa sio kwa gazeti yu bali pia kwenye wasomaji, wajibu wa kuhakikisha kuwa kila makala inakidhi matarajio yenu.

Baada ya utangulizi huo, nielekee kwenye mada ya wiki hii inayohusu tatizo linalozidi kukua la kudidimia kwa uzalendo. Pengine sio rahisi sana “kwa vijana waliozaliwa miaka ya hivi karibuni” kubaini tatizo hili kwa sababu kuna ugumu wa kukielewa kitu ambacho hujawahi kushuhudia mbadala wake.

Kwa mfano, ni vigumu kutambua athari za kutokuwa na uelewa wa usalama wa mtandaoni endapo mhusika hajawahi kuwa mhanga wa uhalifu wa mtandaoni.

Kadhalika, ni vigumu kutambua athari za ukosefu wa amani endapo watu hawajawahi kuwa wahanga wa ukosefu wa amani. Japo vyombo vya habari vinaweza kuonyesha, kwa mfano yanayojiri huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kaskazini kwa Msumbiji, au maeneo mbalimbali ya Nigeria, kutaja sehemu chache ambazo zimegubikwa na janga la ugaidi, ukweli unabaki kuwa kinachoonekana kinabaki kama simulizi tu.

Lakini sio kwenye “vitu vibaya” tu, bali hata kwenye jambo kama ladha ya tunda. Kwa mfano, mtu akikuuliza tofauti ya ladha ya chungwa na nanasi, itakuwa vigumu kueleza kwa ufasaha, na njia nyepesi ni kumpatia mhusika kipande cha chungwa na cha nanasi aweze kuona tofauti ya ladha yeye mwenyewe.

Na ndivyo ilivyo kwenye suala la uzalendo. Ni vigumu kumueleza mtu jinsi uzalendo ulivyoshuka, au unavyozidi kudidimia, katika Tanzania yetu endapo mtu husika hajawahi kushuhudia nchi yetu iliposheheni uzalendo.

Chama tawala CCM hakiwezi kukwepa lawama katika tatizo hili la kushuka kwa uzalendo. Moja ya sababu muhimu zilizokiwezesha chama hicho kuwa chachu ya uzalendo sambamba na kuhamasisha uzalendo miongoni mwa Watanzania, ni itikadi ya kueleweka.

Itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea, sio tu ilikuwa na dira bali pia ilitekelezeka kwa vitendo kupitia sera mbalimbali. Kwa mfano, pamoja na mambo mengine, sera ya vijiji vya ujamaa ilijumuisha wanavijiji kushirikiana kwenye kilimo katika mashamba ya ushirika.

Ushirika huu ulijenga umoja na mshikamano miongoni mwa wanavijiji, na hatua kwa hatua, mshikamano huo ulivuka ngazi za kata, tarafa, wilaya, mikoa hadi taifa.

Viongozi wa zaman hizo, wakiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hawakuhubiri tu kuhusu Ujamaa na Kujitegemea bali walishiriki kwa vitendo. Mara kwa mara viongozi sio tu waliitembelea mashamba ya ushirika vijijini bali pia walishiriki katika shughuli za kilimo.

Zama hizo ndizo zilizozaa neno NDUGU. Kwamba Watanzania ni ndugu licha ya tofauti za makabila, dini, na kadhalika. Tofauti zilizokuwepo zilijenga kiu ya kuelewana badala ya kuwa sababu ya kufarakana. Kwa mfano, sie Wandamba tulitamani kuzielewa mila na tamaduni za wenzetu Wapemba. Wakurya waliona kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa wenzao Wachagga, kama ambavyo Waha na Wamatumbi walivyojibidiisha “kufahamiana.”

Kwa sababu wanazojua “wahusika,” itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea ilitelekezwa na badala yake kukaibuka ubabaishaji ulioacha ombwe katika sekta mbalimbali za maisha ya Watanzania. Kwenye uchumi, watawala wamekuwa wakihubiri kuwa Tanzania bado ni nchi ya kijamaa lakini ukweli upo tofauti. Lakini pia hata kama “ujamaa wa sasa” unaruhusu kinachoitwa “soko huria,” ukweli mchungu ni kwamba kwa kiasi kikubwa rushwa na ufisadi ndio vilivyogeuka kuwa mbadala ya uchumi wa kijamaa.

Kwenye jamii nako changamoto ni lukuki. Kwa upande mmoja “usasa” unataka jamii kuachana na mila na desturi zao ili “ziende na wakati.” Kwa upande mwingine, “kwenda na wakati” kunazidi kumomonyoa maadili yaliyowezesha mshikamano dhabiti katika jamii.

Nihitimishe makala hii endelevu kwa kutanabaisha kuwa kilichonisukuma kutupia jicho janga la kudidimia kwa maadili katika Tanzania yetu ni matishio ya ugaidi wa kimataifa. Matishio hayo yanachangiwa na sababu kuu mbili.

Ya kwanza ni hali ilivyo nchini Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ya pili ni kilichojiri nchini Aghanistan ambapo kundi la kigaidi la Taliban lilifanikiwa kuindoa serikali halali madarakani na sasa kundi hilo limeunda serikali rasmi. Tukio hilo linatarajiwa kuyahamasisha makundi mengine makubwa ya kigaidi kama vile ISIS, Al-Qaeda, Al-Shabaab, na kadhalika.

Kama nilivyotanabaisha awali, makala hii inayohusu kudidimia kwa uzalendo nchini Tanzania ni endelevu. Sehemu ijayo itaangalia jinsi kudidimia kwa uzalendo kunavyoiweka nchi yetu hatarini (vulnerable) kuhusiana na matishio hayo ya ugaidi.

Baruapepe: evarist@chahali.com

Twitter: https://twitter.com/chahali