Sababu Iliyopelekea Mabendera Lugola Kutimuliwa na Jiwe

Yaleyale Ya "Ushirika Wa Wachawi Haudumu."

Image

Moja ya makosa ya kudumu ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete ni mawili. La kwanza ni jinsi alivyowezesha nafasi ya urais kuwa RAHISI. Kwamba every Tom, Dick and Harry could actually become a president of the United Republic of Tanzania.

Na kuna dhana kwamba Kikwete alijibdiisha sana kutafuta mrithi ambaye atasababisha akili za Watanzania zielekezwe kwa mtu huyo badala ya kukasirishwa na utawala wake wa kihalifu kati ya mwaka 2005 hadi 2015.

Na kwa hakika amefanikiwa. Maana leo hii kuna mamilioni ya Watanzania wanaotamani Jk awe rais badala ya Jiwe. Leo hii Jk anaonekana malaika mbele ya “shetani” Jiwe.

Lakini ukweli mwepesi ni kwamba jinsi Jk alivyoikongoroa Tanzania yetu katika miaka 10 ya utawala wake wa kifisadi ndio ulivyojengeka msingi wa utawala ambao ungeweza kabisa kuwaburuza Watanzania kwa kisingizia cha kusafisha madudu ya Jk. Na yalikuwa mengi kupindukia.

Binafsi ninaumia sana ninapomuona Jk anazurura huku nje akiwa “mtu muhimu kimataifa” ilhali ana mchango mkubwa kuifikisha Tanzania ilipo leo. Ieleweke kuwa bila Jk tusingekuwa na huyu dikteta ambaye nae nchi imemshinda mapema tu na silaha pekee aliyobaki nayo ni ubabe, vitisho, ukatili na kila baya unaloweza kufikiria.

Baada ya utangulizi huo ambao naomba kukiri nimeuandika nikiwa na hasira kali, tuelekee kwenye maigizo yaliyojiri jana ambapo Waziri “Mabendera” Kangi Lugola alifutwa kazi na Jiwe.

Kama ilivyo kawaida kwa wazembe wengi wa kufikiri, taarifa hizo zilipokelewa kwa shangwe na baadhi wakiingia kwenye mtego wa kuamini kuwa Jiwe anachukia ufisadi kwa dhati.

Ukweli mchungu ni kwamba Mabendera hakufukuzwa kwa sababu ya ufisadi wa fedha za umma au matumizi ambayo hayakuidhinishwa na bunge. Tuanze na hilo la pili. Katika historia ya Tanzania hakujawahi kutokea mtumishi wa serikali, achilia mbali Rais, ambaye hana heshima kwa Katiba na taasisi za kikatiba, kama Jiwe. Huyu Bwana analiona Bunge kama takataka tu. Na kuna wapuuzi wengi tu huko Bungeni wanaowezesha hilo: mfano hai, majuzi imetangazwa kuwa kutajengwa hospitali ya kanda ya Ziwa huko Chato, akatokea mzembe mmoja na kupongeza suala hilo badala ya kukemea ubaguzi wa waziwazi wa Jiwe anayetaka kila kitu kiende Chato.

Ungetaraji Bunge lihoji nani aliyepitisha matumizi ya ujenzi wa hospitali hiyo ambao tayari umeshaanza, na uthibitisho ni huu pichani

Image

Jiwe anatumia fedha za umma kana kwamba zinatoka mfukoni mwake. Actually not, maana mtu anayetumia fedha kutoka mfukoni mwake anakuwa makini.

Ni “siri ya wazi” kwamba ununuzi wa bombadia umekuwa ukifanyika bila kuzingatia ridhaa ya Bunge. Na pale bunge linaporidhia matumizi, si Jiwe wala “bwana fedha mkuu wa serikali,” mpwawe Doto anayeona umuhimu wa kuzingatia kanuni za matumizi ya fedha za umma.

Kuna taarifa za kuaminika kuwa ulaji na ufisadi unaoendelea kwenye Awamu ya Tano ni zaidi ya maradufu ya miaka 10 ya ufisadi wa utawala wa JK. Tofauti kati ya zama za Jk na sasa ni kwamba media zilikuwa na uhuru wa kuripoti na Bunge lilikuwa na akili japo kidogo kushupalia matumizi mabaya ya fedha za umma. Lakini huyu dikteta amebana uhuru wa vyombo vya habari na Watanzania hawajui kuhusu mengi yanayoendelea “nyuma ya pazia.”

Lakini masuala mengine hayahitaji kuambiwa na media. Kwamfano, kwanini Watanzania wamekalia kimya suala la bombadia - mradi unaoligharimu Taifa matrilioni ya shilingi lakini ambao ufanisi wake haujaonekana hata chembe.

Muda huu naandika makala hii, kuna taarifa kuwa bombadia kadhaa zipo chali, hazifanyi kazi. Na haihitaji uelewa wa usafiri wa anga kujiuliza “hivi hizo ndege 11 zilizokwishanunuliwa hadi sasa zinafanya safari kwenda wapi?”

Turejee kwenye kutimuliwa kwa Mabendera. Taarifa za uhakika zinaeleza kwamba sababu iliyopelekea afutwe kazi ni “kuingilia dili la Jiwe.” Kwamba hiyo fedha inayodaiwa kutafunwa, pamoja na tenda husika, ilikuwa ni dili ya Jiwe mwenyewe.

Tatizo la Mabendera ni kujisahau kwamba aliwekwa hapo - licha ya tuhuma lukuki za ufisadi zilizokuwa zikimkabili kabla na baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo - kufanikisha upigaji na sio kuwapunja waliomkabidhi jukumu hilo.

Hebu jiulize, nchi masikini kama Romania ina nini hasa cha kuiuzia Tanzania, endapo tutaamini maelezo ya Jiwe kuhusu tenda iliyopelekea Mabendera na Mkuu wa Zimamoto kutimuliwa?

Na kama kweli kulikuwa na ufisadi unaoihusisha Wizara na Idara ya Zimamoto, kwanini Katibu Mkuu “amezawadiwa” ubalozi? Kumfunga mdomo?

Yaani kama mazingaombwe flani, only that mazingaombwe hayo ni vitu halisi vinavyohusisha kutafunwa kwa pesa yako ya ngama ya wewe mlalawima.

Kwa bahati mbaya - au makusudi - suala hili ndio limekwisha kimyakimya. Hakutokuwa na jitihada za kubaini ukweli. Na wakati akina Eric Kabendera na Tito Magoti wanateseka huko jela kwa tuhuma feki za “utakatishaji fedha,” si Jiwe, mpwawe Doto au Mabendera atakayewajibishwa kwa ujambazi husika ambao hata kiwango chenyewe hakieleweki vizuri.

Sina hakika mwisho wa haya utakuwaje ila nilicho na hakika nacho ni kwamba wanyonge mtaendelea kuadhibiwa, japomna fursa adimu hapo Oktoba kusema HAPANA. Je mtaweza? You know better than I do.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali