Rostam vs Membe, Na Jinsi Jiwe Anavyojikaanga Kwa Mafuta Yake Mwenyewe

Jicho La Kishushushu Kuhusu Yanayojiri Chini Ya Kapeti la Siasa za Urais 2020

Kwanza, naomba samahani kwa kuchelewa kukuletea toleo la wiki hii la #BaruaYaChahali. Natumaini uliipokea kunradhi yangu niliyokutumia juzi.

Mada ya wiki hii ni siasa, lakini ni fupi tu. Inalenga kukusaidia kuelewa "yanayojiri nyuma ya pazia" kwenye duru za siasa za Tanzania.

Natumaini kuwa ulimsikia mfanyabiashara tajiri mkubwa, Rostam Aziz, "swahiba" mpya wa Magufuli, akimuwashia moto mmoja wa wana-CCM wenye majina makubwa, Bernard Membe.

Katika clip ya video iliyosambaa vya kutosha mtandaoni, Rostam alisikika akimtaka Membe atulie na kumuacha Magufuli awe mgombea pekee ya urais kwa tiketi ya CCM hapo mwakani.

Membe nae akamjibu kwa njia hiyohiyo ya clip ya video akimtaka Rostam, ambaye Membe alidai kuwa ni mchumi, atumie taaluma hiyo kuzingumzia uchumi, "biashara zinazofungwa," na masuala "muhimu kama hayo," badala ya kuongelea watu.


Membe alimwambia Rostam kuwa wao wote "wamekatwa mkia" na kumtaka mfanyabiashara huyo kutojifanya "Mkristo zaidi wa Warumi."

Mie mtumishi wako, niliziangalia video zote mbili kwa jicho la kishushushu, na tafsiri yake ni nyepesi tu: huo ulikuwa mchezo wa kuigiza ambao mlengwa ni Jiwe, Magufuli.


Rostam hadi muda huu amefanikiwa mno kumlaghai Magufuli kuwa "yupo upande wake," na ndio maana "ushauri wake kuhusu Voda ulitekelezwa" bila kujali athari zake kwa taifa.

Kadhalika, Rostam amepiga hatua kubwa katika kujitengenezea nafasi kama "kingmaker" wa siasa za uchaguzi mkuu ujao baada ya "kumrejesha kundini" swahiba yake wa muda mrefu, Edward Lowassa.

Kinachofanyika ni jitihada za kumkaanga Magufuli kwa mafuta yake mwenyewe.

Rostam ni mhanga wa siasa za Magufuli - kama ilivyo kwa Membe, Lowassa na hata Jk. Ikumbukwe kuwa Rostam, Lowassa na Kikwete walikuwa kwenye “utatu usio mtakatifu” ambao ulipigana kufa na kupona kati ya mwaka 1995 hadi 2005 na kufanikiwa kumwingiza Jk madarakani huku Lowassa akipewa uwaziri mkuu. Kwa pamoja, watu hao watatu waliunda genge la kihistoria la kisiasa lililofahamika kama MTANDAO, genge lililojumuisha watu kutoka kila kada, from Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa to Maaskofu/Mashehe, from wauza madawa ya kulevya to maafisa waandamizi wa JWTZ. Mtandao ulijumuisha kila kada. Nina nyaraka kadhaa kuhusu genge hilo, na pindi nafasi huko mbeleni ikiruhusu nitaandika kwa kirefu.

Jk alikuwa yupoyupo tu, lakini turufu yake ilikuwa ni haiba yake. Na pia alikuwa na kiu ya kuwa rais. Lowassa alikuwa ndiye hasa “akili ya Jk,” maana alikuwa mwanasiasa mwenye ushawishi kiitikadi na kifedha. Rostam alikuwa “bwana fedha.” Naamini wewe msomaji unaelewa vema yaliyojiri baada ya jitihada zao kuingia Ikulu kufanikiwa.

Kwa upande mwingine, Membe alikuwa miongoni mwa watu muhimu kwa mtandao huo hasa kutokana na background yake huko Idara ya Usalama wa Taifa. Ndio maana baada ya Jk kuingia Ikulu, akamteua Membe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, wadhifa uliomfanya kuzurura na Jk kwenye kila “safari za uvumbuzi za Vasco da Gama.”

Ofkoz baadaye Jk na Lowassa walikorogana, kwa sababu “ushirika wa wachawi haudumu,” na Jk kuanza kumwandaa Membe kuwa mrithi wake, kimsingi watu hao wanne - Membe, Lowassa, Jk na Rostam waliendelea kuwa walewale wa Mtandao. Na japo Jk alifanya jitihada kubwa kumkwamisha Lowassa kuingia Ikulu kwa kuhofia kulipiziwa kisasi na Lowassa, jitihada zake za kutaka Membe awe mrithi wake hazikuzaa matunda, hasa kutokana na uzembe wa Membe (licha ya kupewa sapoti kubwa na Jk aliishia kutobebeka na akaishia kwenye tano bora tu).

Siasa za Magufuli - ukanda, ukabila, visasi, ubabe, chuki dhidi ya wafanyabishara kwa kisingizio cha vita dhidi ya ufisadi, kuwapuuza akina JK na makada wengine wa CCM - zilipelekea kujenga kile Waingereza wanasema “enemy of my enemy is my friend” (adui wa adui yangu ni rafiki yangu). Magufuli ni bad news kwa Jk. Bad news kwa Lowassa. Bad news kwa Membe. Bad news kwa Rostam. Bad news kwa kundi zima la Mtandao ambalo hadi leo bado lipo hai japo wahusika wengi kila mmoja yupo bize kuhangaikia “survival” yake.

Kuna msemo mmoja wa Waingereza unaotafsirika kama “ushirika kwenye chuki ni mwanzo wa urafiki muhimu.” Kwa mantiki hiyo, licha ya takriban kila mwana-Mtandao kuwa na maslahi yake binafsi, takriban wote wana chuki kali dhidi ya Magufuli. Na chuki “ushirika huo wa chuki” unawajengea “urafiki muhimu.”

Kwa kutumia utajiri wake mkubwa, sambamba na kuahidi kuwa “mshirika muhimu kwenye ujenzi wa Tanzania ya Viwanda ya Magufuli,” na ahadi ya kuchangia kampeni za Magufuli mwaka 2020, Rostam alifanikiwa kumshawishi Magufuli amuamini kuwa mshirika muhimu.

Rostam kama nimfanyabiashara mjanja, alibaini mapema kuwa njia nzuri nzuri ya kukabiliana na Jiwe ni kujenga urafiki nae. And it worked like magic, katika muda mfupi tu, Rostam ametokea kuwa mmoja wa watu muhimu kwa Jiwe na taratibu anajijengea nafasi kama "January Makamba au Kinana wa mwaka 2020" (yaani sawa watu waliompigania mno Magufuli mwaka 2020)

Rostam anamzuga Jiwe kwa kumuwakia Membe ili Jiwe aendelee kuamini kuwa tishio kwake mwakani huko CCM ni Membe ilhali yeye Rostam, Lowassa, Jk, Mzee Apson, nk wanamsafishia njia "mgombea wao" ambaye Jiwe atakapokuja kumfahamu (mgombe huyo) itakuwa tayari too late kwake kuzuwia lolote.

Lengo ni kumng’oa Jiwe kwa gharama yoyote ile. Na kama kila kitu kitakwenda kama kinavyokwenda muda huu, Jiwe ataishia kuwa Rais wa muhula mmoja.

Je Rostam na genge lake wanataka kumuondoa Jiwe kwa maslahi ya wewe mlalawima? Je Jiwe no bora kuliko genge hilo la kifisadi ambalo wenye kumbukumbu nzuri wanajua liliyofanya 2005 - 2010? Majibu ya maswali hayo unayo wewe mwana wa nchi.

Nakutakia siku na wiki njema. Tukutane tena wiki ijayo.

Ndimi mtumishi wako

Evarist Chahali