Ripoti ya kiintelijensia kuhusu kifo cha Membe
Utangulizi
Jana Mei 12, 2023 ilitangazwa kwamba aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe, amefariki dunia. Licha ya kushika wadhifa huo wa waziri mwandamizi katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete iliyodumu tangu 2005 hadi 2015, Membe pia alikuwa kada mwandamizi katika chama tawala CCM.
Ripoti hii ya kiintelijensia inaeleza wasifu mfupi wa Membe kabla ya kujikita kwenye sababu ya kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe.
Jasusi Membe
Moja ya mambo yaliyompa umaarufu mkubwa Membe ni “siri ya wazi” kwamba aliwahi kuwa Afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, na hiyo ilipelekea mwanasiasa huyo kufahamika pia kwa jina la utani la “Jasusi Membe”.
Membe mgombea urais
Baada ya Kikwete kumaliza muda wake mwaka 2015, na kwa vile swahiba wake wa zamani Edward Lowassa alikuwa ameshahama CCM na kujiunga na Chadema ambako alitangazwa kuwa mgombea urais, chaguo la Kikwete kupata mrithi wake lilikuwa kwa Membe.
Na haikuwa Kikwete pekee bali familia nzima ya Kikwete ilikuwa inamuunga mkono Membe. Hata hivyo, Membe aliboronga katika kinyanganyiro cha CCM kumpata mrithi wa Kikwete, na akaishia kwenye “tano bora”, na hatimaye mwanasiasa aliyekuwa hana umaarufu mkubwa, marehemu John Magufuli akaibuka kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Membe vs Magufuli
Mara baada ya Magufuli kuingia madarakani, ambapo aliweka wazi kuwa hatofanya safari za nje ya nchi, Membe alijitokeza hadharani kudai kuwa itamlazimu Magufuli asafiri kwani Tanzania sio kisiwa. Kauli hiyo iliyolaaniwa vikali na wafuasi wa Magufuli ilikuwa mwanzo tu wa uhasama mrefu kati ya wana-CCM hao.
Miaka kadhaa baadaye, Membe alionyesha dhamira ya kujaribu tena kuwania urais, lakini safari hii akikabiliwa na kizingiti cha utamaduni wa CCM kwamba rais anayemaliza muhula wa kwanza ndio mgombea pekee kwenye kinyang’anyiro kinachofuata cha urais. Kwa kutaka kuwania urais, ilimaanisha kuwa Membe angechuana na Magufuli. Jitihada za mwanasiasa huyo ziliishia kwa yeye kufukuzwa uanachama wa CCM kwa sababu zilizotafsiriwa kuwa “ukaidi wa kutaka kuchuana na Magufuli.”
Membe mgombea ACT-Wazalendo
Baada ya kufukuzwa uanachama CCM, Membe alijiunga na ACT-Wazalendo, ambako chama hicho kilimtagaza kuwa mgombea wake katika nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Hata hivyo, huku akitarajiwa kuwa angetoa upinzani mkali, safari yake ya kuwania urais iliishia kuonekana mzaha baada ya kufanya mkutano mmoja tu wa hadhara kabla ya kutokomea nje ya nchi.
Sanaa za kiza (dark arts)?
Baada ya kuboronga kwenye kuwania urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, na baadaye kutangaza kujiondoa kwenye chama hicho, kulizuka tetesi kuwa alichofanya Membe ni “sanaa za kiza” (dark arts) yaani “mambo ya kijasusi”. Ilidaiwa kuwa hata “ugomvi wake na Magufuli” ulikuwa mkakati tu wa yeye kuondoka CCM kama majeruhi kisha apokelewe na upinzani kama “mhanga wa uonevu wa CCM” kabla ya kufanya hujuma dhidi ya upinzani “ndani kwa ndani”.
Kwa vile “marehemu hasemwi vibaya”, Jasusi anahifadhi kilichojiri wakati huo kwa minajili ya kutunza kumbukumbu ya marehemu 😊
Membe vs Musiba
Wakati wa utawala wa Magufuli, Membe alikuwa mmoja wa watu walioandamwa mno na Cyprian Musiba, mtu aliyejipa wadhifa wa “mwanaharakati huru” aliyezusha tuhuma mbalimbali kwa kila aliyemuona kama “mpinzani wa Magufuli” (Jasusi pia alikuwa miongoni mwa wahanga wa Musiba).
Mwaka 2018 wakati Magufuli akiwa hai, Membe alifungua kesi ya madai dhidi ya Musiba, lakini kwa vile ilikuwa “siri ya wazi” kwamba Musiba anakingiwa kifua na Magufuli, kesi hiyo haikutarajiwa kuwa na athari yoyote kwa Musiba.
Hata hivyo, mambo yalibadilika kufuatia kifo cha Magufuli mwezi Machi 2021, ambapo miezi 7 baadaye, Mahakama ilimtia hatiani Musiba na kumtaka amlipe Membe fidia ya shilingi bilioni 6.
Baada ya danadana nyingi, hivi majuzi tu Mahakama ilitoa siku 14 kwa Musiba kulipa deni hilo, vinginevyo kampuni ya ufilisi ya Yono ingepiga mnada mali zake.