Propaganda hizi za kitoto zina msaada gani kwa Mbowe?
Jana nilikutana na moja ya porojo zinazoendelea takriban kila siku kuhusiana na kesi ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe.


Huhitaji kuwa na akili nzuri kubaini kuwa kilichoongewa hapa ni uzushi wa kitoto. Unajua, mtu anaweza kuzusha jambo na akafanya jitihada jambo hilo liaminike, na akajibidiisha kujenga mantiki kwenye uzushi huo. Lakini katika uzushi huu, mzushi husika wala hakuona haja ya kujenga mazingira hayo.
Lakini uzushi huu ni endelevu. Umekuwa ukisikika takriban kila siku. Kwa kifupi, hoja ni kwamba “serikali ya Mama Samia inahangaika kumbembeleza Mbowe akubali kusamehewa kwa masharti ya kuacha kushughulikia suala la Katiba mpya.” Katika uzushi huu mpya, wameongeza na suala jipya la “wabunge 19 wa viti maalum” (Halima Mdee na wenzake).
Hivi serikali ina tija gani katika “kumbembeleza Mbowe” kuhusu jambo lolote lile? Bila kumshushia heshima, hivi kabla ya kukamatwa na kufunguliwa kesi, alikuwa tishio kiasi gani kwa CCM au/na Mama Samia?
Nauliza hivyo kwa sababu porojo hii ya “serikali kumbembeleza Mbowe” imejikita kwenye kujenga hisia kuwa “Mbowe akiwa huru ni hatari sana kwa serikali/Mama Samia.”
Naam, Mbowe ni mwanasiasa mzoefu na ana mchango mkubwa katika siasa za Tanzania hasa za upinzani. Hata hivyo si mwanasiasa tishio kwa CCM, na hajawahi kuwa tishio kwa utawala wowote ule wa CCM. Baada ya jaribio lake kuwania urais mwaka 2005 kutokuwa na mafanikio, Chadema ililazimika kusimamisha wagombea wengine kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho. Mwaka 2010 mgombea alikuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt Willbrord Slaa, kisha mwaka 2015 mgombea akawa kada wa muda mrefu wa CCM, Edward Lowassa, na mwaka 2020 mgombea akawa Tundu Lissu.
Yawezakujengwa hoja kwamba uamuzi wa Mbowe kuwapisha wengine kugombea ulikuwa ni wa busara kwa maana ya kuwapa wengine nafasi ya kugombea, lakini ukweli ulio bayana kuwa uamuzi huo ulichangiwa na ukweli kuwa yeye kama mwanasiasa hakuwa na nafasi ya kutoa upinzani wowote wa maana kwa wagombea wa CCM.
Lakini hata kwa minajili ya kile Waingereza wanasema “giving benefit of the doubt” tukisema Mbowe ni tishio, kwanini serikali ya CCM isitumie “mbinu zake chafu kumlazimisha mwanasiasa huyo akubali matakwa ya chama hicho”?
Pengine hili halifahamiki, na halitofahamika milele: moja ya silaha kubwa iliyotumiwa na Magufuli ilikuwa kutumia ulawiti kama silaha ya kisiasa.

Jasusi @Chahali
@MagufuliJP's Tanzania: "6 young men... were arrested and tortured by police officers and were reportedly... forced to commit sodomy against each other while at the police station" | Vijana 6 walikamatwa, wakateswa na kuamuriwa kulawitiana Hii ndio #Tanzania ya @MagufuliJP https://t.co/FLo67vBzo7Unaweza kusema “ah lakini Magufuli si ameshaondoka”? Ukweli mchungu ni kwamba Magufuli hakufanya hayo kwa vile tu alikuwa dikteta bali mazingira yalimruhusu kufanya hayo. Kilichomwezesha Magufuli kuwa dikteta ni mfumo unaoruhusu violence kama nyenzo ya kisiasa.
Huenda kuna ambao walikuwa hawajazaliwa mwaka 2001, lakini vurugu zilizojiri huko Zanzibar kufuatia wizi wa kura uliofanywa na CCM ulipelekea idadi kubwa ya vifo ambayo mpaka leo haijawahi kuwekwa hadharani.
Lakini matumizi ya violence kama nyenzo ya kisiasa kwa CCM hayakuanzia wala kukomea hapo. Yameendelea kitambo. Lakini tofauti na huko nyuma, katika utawala wa Magufuli, mambo haya yalifanyika waziwazi bila aibu.
Mengi ya yaliyojiri katika utawala wa Magufuli yatabaki kuwa siri milele kwa sababu wengi wa wahanga wake hawawezi kueleza yaliyowasibu walipokuwa kwenye mikono ya watesi wao…kwa sababu ni mambo yanayodhalilisha utu wao.
Lakini hata kama Magufuli angekuwa malaika, maisha ya jela ya Tanzania sio kitu cha kukiombea hata siku moja. Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya wanasiasa wa Chadema waliowahi kuona machungu ya jela huko nyuma, leo wapo mstari wa mbele kudai “acha tu Mbowe akae jela, hakuna kuomba msamaha.” Sawa, ni haki yao ya kikatiba kuwa na msimamo huo lakini naamini faraghani wanafahamu yanayomsibu mwenyekiti huyo wa chama chao.
Nihitimishe kwa kutanabaisha kuwa kuna watu huko Chadema wana maslahi katika kuona Mbowe anasota ndani kwa muda mrefu kadri iwezekanavyo. Na katika kuhakikisha hilo linatokea, wanaibuka na kauli ambazo zinaweza kuchangia kesi ya Mbowe kuzidi kuwa ngumu. Kudai kuwa Mbowe alitumia semu huko gerezani ni kumtafutia mateso ya bure kwa sababu watu hawaruhusiwi kuwa na simu jela.
Lakini pia kwa kutengeneza uzushi huo kwamba “wanambembeleza Mbowe akubali kusamehewa ili akitoka asipiganie Katiba mpya” wanatengeneza mazingira ya “serikali ya Mama Samia kuachana kabisa na wazo la kuweka utu mbele ya sheria na kufuta kesi hiyo.” Kimsingi, wanamfitisha Mbowe na serikali ya Mama Samia ili kusiwe na uwezekano wowote wa kesi hiyo kumalizwa kwa “njia za kibinadamu.”
Mwisho, ikumbukwe tu kuwa licha ya kuwa mwanasiasa, Mbowe ni mfanyabiashara. Na hakuna binashara inayowezekana wakati mhusika yule jela. Mbowe alikuwa mmoja wa wahanga wakubwa wa siasa za chuki za Magufuli ambapo alimhujumu vibaya kwenye biashara zake. Kabla hajasimama vizuri akakumbana na hiyo kesi ya ugaidi na uhujumu uchumi (iliyotengenezwa zama za Magufuli na sio katika utawala huu wa Mama Samia). Kwa mantiki hiyo, kuwepo kwake nje - iwe kwa kukutwa hana hatia na Jaji Tiganga au kwa kupewa msamaha na Mama Samia - kuna tija zaidi kuliko kuendelea kusota jela zaidi ya miezi 6 sasa.
Siku njema