Pande Mbili Za Lissu Kuvuliwa Ubunge

Kilichotokea Ni Mwendelezo Tu Wa Azma Ya Magufuli Kuua Upinzani, Kutawala Milele

Kabla sijaingia kwenye mada hii, ninaomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa nyote mliojiunga kuwa wanachama wa #BaruaYaChahali ambayo sasa ni mkusanyiko wa vijarida vitano kwa wiki.

Mmewezesha #BaruaYaChahali kuweka historia kuwa chapisho la kwanza kabisa la Mtanzania lenye paid subscription (uanachama wa kulipia, japo sipendi neno “kulipia” kwa sababu mnachotoa ni mchango na sio malipo as such). Na mmeniwezesha mtumishi wenu kuwa Mtanzania wa kwanza kuweka historia hiyo. Sina cha kuwalipa bali kuahidi kuwatumikia kwa nguvu zangu zote.

Baada ya shukrani hizo, naomba kuwapa fursa kuwa watu wa kwanza kufahamu kuhusu mkakati wangu wa mabadiliko ya kisiasa nchini Tanzania. Naomba mniruhusu nisitoe ufafanuzi kwa sasa, nitaeleza kwa kirefu katika toleo lijalo. Kwa sasa, soma bandiko hili ambalo baadaye litakuwa kwenye ukurasa wangu wa Instagram.

“Kuacha kelele za siasa” hakuhusiani na kijarida hiki kinachokujia kila Jumatatu. Hata hivyo, sintoongelea masuala yanayohusiana na “vita yangu ya msituni” iliyoanza rasmi leo Julai Mosi 2019.

Twende kwenye mada ya wiki hii. Takriban kila mmoja wenu anafahamu kilichojiri wiki iliyopita ambapo mbunge wa Singida Mashariki. Tundu Lissu alivuliwa ubunge.

Mengi yameshaongewa na nisingependa kuyarudia. Hata hivyo, ni muhimu kuliweka suala hali katika muktadha stahili, hasa kwa vile takriban kila linalojiri katika wakati huu tulionalo sio tu litahukumiwa na vizazi vijavyo bali pia lina athari kwetu na kwa vizazi vijavyo. Ni muhimu kwa sie tunaojihangaisha kuipigania nchi yetu na tunaojitoa mhanga kuwa wasemaji wa wasio na sauti, kutokaa kimya katika nyakati kama hizi.

Kuna pande mbili za Lissu kuvuliwa ubunge. Ya kwanza, takriban sote twaijua.

Naam, uamuzi wa kumvua Lissu ubunge ulifanywa na Jiwe Magufuli. Na kwa bahati mbaya, Mtu Mfupi Ndugai hakuwa na jinsi ya kutoafikiana na Jiwe kwa sababu tangu mwanzo alijitengenezea mazingira ya kuwa kibaraka wa Jiwe.

Wanaomfahamu Jiwe wanaeleza kuwa ni mtu anayependa mno kutumia watu, kisha kuwatelekeza kama sio kuwadhuru kabisa. Na mtumishi wako nina mfano hai, niliubandika juzi kwenye ukurasa wangu wa Instagram.

Huyu ndiye Jiwe bwana. Kibaya zaidi kwa Mtu Mfupi ni ukweli kwamba nafasi yake ya Uspika ipo mikononi mwa Jiwe. Na ndio turufu aliyoitumia Jiwe kumshinikiza Mtu Mfupi kuchukua maamuzi hayo.

Kibaya zaidi kwa Mtu Mfupi, majuzi kaingia kwenye ugomvi na mtoto mpendwa wa Jiwe, Pince Bashite of Koromije. Bashite anataka Mtu Mfupi aidha apigwe chini muda huu au jina lake likatwe hapo mwakani. Kwahiyo ishu ya Lissu ni kama Jiwe kampe Mtu Mfupi lifeline ya kujinusuru.

Lakini suala hili la Lissu kuvuliwa ubunge lina upande wa pili usiopendeza kama upande wa kwanza. Na upande huo unahusu mapungufu ya Lissu mwenyewe na chama chake cha Chadema.

Sijui nianzie wapi, lakini pengine turudi nyuma, na kuikumbuka Chadema ambayo baadhi yetu tuliiunga mkono, kabla ya ujio wa Lowassa. Chama hiki kiliaminika mno kiasi kwamba baadhi ya watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa walikuwa radhi kuweka rehani ajira zao na hata maisha yao, na kukipatia siri nyeti chama hicho.

Ni mazingira hayo ndiyo yaliyoiwezesha Chadema kuibua skandali mbalimbali za ufisadi kama vile EPA, Kagoda, Buzwagi, Richmond, Meremeta, nk. Watumishi mbalimbali wa umma, ikiwa ni pamoja na wa Kitengo, waliiamini Chadema na kuiona kama chama kinachoweza kuwa mbadala halisi wa CCM.

Lakini mara baada ya kumpokea Lowassa mwaka 2015, chama hicho kimwekuwa kipokipo tu. Turufu kuu ya Chadema ilikuwa kwenye msimamo wake dhidi ya ufisadi. Lakini chama hicho kililazimika kuitosa ajenda hiyo ili kutomuudhi Lowassa,mwanasiasa ambaye Chadema ilimuita “baba wa ufisadi” kwa miaka 9 mfululizo, kabla ya kumpokea na kujaribu kumsafisha kwa miezi mitatu.

Chadema hawawezi kukwepa lawama kuhusu ishu ya Lissu kuvuliwa ubunge kama ambavyo haiwezi kukwepa lawama kwenye ishu ya kuondokewa na lundo la madiwani na baadhi ya wabunge (na kwa taarifa tu, kuna wengine kadhaa wanasubiri muda tu kabla ya “kuvua gwanda na kuvaa gamba.”)

Laiti ingekuwa “Chadema ile tuliyoizowea” sio tu ingebaini mapema kuhusu madiwani na wabunge waliokuwa na mpango wa kuhama, na pengine kuchukua hatua mwafaka, bali pia hata hii ishu ya Lissu kuvuliwa ubunge ingefahamika mapema kabla haijatokea.

Angalia mfano hai wa “Chadema ile tuliyoizowea” hapa pichani

Kwa sababu siasa ni kama vita, na zama hizi za siasa za chuki za Jiwe ni vita kubwa kabisa. Kwahiyo ni lazima chama kinachotaka kuwa mbadala wa CCM kiwe na intelijensia ya kutosha kufahamu mikakati mbalimbali inayolenga kukidhoofisha na hata kukiuwa.

Jiwe ana dhamira ya dhati kuiangamiza Chadema. Na pengine hili wala halihitaji kuwa na intelijensia kwa sababu lipo bayana.

Sijui tatizo hasa la Chadema ni ombwe la uongozi au imeelemewa na mamluki, lakini hakuna jitihada za makusudi kuziwia dhamira ya Jiwe kuwaangamiza. Muda huu tunaoongea, mbunge mmoja wa chama hicho ni afisa mwandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho wanafahamu hilo.

Lakini pia chama hicho kina mapandikizi mbalimbali, wa CCM na wa kitengo, ikiwa ni pamoja na huyu diwani wa chama hicho aliyepo hapa Uingereza masomoni, ambaye sio tu ni mtumishi wa kitengo bali pia alikuwa mtu muhimu kwenye mkakati wa kiitengo kuniangamiza mie mtumishi wako

Kwahiyo laiti Chadema “ingekuwa inajielewa” basi kwa hakika ingefahamu mpango wa Jiwe kumtumia Mtu Mfupi kumvua Lissu ubunge. Lakini kama ambavyo chama hicho hakijihangaishi kujua wabunge wake gani wapo mbioni kukitosa na kujiunga na CCM, hakukuwa na jitihada zozote kubaini mikakati dhidi ya Lissu na chama hicho kwa ujumla.

Sie wengine wenye ujuzi si haba wa “sanaa za kiza” (dark arts) yaani ujasusi/ushushushu tumekuwa tayari muda wowote ule kutoa msaada lakini kanuni muhimu ya msaada ni kwamba “msaada huombwa.” Leo hii nikiwafuata Chadema na kuwaambia flani na flani wanawahujumu, hisia za haraka zinaweza kuwa “huyu Chahali katumwa na Jiwe/kitengo.” Kwahiyo licha ya kuumizwa na jinsi chama hicho kinavyohujumiwa vibaya mno, inabidi kukaa kimya tu.

Kosa la pili la Chadema kuhusu ishu ya Lissu ni kosa endelevu. Na hili sio kwa Chadema au vyama vya upinzani pekee bali Watanzania kwa ujumla.

Katika mazingira haya tuliyoishi nayo kwa miaka minne, unakwenda mwaka wa tano sasa, kwanini Jiwe asiamini kuwa “udikteta unalipa”? Maana Watanzania wanasubiri mpaka mtu atekwe ndio waanze kelele za #BringBackNaniliu. Ndo maana mtumishi wako nimeachana na kupoteza muda wangu kushiriki kwenye hizi kampeni za #BringBack. Na kinachokera ni kwamba hao watu tunaopiga kelele kwa ajili yao, wakishakuwa nrought back hawana muda wa kututafuta kusema japo asante ya kinafiki.

Naam, Chadema, Upinzani na Watanzania mmemruhusu Jiwe kulamba asali na sasa kachonga mzinga. Ninaamini kila mtu mwenye akili nzuri anafahamu maovu ya Jiwe lakini hakuna udhati katika kukabiliana nae.

Ni hivi, Jiwe ameshafanya maovu mbalimbali, na anajua fika kuwa pindi akitoka madarakani, atakuwa rais wa kwanza katika historia ya nchi yetu kutupwa jela. Hilo analifahamu fika. Anajua kuwa akitoka madarakani kuna mengi yanayofichwa muda huu yatabainika, kwa mfano idadi ya Watanzania waliouawa huko MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji)

Mtumishi wako niliwahi kufanya petition kuhusu ishu ya MKIRU lakini ikakwama kutokana na Tanzania kutokuwa signatory wa mkataba unaohusu haki za “raia waliopotezwa na dola.”

Kwahiyo, sio tu Jiwe na mwanae Bashite wataendelea kuwatumia #WatuWasiojulikana dhidi yenu bali pia ishu za uonevu na unyanyasaji wa kisiasa kama hiyo ya Lissu zitaendelea.

Image

Naam, #WatuWasiojulikana ni Jiwe na mwanae Bashite.

Kwa upande wa Lissu mwenyewe, kwanza ni vema akafahamu kuwa kupoteza ubunge kwa sababu zinazofanana japo kwa mbali na zilizopelekea mbunge mwingine wa chama hicho , Joshua Nassari, kupoteza ubunge, kunaweza kabisa kujenga taswira inayozunguka ishu ya Nassari kuwa “alipewa chake.”

Ofkoz, sio rahisi kwa Lissu “kununuliwa na Jiwe,” lakini tunaishi katika zama ambazo lolote lawezekana. Na ikumbukwe kuwa baadhi yetu hatukuzipokea vema taarifa za malipo ya stahili zake ambayo baadhi ya tetesi yalidai yaliambatana na masharti flani.

Licha ya Lissu kuwa mwanasheria aliyebobea, lakini pia anafahamu fika jinsi Jiwe anavyotamani kumwangamiza baada ya kumkosakosa kwenye jaribio la mauaji. Sasa kwanini atoe mwanya wa kisheria kama huo wa kutosaini fomu za Tume ya Maadili?

Sie ambao tumekuwa katika mapambano endelevu ya kuhakikisha hatutoi fursa kwa majahili kutudhuru tunafahamu bayana kuwa wakati sie twahitaji kila sekunde ya dakika kutofanya kosa lolote lile, watesi wetu wanahitaji sekunde moja tu kutufanyizia.

Unapokuwa katika mapambano dhidi ya adui anayepania kukuangamiza, hupaswi kufanya kosa la aina yeyote ile, unless iwe kosa la kibinadamu tu.

Sijui kama hiyo dhamira ya Lissu kwenda mahakamani itakuwa na ufanisi, lakini kwa kiasi kikubwa tu, hujuma hii ingeweza kuzuiwa kwa njia mbalimbali nizilizotanabaisha katika makala hii.

Nimalizie kwa kuwakumbusha nyote mliiomba kuongezewa muda kujisajili uanachama wa #BaruaYaChahali, ombi lenu lilikubaliwa jana na nimewapatia wiki mbili, hadi tarehe 14 ya mwezi huu. Utaratibu wa kutuma mchango ni uleule wa awali

Kwa mlio nje ya Tanzania, mwaweza kuchangia kwa

KUBONYEZA HAPA.

Nawatakia Julai njema.

Ndimi mtumishi wenu

Evarist Chahali