Ombi Kwenu Waheshimiwa Nape, January Makamba na Ridhiwani : Kama Wahanga wa "Uanahabari wa Musiba" Huko Nyuma, Tupieni Jicho Jitihada za JAMVI LA HABARI Kuturejesha Zama za "Magazeti ya Chuki"
Miongoni mwa sababu zinazotupa baadhi yetu matumaini katika serkali ya Mama Samia Suluhu ni uwepo wa watendaji ambao huko nyuma walikuwa wahanga wa siasa za chuki.
Moja ya nyenzo muhimu ya kusambaza siasa hizo za chuki zilizotawala sehemu kubwa ya utawala wa Magufuli ni magazeti ya kihuni ambayo yaliweka kando kabisa taaluma ya uandishi wa habari na yakajipa jukumu la kuwaandama wale wote ambao Magufuli aliowaona kuwa wapinzani wake.
Magazeti kama Tanzanite na Fahari Yetu yaliyomilikiwa na Musiba yalifanya kila aina ya uovu kunyanyasa, kutisha na kutukana watu wasio na hatia kwa minajili ya kumpendeza Magufuli. Hata hivyo, taarifa zilidai kuwa magazeti hayo yalikuwa yakiendeshwa kwa fedha za serikali chini ya usimamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Sambamba na magazeti hayo ya Musiba ni gazeti la Jamvi la Habari ambalo japo asili yake ni kwenye vyama vya upinzani, lilifanikiwa kujipendekeza kwa Magufuli na likawa kama “kulwa na doto” wa Tanzanite/Fahari Yetu kwenye kusambaza chuki.
Miongoni mwa wahanga wa magazeti hayo ni pamoja na Mheshimiwa Nape Nnauye, Mheshimiwa January Makamba na Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ambao kwa nyakati mbalimbali waliandamwa na magazeti hayo ya kizushi.
Kadhalika, Mkurugenzi mpya wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, alikuwa mmoja wa wahanga wa uandishi wa habari wa kusambaza chuki wa magazeti hayo, kutokana na nafasi yake ya wakati huo kama mtangazaji wa BBC Swahili, ambayo zama hizo ilionwa na Magufuli na wapambe wake kuwa ni “chombo cha habari cha mabeberu.”
Wakati ni wazi kuwa zama za Musiba na takataka zake za Tanzanite na Fahari Yetu zimefikia ukingoni, Jamvi la Habari limefanikiwa kujipendekeza kwa serikali ya Mama Samia kwa mtindo uleule wa uandishi wa kusifia, pengine zaidi ya magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo.
Hata hivyo, majuzi gazeti hilo limejiingiza kwenye sakata la Ngorongoro, na kama kawaida yake, likadai kuwa wanaharakati wanaotetea haki za Wamasai wa eneo hilo wamehongwa pesa ili kuiua Ngorongoro na Serengeti.


Gazeti hili linataka kuturudisha kulekule kwenye siasa za chuki ambapo kila mtetezi wa haki za binadamu/kijamii alituhumiwa kuwa kuwadi wa mabeberu, amelipwa fedha na watu flani, bila kusahau nyenzo muhimu ya udhalilishaji kuwa mhusika ni shoga.
Sasa kwa vile Mheshimiwa Nape, January, Ridhiwani na Zuhura ni wahanga wa aina hiyo isiyofaa ya uandishi wa habari, nitumie nafasi hii kuwasihi wafanye kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Jamvi la Habari halitumii ovyo uhuru wa habari ambapo alhamdulilah Mama Samia anaurejesha si haba, kudhalilisha watu wengine kwa vile tu wanasimamia kitu tofauti na matakwa ya gazeti hilo.
Ni muhimu waheshimiwa hawa kukumbuka jinsi takataka za Musiba zilivyoanza mashambulizi yake: zilianza kuwalenga wanaharakati wa mtandaoni kabla hazijawageuzia kibao waheshimiwa mbalimbali. Ndivyo chuki inavyofanya kazi. Inaanza dhidi ya mtu mmoja, baadaye watu kadhaa, kisha kundi dogo na hatimaye inasambaa dhidi ya lundo la watu.
Nihitimishe kuwa naandika haya kama Mtanzania ninayeendelea kuwa na imani na Mama Samia, na ni imani hiyo kwake inayonisukuma kutoa tahadhari hii kwani aina ya uandishi wa habari usiozingatia maadili unaweza kuchafua sifa za Mama Samia hasa kwa vile gazeti hilo la Jamvi la Habari limekuwa mstari wa mbele kummwagia sifa (kujikomba?)
Siku njema