Nchi Zinazopambana Dhidi Ya UVIKO-19 Kwa Uwazi Zina Nafasi Nzuri Ya Kufufua Uchumi

Former Reserve Bank of India (RBI) governor Raghuram Rajan said that he warned that the negative impact of demonetization would outway the postives. AFP

Jana usiku nilikuwa naangalia kipindi cha runinga cha Hard Talk cha BBC ya hapa Uingereza ambapo mhojiwa alikuwa Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya India Raghuram Rajan (pichani).

Huyu ni mmoja wa wachumi wanaoheshimika duniani. Kilichonifanya niandike makala hii ni swali aliloulizwa kuhusu mustakabali wa uchumi wa nchi mbalimbali pindi janga la UVIKO-19 (Ugonjwa wa Virusi vya Korona vya mwaka 2019) ukidhibitiwa au kuondoka kabisa.

Pamoja na mambo mengine aliyoongelea, kuna pointi moja ya msingi iliyonigusa na ndio nitaiongelea kwa sababu inaihusu Tanzania yetu. Pointi hiyo ni kuaminika kwa serikali iliyoko madarakani wakati wa janga la UVIKO-19. Kuaminika huko ni kwa sura mbili, ndani na nje ya nchi.

Kwa Tanzania, ndani ya nchi sio tatizo sana kwa Magufuli kutokana na Watanzania kuwa na vipaumbele fyongo.Japo Gavana mstaafu Rajan anabashiri kuwa serikali zinazofanya mzaha katika kukabiliana na janga la UVIKO-19 zitapelekea kuamka kwa hasira za umma, hasira ambazo mchumi huyo anatabiri zitapelekea kung’oka kwa tawala husika, Watanzania wengi ni kama wamekubali kuwa kinachoendelea muda huu ni stahili yao.Kwahiyo uwezekano wa “kulipa kisasi” dhidi ya mzaha katika jinsi serikali ya Magufuli inavyoshughulikia janga la korona ni sawa na sifuri.

Mtihani kwa serikali ya Magufuli ni jinsi ilivyopoteza kuaminika kwake kimataifa. Yayumkinika kuhisi kwamba Tanzania itakuwa na wakati mgumu kuanzia kwa nchi jirani kama Uganda, Kenya, nk ambazo muda huu zinajibidiisha vya kutosha kupambana na janga la UVIKO-19, na itakuwa na wakati mgumu zaidi kwa mataifa ya Magharibi ambayo baadhi yameonyesha bayana kutorishidhwa na jinsi Magufuli anavyoihadaa dunia kuhusu UVIKO-19.

Ni rahisi kwa akina Kigwangalla au MC wa serikali Dkt Abbas kuhadaa kuhusu ujio wa watalii feki lakini ni ngumu kugeuza hadaa hizo kuwa mapato ya utalii ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania.

Itachukua muda mrefu kwa mtalii yeyote yule kutia mguu Tanzania kwa sababu serikali ya Magufuli imeamua kupuuza “utaratibu wa kimataifa” wa kubainisha visa vipya vya korona, vifo na idadi ya waliopona. Katika mfano wa mtaani, ni kama usikie kuwa nyumbani kwa rafiki yako flani kuna mgonjwa wa kifua kikuu, lakini rafiki yako huyo hataki kusema lolote kuhusu afya ya mgonjwa wake. Ni wazi kuwa hata kwa mtutu hutoenda kumtembelea.

Nini mtazamo wako?