'Mpiga Ramli Mkuu' Aumbuka, Aliwadanganya Waumini Wake Kuwa Mama Samia Hakualikwa Kushiriki Mkutano, Mama Yetu Aonekana Akishiriki Kwa Video

Niwe mkweli. Nimeshatanabaisha mara kadhaa kuwa namuunga mkono Mama Samia. Kwa sababu mbalimbali. Kubwa zaidi ni ukweli kwamba kufanikiwa kwake ni kufanikiwa kwetu sote. Na baadhi yetu tumechoka kuiona Tanzania yetu ikisuasua badala ya kuwepo mahali inapostahili. Naamini kwa dhati kuwa tukimpa sapoti ya kutosha, Mama Samia anaweza kutufikisha kwenye Tanzania tunayostahili.

Kuna watakaokebehi kuwa “ah wewe jasusi unataka ukuu wa wilaya,” au wengine kudhihaki kuwa “unataka Mama akusamehe urudi nyumbani.” Uzuri ni kwamba mie ni mmoja wa Watanzania wanaotukanwa mno, na kwa hakika moja ya vitu visivyonisumbua ni matusi. Si kwamba napenda matusi bali sijawahi kunyimwa usingizi na matusi.

Kipindi cha utawala wa marehemu Magufuli kitakumbukwa zaidi kwa siasa za chuki zilizoshuhudia watu kadhaa wasio na hatia wakiumizwa kwa njia moja au nyingine. Na moja ya silaha muhimu ya utawala huo dhalimu ilikuwa kutumia matusi na udhalilishaji. Na wakala mkuu wa matusi alikuwa shetani aitwaye Musiba. Sidhani kama kuna mtu asiyemfahamu.

Huyu haramia ndio mwasisi wa jina la “Watu Hatari.”

Lakini inaonekana kuwa jahili huyo amepata mrithi wake. Na licha ya ukweli kuwa Musiba alikuwa akisaidiwa na dola kutukana na kuchafua watu, hakuwa na hadhira kubwa. Magazeti yake yaliishia kuwa kama toilet papers na mtandaoni alionekana kituko. Followers wake pekee walikuwa wahuni wa MATAGA (sijui wamefia wapi viumbe hawa).

Lakini huyu mrithi wa Musiba yeye ana followers lukuki, takriban nusu milioni huko Twita. Na ana supply ya kutosha ya kitu Watanzania wanapenda mno, yaani UBUYU. Na alikuwa hana uhaba wa ubuyu wakati wa zama za Magufuli kwa sababu Waziri mmoja wa zamani wa zama za Kikwete, na ambaye alijaribu bila mafanikio kuwania urais, alikuwa ndio chanzo kikuu cha ubuyu kwa huyo “mrithi wa Musiba.”

Sasa baada ya Mama Samia kuingia madarakani, moja ya mambo aliyoyafanya na kufanikiwa vizuri ni kuziba mianya ya uvujishaji taarifa, hali iliyopelekea galacha ya ubuyu ageukie maeneo makuu mawili, “upigaji ramli” na “kuwalisha watu matango pori.” Lakini kwa vile wapenzi wa ubuyu wapo tayari kwa lolote, ramli imekuwa kama mlo kwao huku wakitoka vitambi kwa kulishwa matango pori mfululizo.

Tuache hayo. Jana, mpiga ramli huyo alifanya uzushi kuwa Mama Samia hakualikwa kwenye mkutano ulioitishwa na Ufaransa kuhusu uchumi wa Afrika ulioathiriwa na janga la korona.

Hii ndio ramli yake

Alilishwa matango pori kuwa Mama Samia hakualikwa. Lakini wanasema Mungu hamfichi mnafiki, muda mfupi baadaye Ikulu ikaweka hadharani picha za Mama Samia akihudhuria mkutano huo kwa njia ya video.

Kabla ya ramli hiyo, aliendelea na udhalilishaji dhidi ya Mama Samia kwa kumlumu “kwa kauli yake ya kuwataka polisi wa trafiki wasigeuze makosa kuwa kitegauchumi.”

Na kama kawaida yake, ameshindwa kuficha chuki yake kubwa dhidi ya ndugu zetu Wazanzibari, na kudai Mama Samia ni chiriku…TYPICAL ZANZIBARI. Kioja ni kwamba mmoja wa waumini wake wakubwa ni Mzanzibari pia.

Huyu mtu si kwamba hajawahi kuona jema lolote la Mama Samia bali kama nilivyotanabaisha kwenye MAKALA HII, yeye na wenzake ni sehemu ya mkakati wa kumhujumu Mama Samia.

Hata hivyo, anawezeshwa na makundi makuu mawili. Kubwa zaidi ni la “wapenda ubuyu,” ambao hawakerwi na matusi na udhalilishaji unaofanywa na jahili huyo alimradi anawapatia dozi ya ubuyu. Na japo sasa ni mwendo wa matango pori zaidi kuliko ubuyu, bado ana lundo la waumini.

Kundi la pili ni la baadhi ya wafuasi wa Upinzani. Kutokana na ombwe la uongozi, baadhi ya wafuasi wa Upinzani wanaona “wanaharakati wa matusi” kama watu wa kuongelea kero zao (kama ni kero kweli au mazowea tu ya ulalamishi). Na kwa kutambua hilo, ndo maana mhalifu huyu amegeuka rangi kama kinyonga, na kujinadi kuwa ni mfuasi wa upinzani ilhali amekuwa akiwatukana Wapinzani mara kwa mara

Na huku akiwahadaa waumini wake, kipindi cha uchaguzi alikuwa anamponda Lissu na kumnadi “jasusi” Membe.

Ni matumaini yangu kwamba Watanzania japo wachache wanaokerwa na matusi na udhalilishaji unaofanywa na mhalifu huyu dhidi ya Mama yetu Samia hawatoendelea kumvumilia kiumbe huyu.

Sambamba na hilo, ni matumaini yangu kuwa vyombo vya dola vitachukua hatua stahili hasa kwa vile mpiga ramli huyu ni mhalifu aliyetoroka kifungo cha miaka 15 mwaka 2015 baada ya kuhukumiwa kwa kosa la wizi wa shilingi milioni 177. Waweza kusoma taarifa kamili kuhusu uhalifu wake HAPA.