Milipuko ya Mabomu Uganda, Tahadhari ya Ugaidi Kenya, Mashambulizi ya Kigaidi Msumbiji, DRC ni "Wake-up Call" kwa Mzaha wa Kesi ya "Ugaidi" Dhidi ya Mbowe

Kuna jamaa yangu mmoja alinitumia ujumbe majuzi kunipongeza kuwa napaswa nijivunie jitihada zangu kwenye sekta ya intelijensia hususan kutupia jicho habari/matishio ya ugaidi.

Nilimshukuru lakini nilikataa pongezi hizo kwa sababu moja kuu. Hupaswi kujivunia kuwa mzalendo, kwa sababu uzalendo sio sifa bali wajibu. Kama ambavyo hatujivuni tunapokula, kwa sababu ni wajibu wetu kufanya hivyo, ndivyo ambavyo uzalendo unapaswa kuwa suala la lazima.

Muda mfupi uliopita kumetokea milipuko miwili ya mabomu jijini Kampala, Uganda. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa mtu mmoja amefariki, lakini huenda idadi ikawa ni kubwa zaidi. Milipuko hiyo imetokea mjini kati (city centre) jirani na jengo la bunge la nchi hiyo. Sijivunii kuwa miongoni mwa vyombo vya habar vya kwanza duniani kuripoti tukio hilo. Sijivunii kwa sababu huo ni wajibu, si suala la kujivunia.

Pengine blogu ya Ujasusi kuwa miongoni mwa vyombo vya habari vya kwanza duniani kuripoti habari hiyo ni sababu tosha kwako kujisajili ili utumiwe habari zinazochapishwa kila siku kuhusiana na ujasusi na majasusi. Jisajili HAPA.

Wakati hayo yakiendelea nchini Uganda, huko Kenya nako kumetolewa tahadhari kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi katika maeneo ya mpaka kati ya nchi hiyo na Somalia. Tahadhari hiyo imetolewa na Uingereza.

Wakati huo huo, kikundi cha kigaidi cha “wilaya ya Afrika ya Kati” ya kikundi cha kigaidi cha ISIS (Islamic State Central Africa Province, kwa kifupi ISCAP) kinaendelea na kampeni zake za kigaidi nchini Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nimekuwa nikiripoti mfululizo kuhusu kikundi hicho. Kadhalika nimeandika chambuzi mbili za kiintelijensia kuhusu matishio yaliyopo kwa Tanzania kuhusiana na kikundi hicho.

Kwa muda mrefu, wanasiasa mbalimbali wa CCM wamekuwa wakitumia suala la ugaidi kama “mdoli” wa kuwanyanyasia wapinzani. Huko nyuma chama cha CUF kilituhumiwa kuwa cha kigaidi. Na sasa Chadema inazushiwa tuhuma hizo, huku Mwenyekiti wake Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe, akiendelea kufanyiwa uonevu katika kesi ya kubambikiwa kwamba alipanga vitendo vya kigaidi.

Rai yangu kwa serikali ya Mama Samia, Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi na CCM kwa ujumla ni fupi: ACHENI KUFANYIA MZAHA SUALA LA UGAIDI.

Mwisho, kuanzia wiki hii, ninawaletea mfululizo wa makala kuhusu suala la uzalendo, na jinsi kudidimia kwake kunavyoweza kuwa tishio kwa usalama kwa Tanzania yetu, Mfululizo huo unachapishwa katika gazeti la RAIA MWEMA kila Jumatano.

Siku njema