Mgogoro Kati Ya Jiwe na Kimombo

Kunahitajika Mjadala Wa Kitaifa Kuhusu Mustakabali Wa Kiswahili

Nianze kwa kuwashukuru wengi mliojitokeza kujisajili upya kwa ajili ya muundo mpya wa kijarida hiki, ambapo kwa malipo kidogo tu ya sh 50,000 kwa mwaka, “mwanachama” (paid subscriber) atatumiwa sio tu kijarida hiki bali vijarida vingine vinne.

Idadi ya waliokwishajisajili ni watu 70. Pengine inaweza kuonekana ni idadi ndogo lakini kwangu ni bora niwatumikie watu wawili wanaothamini jitihada zinazowezesha utumishi wangu kwao kuliko lundo la mamia ya watu ambao miongoni mwao hawana hata muda wa kufungua baruapepe ninazowatumia.

Nimalizie utangulizi huu kwa kuwajulisha nyote mliojisajili kuwa nimewatumia toleo la kwanza la #BaruaYaShushushu.

Ninakaribisha maoni kuhusu kijarida hicho.

Twende kwenye mada ya leo. Lakini kabda ya kuingia kwenye mada hii, naomba kutumia twiti ifuatayo kama reference

Niliandika twiti hiyo kama mchango wangu katika mjadala uliovuma wiki iliyopita kuhusu “Kiingereza za Jiwe” (Magufuli).

Kimsingi uwezo duni wa Kiingereza cha mkuu huyo wa nchi haukupaswa kuwa jambo la mjadala laiti wahuni wanaofahamika kama MATAGA (Make Tanzania Great Again) wasingelikoroga. Na uthibitisho ni huu hapa

MATAGA ni wababaishaji flani walioajiriwa huko Idara ya Usalama wa Taifa wakiwa hawajui A wala B kuhusu taaluma hiyo, na kwa vile ajira zao zilikuwa za upendeleo, wala hawakupelekwa “Malindi” (Mbweni ) kwenye chuo cha Idara hiyo ambapo kila afisa anayejiunga anatakiwa kufanya kozi inayofahamika kama JBC.

Sasa hao vichwapanzi wa MATAGA waliokotwa tu mtaani, kigezo muhimu kikiwa kutoka Kanda ya Ziwa kama Jiwe, na kukabidhiwa majukumu yaliyo nje kabisa ya uwezo wao. Matokeo yake wamekuwa wakitusumbua mitandaoni.

Jiwe mwenyewe amenukuliwa mara kadhaa akitanabaisha kuwa hao MATAGA ni watupu kabisa kichwani. Na jukumu pekee wanalolimudu ni kusifia hata visivyostahili kusifiwa. Ndio hawa wanaitwa “praise team.”

Turudi kwenye ishu ya “Kiingereza cha Jiwe.” Kwamba lugha hiyo inamsumbua Jiwe, hilo halina mjadala. Lakini halipaswi kuwa suala la maana sana hasa ikizingatiwa kuwa background ya Jiwe ni katika sayansi (Kemia), na si ajabu kwa wenzetu waliosoma masomo ya sayansi kusumbuliwa na Kiingereza.

Tatizo la MATAGA ni kwamba Jiwe alipooendesha “mkutano muhimu” kwa Kiingereza, ilikuwa ni habari ya kujivunia. Yaani “kuwananga wale wanaomtuhumu Jiwe kuwa anachapia kwenye lugha hiyo ya Malkia Elizabeth wa Pili.” Lakini Jiwe alipolikoroga kwenye dhifa ya kitaifa huko Zimbabwe ambapo alishindwa kuongea Kiingereza, na MATAGA kwa uchovu wao wakashindwa kuwa wakalimani, MATAGA hao hao wakaanza kukiponda Kiingereza kilekile walichomsifia Jiwe alipoongoza “mkutano muhimu.”

Tukiweka kando “ugomvi kati ya Jiwe na Kiingereza” na ubabaishaji wa praise team wa MATAGA, kuna haja ya msingi kwa sisi kama Taifa kuwa na mjadala mpana kuhusu mustakabali wa Kiswahili. Tatizo lililopo ni zaidi ya mapungufu ya akina Jiwe. Tatizo ni kwamba tupotupo tu. Kiingereza ni mgogoro kwa Watanzania wengi, lakini kwenye Kiswahili nako tunakutana na lundo la wababaishaji wanaojifanya hawawezi kuongea Kiswahili “full-time” na inawalazimu kuchanganya Kiswahili na Kiingereza. Sikiliza wabunge wwetu wanavyojifanya hawajui Kiswahili vizuri.

Jiwe ameahidi kupeleka walimu wa Kiswahili huko Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe lakini porojo hizo hazijaanza leo. Na kwa bahati mbaya, zitaendelea kwa muda mrefu.

Kuna mjadala ambao ulikufa kabla haujaanza kuhusu matumizi ya Kiswahili sekondari hadi chuo kikuu. Pengine ni muhimu kuufufua mjadala huu japo binafsi sidhani kama Kiswahili kinajitosheleza kiasi cha kuweza kutumika kama lugha ya kufindishia sekondari hadi chuo kikuu.

Tunatakiwa kama taifa tuamue moja, aidha Kiswahili ni muhimu kuliko Kiingereza na si kwa maneno tu bali kwa vitendo pia, au Kiingereza ni muhimu kuliko Kiingereza na akina Jiwe wafanye bidii kuboresha uwezo wao kwenye lugha hiyo, au - na hili kwangu naona ndio wazo zuri zaidi - kukipa kipaumbele Kiswahili kama lugha ya taifa lakini kutosahau nafasi ya Kiingereza hususan kwenye masuala ya kimtaifa na “maeneo mageni” kama ya sayansi na teknolojia.

Nikamilishe toleo hili kwa kuwakumbusha wanaohitaji kujisajili upya kuwa “wanachama” (paid subscribers) wa kijarida hiki, usajili unaendelea BONYEZA HAPA

Nakutakia siku na wiki njema.

Ndimi mtumishi wako

Evarist Chahali