Mama @SuluhuSamia Leo Anaanza Ziara Ya Siku 3 Nchini Misri. Je Wanaodai "Anasafiri Sana" Wana Hoja ya Msingi au "Kila Jambo Kwao Ni Baya"?

Kama unafuatilia twiti zangu basi bila shaka umeshakumbana na twiti zangu kadhaa zinazotaja “Kanuni ya FBI.” Kwa kifupi kanuni hiyo isiyo rasmi inasema hivi “FBI (Shirika la Ushushusu wa ndani nchini Marekani) hawakuulizi kama unajua kitu flani endapo hawana uhakika kuwa tayari unajua kuhusu hicho wanachokuuliza.”

Huwa natumia msemo huo ninapowasilisha tafakuri zangu ambazo tayari nimeshazipatia hitimisho lakini nahitaji tu kusikia mitazamo ya wadau wengine. Na msemo huo umetokea kupata mashabiki kadhaa huko Twitter, which is always nice.

Twende kwenye mada husika. Jana baada ya kupatikana taarifa kuwa Mama Samia atakuwa safarini tena, this time akielekea Misri, ikiwa ni siku chache tu baada ya kututembelea hapa Glasgow ambako alishiriki Mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari za tabianchi. Na safari hiyo pia ilikuja siku chache tu baada ya Mama yetu kutembelea Marekani ambako alihudhuria na kuhutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katika pitapita zangu mtandaoni, nimekutana na mijadala mbalimbali ikongelea “safari za Mama.” Tatizo la mijadala hiyo ni kwamba mingi imejikita kwenye misimamo ya kiitikadi kuliko maslahi ya taifa. Ni mijadala kati ya wana-CCM vs Wapinzani.

Na hili ni tatizo kubwa kwa Tanzania yetu. Takriban kila jambo linaangalia kwa miwani ya itikadi. Ndio maana wengi wa watu wasio na itikadi huamua kukaa kimya badala ya kujiingiza kwenye mijadala ambayo haina tija.

Tukiweka kando wahusika kujikita kwenye itikadi, hoja kuu kwenye mijadala hiyo ni, kwa upande mmoja, “Mama Samia anasafiri sana,” ilhali kwa upande mwingine, “Hakuna tatizo kwa Mama Samia kusafiri sana,” au “wala sio kweli kuwa anasafiri sana, bali tatizo analinganishwa na mtangulizi wake, marehemu Magufuli ambaye ilikuwa nadra kwake kufanya safari nje ya Tanzania.” Lakini pia kuna wanaotetea safari hizo kwa kigezo kwamba “zina manufaa.”

Kwa wanaofuatilia chambuzi zangu za kijasusi, niliwahi kuongelea mapema kabisa, mara baada ya Mama Samia kuapishwa, kwamba moja ya changamoto atakazokumbana nazo ni kulinganishwa na watawala wawili waliomtangulia, marehemu Magufuli, na mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.

Na nilitanabaisha kuwa sababu kuu ya ulinganishi huo ni tofauti kubwa baina ya watangulizi hao. Kwa vile mada inahusu safari za Mama Samia, naomba niweke kando tofauti nyingine kati ya Jk na marehemu Magufuli.

Jk alikuwa msafiri kweli kweli, mpaka akapewa jina la utani la Vasco da Gama

Angalia twiti zangu hizi za “miaka hiyo” 😊

Lakini mtangulizi wa Jk, marehemu Magufuli, hakuwahi kutoka nje ya Afrika hadi mauti yalipomkuta Machi 12, 2021.

Safari ya kwanza ya marehemu Magufuli nje ya Tanzania ilikuwa Machi 7, 2016 alipozuru Rwanda, zaidi ya miezi minne tangu aingie madarakani. Safari ya kwanza ya Mama Samia nje ya Tanzania ilijiri takriban wiki tatu tu baada ya kuingia madarakani, ambapo April 11 mwaka huu alizuru Uganda japo ilielezwa kuwa ni ziara ya kikazi kuliko ziara rasmi ya kitaifa.

Kwa kumlinganisha na Jk, takriban mwaka mmoja baada ya kuapishwa, marehemu Magufuli alikuwa amefanya safari mbili tu nje ya Tanzania kulinganisha na safari 25 za mtangulizi wake, Jk.

Mpaka mauti yanamkuta, marehemu Magufuli alikuwa amefanya safari 8 tu nje ya Tanzania - Rwanda, Kenya, Ethiopia, Uganda, Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Malawi. Na safari zote zilikuwa barani Afrika.

Kwa mujibu wa takwimu pekee nilizoweza kuzipata, hadi Januari 2015, Jk alikuwa ameshasafiri nje mara 427 kwa mujibu wa mdau mmoja huko Jamii Forums aliyekuwa akirekodi kila safari lakini nahisi aliishiwa pumzi ilipofika Januari 2015 miezi 9 kabla ya Jk kumaliza urais wake.

Kwahiyo, kwa mahesabu yasiyo rasmi, Jk alifanya wastani wa safari 42 kwa mwaka sawa na takriban safari 3 kila mwezi. Huyu mheshimiwa alipenda safari kupita maelezo.

Kwa mujibu wa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania, moja ya sababu zilizofanya utawala wa Jk ugubikwe sana na tuhuma za ufisadi ni hizo safari mfululizo. Kwamba kwa muda mwingi, “urais ulikuwa mikononi mwa watu wengine” wakati yeye yupo safarini. Sasa kwa nchi zetu zenye mfumo “wa kuungaunga” wa utawala, ukimpa mtu dakika chache tu za kufanya maamuzi muhimu, mamilioni kadhaa yatayeyuka. Hili halihitaji uwe jasusi kama mie kulielewa.

Kwa upande wa Mama Samia, hadi sasa - takriban miezi saba tangu aingie madarakani Machi 19 mwaka huu - ameshasafiri nje ya Tanzania mara 10, yaani wastani wa safari moja nje kila mwezi. Pamoja na safari ya leo Novemba 10 huko Misri,

Mama Samia ameshazuru Uganda (Aprili 11, 2021)

Kenya (Mei 4, 2021)

Rwanda (Agosti 2, 2021)

Msumbiji (Juni 22, 2021)

Burundi (Julai 16, 2021)

Malawi (Agosti 16, 2021)

Zambia (Agosti 24, 2021)

Marekani (Septemba 19, 2021)

na hapa Uskochi/Uingereza (Oktoba 31, 2021)

(kama kumbukumbu zangu zipo sahihi. Naomba nisirushiwe mawe endapo kuna nchi nimeisahau hapo😊).

Mtazamo wangu

Kwanza, wanaohoji kuhusu safari hizo wana kila haki na sababu ya kufanya hivyo. Kila safari ya Mama Samia inagharamiwa na walipakodi wa Tanzania.

Pili, wanaotetea safari hizo nao wana haki ya kufanya hivyo japo katika pitapita zangu mtandaoni nimebaini kuwa wana upungufu kwenye hoja za kutetea wingi wa safari hizo.

Tatu, kwa kuzingatia jinsi marehemu Magufuli alivyoifanya Tanzania itengwe kimataifa, ni muhimu kwa Mama Samia kuboresha mahusiano yetu kimataifa japo si lazima iwe kwa kusafiri.

Nne, na hili ndio la muhimu zaidi kwangu, tatizo sio safari mfululizo as such. Tatizo ni kwamba wasaidizi wa Mama Samia wanafeli katika kuwaelimisha Watanzania kuhusu umuhimu wa safari hizo (kama upo). Tatizo kama hilo lilikuwepo zama za Jk, ambapo wahusika walikuwa bize kutuonyesha picha za Jk akiwa nje badala ya kuwafahamisha Watanzania kuhusu faida za ziara husika (kama zipo).

Siku njema