Mama Samia Anahujumiwa Au Anajihujumu?

Suala la tozo kwenye miamala ya simu limeibu maswali mbalimbali kuhusu Mama Samia. Bila kuorodhesha maswali hayo, kubwa ni iwapo anahujumiwa au anajihujumu.

Ndio tunafahamu kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto lukuki za kiuchumi na kunahitajika hatua mbalimbali kurekebisha uchumi. Hata hivyo, tiba ambayo ni sumu kwa mgonjwa si tiba bali sumu. Kadhalika, japo ni muhimu kwa serikali ya Mama Samia kuchukua hatua mbalimbali kuukwamua uchumi wa Tanzania, hatua hizo hazipaswi kuwaumiza walalahoi.

Hadi muda huu, Mama Samia anaonekana kupuuza vilio vya Watanzania kuhusiana na tozo za miamala. Ni kupuuza huko kunakopelekea dhana kuwa ni yeye, na wala si Waziri wake wa Fedha, Mwigulu, aliyeamua kuanzisha tozo hiyo ambayo makali yake yameanza kuonekana jana.

Baadhi yetu tumekuwa watetezi wa hiari wa Mama Samia. Na haijawa kazi rahisi kwani licha ya kurushiwa tuhuma mbalimbali ikiwa na pamoja na kuambiwa tunataka u-DC, hakuna jitihada zozote kwa upande wa serikali kujibidiisha kukabiliana na tuhuma hizo.

Kuna malalamiko kuwa Mama Samia amekuwa mzito kufanya maamuzi yanayopaswa kufanywa haraka. Uamuzi wake wa kurithi takriban kabineti nzima ya mtangulizi wake na kushindwa kuunda kabineti yake mwenyewe unaweza kutafsiriwa kuwa ni mapungufu katika utendaji kazi wake.

Kuna baadhi ya mawaziri wanaonekana kabisa kuwa mzigo lakini hakuna hatua zinazochukuliwa. Kuna ripoti ya CAG aliyopokea kwa mbwembwe lakini haijafanyiwa kazi.

Kuna jeshini ambako alimtoa Mnadhimu Mkuu Luteni Jenerali Yakubu Mohamed na kumpa ubalozi lakini hadi sasa, takriban miezi miwili hivi, hajateua mbadala wake.

Kuna Idara ya Usalama wa Taifa ambako inafahamika kuwa bayana kuhusu upinzani mkali uliokuwepo dhidi ya Mama Samia kuapishwa kuwa Rais wa sita wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Marehemu John Magufuli.

Lakini hayo sio muhimu kulinganisha na suala hili la muamala. Na endapo Mama Samia hatochukua hatua stahili, sio tu itakuwa ni doa kwa uongozi wake bali pia anaweza kuanza kupoteza sapoti anayohitaji mno kutoka kwa wananchi wa kawaida.