Makamanda Wanaume Chadema Mmeaibisha. Umahiri Wenu Ni Kujimwambafai Tu Na ID Feki Mtandaoni, Lakini Kudai Haki Mnawasusia BAWACHA Peke Yao 🙄

Ni wazi kwamba licha ya kelele zote mtandaoni, hadi kufikia hatua ya kumtisha Mama Samia kwamba “atanyolewa na wembe uliotumika kumnyoa Magufuli.”

Je huo wembe umepotea?

Ukweli mchungu ni kwamba sio tu hakukuwa na wembe bali pia hakukuwa na plan B kuhusu nini kifanyike endapo Mbowe angekamatwa.

Na ndio maana, masaa 72 yamepita tangu Mbowe afikishwe mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi lakini hakuna tamko lolote kutoka Chadema. Ni kama Mbowe ametelekezwa.

Naamini kuna wanaokerwa na hali hii lakini wanaogopa kutukanwa maana sasa huo ndio mtaji mkubwa wa chama kupitia kwa baadhi ya wanaharakati wa mtandaoni ambao lugha pekee wanayomudu kuongea ni matusi.

Kama nilivyoandika kwenye makala ya jana hapa, Chadema ina ombwe la uongozi. Na wala ombwe hilo halijasababishwa na Mbowe kuwa jela. Lilikuwepo kabla hajakamatwa. Ndio maana kwa muda mrefu sasa, mwelekeo wa chama umekuwa ukitegemea zaidi mwelekeo wa baadhi ya wanaharakati wa mtandaoni.

Lakini pengine kitu cha kufadhaisha sana ni tukio la jana ambapo wana-BAWACHA kadhaa walijitoa mhanga na kwenda Ubalozi wa Marekani kuomba nchi hiyo iingilie kati ili Mbowe atolewe jela.

Japo wazo lenyewe halina mashiko, kwa vile siku ya nane leo tangu Mbowe akamatwe na ubalozi wa nchi hiyo haujasema lolote, wana-BAWACHA hao wanastahili pongezi kwa ujasiri wao.

Tukio hili linaashiria ukweli mmoja mchungu: makamanda wa kiume wa Chadema ni mahiri katika kujimwambafai huko mtandaoni, na wepesi wa kutukana wanapokosolewa, lakini ni useless linapokuja suala la kuingia front. Wepesi kujazana TwitterSpaces lakini hawana jeuri ya kufanya kilichofanywa na akinamama wa BAWACHA.

Ukweli huu mchungu, na mwingineo ambao mie pamoja na watu wengine tumekuwa tukiuweka hadharani, umechochea matusi zaidi kutoka kwa makamanda. Lakini sie wengine matusi ni kama pongezi. musiba alitukana mpaka akachoka. Kigogo nae katukana mpaka kachoka. Matusi hayajawahi kumtoa mtu uhai.

Kwa upande mwingine, wakati BAWACHA wanakwenda Ubalozi wa Marekani kuomba uingilie suala hilo, ubalozi huo upo bize kumpongeza Mama Samia kwa kuwezesha upatikanaji wa chanjo ya korona ambapo Wamarekani wamechangia dozi milioni moja.

Kadhalika, ubalozi huo umeeleza kuhusu ujio wa Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Marekani barani Afrika, Jenerali Stephen Townsend, ambaye pamoja na mambo mengine amefungua mazoezi ya pamoja ya kijeshi baina ya Marekani na Tanzania, ambayo mara ya mwisho yalifanyika 2017.

Hawa ndio wa kuwategemea wamshurutishe Mama Samia amwachie Mbowe?

Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha ndugu zangu wa Chadema hasa vijana, kutambua kwamba kujipa matumaini sio mkakati unaoweza kuleta ufanisi. Kuendelea kujazana upepo mtandaoni huku mnatumia fake ID kutukana watu hakutowezesha Mbowe kutendewa haki. Na kujazana TwitterSpaces ilhali mkiambiwa kuingia mtaani mnakuwa wadogo kama piritoni ni uselessness ya hali ya juu.

Ushauri wangu kwenu ni DIALOGUE. Kama hiyo waliyoifanya BAWACHA ila wamekosea tu kwenda Ubalozi wa Marekani kwa sababu wa kuongea nae ni Mama Samia na serikali yake na sio “hao mabeberu ambao Lissu kahangaika nae miaka kadhaa na hawajawahi kuiwekea Tanzania vikwazo.” Na suala tu la kuomba waweke vikwazo linakipotezea chama hicho uhalali wa kuwa wawakilishi wa wananchi kwa sababu mwakilishi wako hawezi kukuombea njaa.

Mwisho kabisa, Waingereza wanasema matatizo ni mama wa ubunifu. Yawezekana changamoto hii ikapelekea baadhi ya wana-Chadema kutafakari kuhusu chama chao -kilipotoka, kilipo na kiendako - na kuamua kufanya uamuzi sahihi. Kubwa kabisa ni kuhakikisha kuwa chama hicho hakiporwi na wanaharakati wa mtandaoni.

Alamsiki