MakalaYa Wazi: Tathmini Ya Lissu Kuahirisha Kurejea

Baadhi Yetu Tulihisi Mapema Kuwa Asingerejea Septemba Hii

Kabla ya kuingia kwenye makala hii ya wazi ya kijarida cha #BaruaYaChahali naomba kukupatia matangazo mawili. Yote yanahusu vitabu vyangu. La kwanza ni kuhusu vitabu hivi viwili ambavyo vipo sokoni. Maelezo ya jinsi ya kuvipata yapo pichani.

Tangazo la pili ni kuhusu kitabu changu kipya kinachohusu “KUBETI KULIKOPITILIZA” ambacho nitakichapisha siku chache zijazo. Endapo utakihitaji au una mtu ungetamani kumuona anaondoka kwenye janga hilo la kubeti kulikopitiliza, basi unaweza kufanya pre-order kwa kunitumia baruapepe HAPA.

Baada ya matangazo hayo mawili ambayo natumaini hayajakukwaza, twende kwenye mada husika.

Awali ilitangazwa kuwa Bwana Tundu Lissu angerejea nyumbani jana ikiwa ni siku ya maadhimisho ya siku aliyoshambuliwa kwa risasi, na ni kwa miujiza tu ya Mungu akaweza kusalimika. Kama ulikuwa unatafuta uthibithso wa uwezo wa Mungu dhidi ya watesi wako, tukio hilo la Lissu ni mahala pazuri kuanzia.

Nisingependa kuingia kwa undani kuhusu nani hasa alipanga na kutekeleza shambulio hilo, lakini huhitaji kuwa shushushu mstaafu kama mie kubaini kuwa Jiwe na mwanae Bashite ni prime suspects. Kuna sababu milioni kidogo za wao kutaka Lissu - au mtumwingine yeyote yule anayeonekana tishio kwa utawala wao - aondoke duniani.

Na wala sio ngumu kubaini kwanini serikali ya Jiwe imepuuzia kuchunguza tukio hilo kwa sababu za wazi. Jambazi hawezi kuchunguza ujambazi alioshiriki.

Sasa kwa vile ni mwaka sasa tangu Lissu afanyiwe unyama huo na sio tu hakuna uchunguzi bali pia waliohusika hawajakamatwa, ingekuwa sio busara kwa Lissu kurudi Tz.

Wengine tulitambua hilo mapema

Na majuzi ilipofahamika kuwa Lissu hatorudi, nikakumbushia tweet hiyo

Haikuwa salama kwa Lissu kurudi. Hilo halina mjadala. Lisiloingia akilini ni uamuzi wa Lissu mwenyewe, na Chadema kwa upande mwingine, kuendeleza porojo kuwa mwanasiasa huyo angerejea huku wakijua bayana kuwa haitokuwa hivyo.

Unaweza kusema “ah ilikuwa mbinu ya kumkomoa Jiwe na Bashite, au CCM.” Hata kama ni kweli kwamba ilikuwa mbinu, hasara ni kubwa kuliko faida.

Moja ya hasara kubwa ni marudio ya kilichojiri wakati Chadema ilipotangaza maandamano ya UKUTA. Wakahamasisha wanachama wao nchi nzima, dakika za mwisho “wakachomoa” na kutoa sababu zisizo na mashiko.

Naomba ieleweke kwamba hapa siilamu Chadema kwa kutofanya maandamano hayo bali kuyaahirisha kwa sababu zisizo na maana, tena dakika za majeruhi. Kama “intelijensia” yao ilibaini kuwa maandamano hayo yangepelekea maafa, walipaswa sio tu kutangaza kuyafuta bali pia kuwasilisha ujumbe huo kwa wanachama wao katika namna ambayo isingepelekea kuwakatisha tamaa.

Sidhani kama chama hicho kikiamua kufanya maandamano yoyote yale watajitokeza watu wa kushiriki maandamano hayo kwa sababu ni kama ishaanza kuzoeleka kuwa ni chama hicho ni magwiji wa mikakati hewa.

Kuliwahi kuwa na “Operesheni Sangara,” sijui ikaishia wapi. Kukawa na “Operesheni Ondoa Msaliti,” sijui ikaishia wapi. Lakini kubwa kuliko zoteilikuwa hiyo “Operesheni UKUTA,” ambayo nayo iliishia kuwa porojo tu,

Naomba ieleweke kwamba ninafahamu fika mazingira yalivyo magumu kwa vyama vya upinzani nchini Tanzania. Hata hivyo, kuna mambo moja muhimu kabisa: kwanza, hata wakati wa ukoloni, mazingira yalikuwa kama haya yaliyopo sasa ambapo mkoloni hakuridhia akina Nyerere kufanya harakati za kupigania uhuru. Na kwa kutambua hilo, akina Nyerere walitumia kila njia iliyowezekana na hatimaye sio tu mkoloni alisalimu amri bali pia uhuru ulipatikana.

Kwahiyo, kutarajia kwamba labda siku moja Jiwe ataamka na kupatwa na roho ya huruma na kuruhusu shughuli za kisiasa, ni ndoto ya alinacha. Jiwe ameshaonja asali sasa amechonga mzinga.

Kama nilivyowahi kuandika mara kadhaa huko nyuma, hakuna incentive yoyote kwa Jiwe kubadili mwenendo wake. Kwamba licha ya kuwakandamiza wapinzani kwa nguvu kubwa kabisa, response pekee ya wapinzani imekuwa ni kulalamika. Well, hata Tanesco wamekuwa wakilalamikiwa kwa takriban miaka 20 sasa na wamegoma katakata kubadilika. Kwanini itarajiwe kuwa Jiwe atabadilika?

Najua kuna mtakaosema “ah ni rahisi kwako kuongea hayo kwa sababu upo Ulaya.” Well, kuna njia mbili tu kuhusu hali fulani: aidha kuiacha kama ilivyo au kupambana nay kwa nguvu zote ili kuibadili au kuondoa. Kwahiyo aidha kutokubaliana na mwenendo wa siasa za kikatili za Jiwe na kupmabana nae kwa nguvu zote au kumuacha aendelee kuipeleka nchi anakotaka.

Kwa sababu ukweli mchungu ni kwamba sio tu Jiwe atarudi madarakani hapo Noivemba mwakani lakini atarudi madarakani huku akiwa amewahujumu wapinzani vibaya mno kiasi kwamba kutakuwa na wabunge na madiwani wachache tu wa upinzani. Siasa za Tanzania baada ya uchaguzi mkuu ujao zitakuwa za chama kimoja zaidi ya ilivyo sasa.

Kuhusu Bwana Lissu, Chadema wamemwangusha kama walivyomwangusha Sugu, au Mbowe na Esther Matiko, au Lema, au diwani Luena wa Kilombero, au aliyekuwa katibu wa chama hicho Kata ya Hanasisifu Daniel, au Ben Saanane…orodha ni ndefu. Ni kwamba chama hicho kimeyakubali maovu hayo, na ndio maana hakijafanya chochote zaidi ya kulalamika.

Turejee kwenye suala la Bwana Lissu. Japo usalama wake ni muhimu kabisa na ilikuwa uamuzi wa busara kutorudi nyumbani kinyume na ratiba, kutojihangaisha kuwaeleza wanachama wa chama hicho - na pengine Watanzania kwa ujumla - sio tu ni dharau lakini pia ni mwendelezo wa ubabaishaji wa chama hicho.

Kusema safari imeahirishwa kwa vile kuna appointment nyingine na daktari wake ni sababu isiyo na mashiko kwa sababu ni wazi Lissu alikuwa anajua fika ratiba yake ya matibabu.

Pengine unaweza kusema hata kama ameahirisha kurudi sio big deal. Naomba kutofautiana nawe. It is big deal kwa sababu Lissu ni moja ya majina yanayotajwa kuhusu urais kwa tiketi ya Chadema/upinzani hapo mwakani. Kwahiyo consistency ni muhimu ili aaminike beyond wanaomwamini katika chama chake. Ikumbukwe kuwa mahesabu ya siasa za uchaguzi Tanzania yanategemea watu wasio na vyama, hawa ambao wanaweza kudhani Lissu sio mtu serious kuwania nafasi hiyo ya urais, au pengine afya yake sio mwafaka kumudu kuchuana na Jiwe.

Je una maoni gani? Waweza kuniandikia HAPA.

Mwisho, endapo unataka kuwa mwanachama kamili wa vijarida vitano vonavyounda #BaruaYaChahali, BONYEZA HAPA kjiunga. Na endapo unataka kujiondoa kwenye orodha ya wanaotumiwa kijarida hiki, BONYEZA HAPA.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali