Makala Ya Wazi: Tuna La Kujifunza Katika Uvumi Kuhusu Afya Ya Jiwe

Kabla ya kuingia kwenye mada husika ningependa kueleza masikitiko yangu kutokana na taarifa inayosambazwa na Yericko Nyerere anayedai kuwa mie ni miongoni mwa watu wanaoendesha akaunti ya mtu anayejiita Kigogo.

Labda niweke wazi tu kwamba hii si mara ya kwanza - na huenda si mara ya mwisho - kuzushiwa tuhuma na Yericko. Mwaka 2015, nilipoamua kuacha kuishabikia Chadema baada yya chama hicho kumpokea Lowassa, Yericko alinifanyia jambo moja ambalo kwa hakika lilinisikitisha mno. Julai mwaka huo nilifiwa na baba yangu Mzee Chahali, na miongoni mwa watu waliotoa rambirambi alikuwa Mheshimiwa January Makamba.

Na pengine haikuwa uamuzi sahihi kutangaza, nilieleza kuwa Mheshimiwa January alitoa pole ya sh 500,000/=. Na Yericko akaigeuza hiyo pole ya Mheshimiwa January kuwa ni rushwa niliyopewa na January ili nimnadi Jiwe. Sawa, tunaweza kuwa na tofauti za kiitikadi, lakini si vema hata chembe kuingiza siasa kwenye msiba.

Hapa katikati, Yericko akaanzisha uzushi kuwa mie ndio “Daudi Balalli” wa Twitter. In fact yeye ndio mwasisi wa tuhuma hiyo. Sasa kuna wakati huyo mtu anayejiita Balalli alitoa tuhuma flani dhidi ya Mange, na matokeo yake nikaishia kutukanwa matusi ya nguoni na Mange aliyedai kuwa mie ndiye huyo Balalli, madai yaliyotokana na uzushi ulioanzishwa na Yericko.

Sasa ameniingiza kwenye ugomvi wake na huyo mtu anayejiita Kigogo, sambamba na tofauti zake yeye Yericko na Zitto Kabwe. Na jana amesambaza ujumbe huu kwenye Whatsapp groups mbalimbali

This is not fair. Kwa sababu tangu nifahamu kutumia mtandao wa internet sijawahi hata mara moja kutumia jina feki. Nipo Jamii Forums kwa jina langu halisi, Facebook, Instagram, Twitter, Medium, nk. Ninachapisha vijarida vya #BaruaYaChahali kwa jina langu halisi, kama ambavyo naendesha blogu yangu yenye umri wa miaka 13 sasa, ya “Kulikoni Ughaibuni,” kwa jina langu halisi pia.

Sijaandika haya ili kuonewa huruma. Wala sijaandika haya ili mtu achukue jukumu la kumshauri Yericho aache anachofanya. Mie ni mmoja wa Watanzania wanaoongoza kwa kuzushiwa “kila baya” unaloweza kufikiria. Kabla ya Musiba kunitaja kuwa mmoja wa “Watu Hatari,” Kitengo kiliwekeza vya kutosha kwenye kunizushia kila jambo. Lakini naamini kuwa bado nimesimama imara kwa sababu namtanguliza Mungu wangu katika kila jambo.

Lakini pia, Waingereza wana msemo “you can’t bring a good man down.” Sitaki kujisifu kuwa mie ni mtu mwema saaaana, lakini najitahidi kutokuwa mtu muovu. Najitahidi kutumia muda mwingi kuwatumikia watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ninyi mnaotumiwa vijarida hivi. Naamini kuna watu wengi wanaonihukumu vizuri kwa mema ninayowatendea kuliko mabaya wanayosikia kutoka kwa watu wengine.

Enewei, tuachane na hilo. Naamini takriban kila mmoja wenu anafahamu kilichojiri katika takriban masaa 72 yaliyopita. Labda nieleze ilivyokuwa kwa upande wangu. Ijumaa jioni nilitumiwa meseji na mtu mmoja ninayemwamini, kwa amaepata taarifa kwamba Jiwe amepatwa na heart attack na afya yake sio nzuri. Kama ilivyo kawaida yangu nikipata taarifa yoyote ile, nilianza jitihada za kuhakikisha kuwa “sijalishwa matango pori.”

Ijumaa usiku na Jumamosi kutwa nzima na jana Jumapili nzima, takriban kila jitihada ya kupata taarifa yenye uhakika hazikuzaa matunda. Nilielezwa kuwa tukio hilo limegubikwa na usiri mkubwa mno.

Kiu yangu ilitokana na (a) haki yangu kama Mtanzania kufahamu kilichomsibu Rais wangu (b) kama muumini wa “Sharing Is Caring,” niliona nina wajibu wa kupata taarifa sahihi na kuzifikisha kwenu wanajamii.

Sijui kwa hakika kilichotokea maana wakati taarifa zikiendelea kudai kwamba hali ya Jiwe sio nzuri, akajitokeza katika hafla ya jana ya kuapisha wateuliwa kadhaa.

Kuna theories kadhaa hapa. Moja ni kwamba kweli alipatwa na matatizo ya kiafya na hali ilikuwa mbaya lakini baadaye akapata nafuu. Pili ni kwamba kweli alikumbwa na matatizo ya kiafya lakini lakini hali haikuwa mbaya kama ilivyoelezwa. Tatu, “picha imetengenezwa” kwa sababu wanazojua wahusika. Na nne, ukisikia kinachoongewa na MATAGA na Praise Team, “suala hilo limezushwa tu na vibaraka wa mabeberu, na halina ukweli wowote.”

Sijui ukweli ni upi, na sina hakika kama utafahamika. Hilo sio la muhimu zaidi ya mambo makuu mawili. Kwanza, mie mtumishi wenu napenda kutumia fursa hii kumuomba samahani mtu yeyote yule niliyemkwaza katika jitihada zangu za kuhabarisha nilichokuwa nikikisikia kuhusu suala hilo. Mie ni muumini wa “Sharing is Caring,” na kutokana na mazingira yaliyopo ambapo media zimezibwa mdomo, sie wengine tunalazimika kufanya kazi za vyombo vya habari ili kuwafikishia habari ninyi wanajamii.

Hata hivyo, jukumu hili la kusambaza habari kdri unavyozipokea lina risks kadhaa. Moja ni hiyo kama iliyotokea jana. Watu watafurahi kadri unavyowahabarisha lakini pindi habari husika ikichukua mweleleko tofauti na unavyorpoti, utaishia kulaumiwa au hata kuitwa mzushi.

Naomba kukiri kwamba huenda hili ni tukio la mwisho kwa mie mtumishi wako kujipa jukumu la kuuhabarisha umma. Si kwamba nahofia kuitwa “mzushi” au “wakala wa mabeberu,” hapana. Ni ile hali tu kwamba watu unaohangaika kuwa-update kinachoendelea kadri unavyokipokea hawakawii kukugeuka pindi habari husika ikichukua mwelekeo mpya.

Nadhani hili linapaswa kuwa funzo kwa kila anayejitolea kuwa mstari wa mbele kuufahamisha umma kuhusu masuala mbalimbali yasiyowekwa hadharani.

Kwa upande mwingine, tukio hilo limezidi kuonyesha ukweli ambao naamini wengi wenu mnaujua: KUNA MPASUKO KATIKA JAMII. Hili halihitaji utafiti wala ramli.

Na mpasuko huu ni matokeo ya siasa za chuki ambao zimeshika hatamu mno katika utawala wa Jiwe. Kumekuwa na jitihada kubwa sana zinazofanywa na wapambe wa Jiwe kama vile Musiba kuwahadaa Watanzania kuwa kila anayemkosoa Rais hata kwa nia njema basi ni adui wa taifa, msaliti, anawatumikia mabeberu, nk. Lakini pia, kuna jitihada kubwa za kuzifanya siasa za upinzani zionekana kama uhaini na ndio maana viongozi wengi wa vyama vya upinzani wamebambikiziwa kesi za ajabu ajabu.

Ni katika mazingira ya aina hiyo ndio tunashuhudia watu wengi tu wakitamani kiongozi wao akumbwe na janga, na wakipata tetesi hata kama si za kweli kwamba anaumwa, baadhi wanatamani “Ziraili afanye vitu vyake.”

Huu si mwelekeo mzuri kwa taifa letu. Ni rahisi kufanyia mzaha umoja na mshikamano uliotufikisha hapa, lakini pindi ukitutoka itakuwa vigumu mno kuurejesha.

Je Jiwe atabadilika baada ya kufahamu “hisia za Watanzania wengi” dhidi yake? Naomba nihifadhi hisia zangu kwa sasa, labda nikukaribishe wewe mdau unieleze unachofikiri. Waweza kuacha commet hapo chini au NIANDIKIE HAPA.

Mwisho, kijitabu hiki cha bure cha twiti za motivation kitaanza kusambazwa wiki hii kwa mliojisajili.

Kama hujajisajili na unahitaji kufanya hivyo, JISAJILI HAPA.

Ndimi mtumishi wako,

Evarist Chahali