Makala Ya Wazi: Jiwe na Kabudi Wameuza Nchi Kwa Barrick?

Waraka huu wa Zitto unaibua maswali magumu

MAKUBALIANO YA SERIKALI NA BARRICK GOLD CHANGA LA MACHO

Jana, Julai 19, 2019 Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Corporation imetoa Taarifa kwa Umma ya kuinunua Kampuni yake tanzu ya Acacia Mining Plc kwa jumla ya Dola za Marekani Milioni 428. Baada ya malumbano ya takribani miezi 5 Barrick na Acacia wamekubaliana juu ya thamani ya Kampuni ya Acacia kuwa ni Dola za Marekani milioni 951 (wastani wa TZS 2.2 Trilioni).

Itakumbukwa kuwa kabla ya sakata la Makanikia la Mwezi Machi mwaka 2017, Kampuni ya Acacia ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani Milioni 4,400 (wastani wa TZS 10 Trilioni). Kwa mujibu wa kanuni za Masoko ya Hisa na Mitaji, taarifa za manunuzi ya makampuni huwekwa wazi pamoja na nyaraka nyengine zote husika.

Kwa Watanzania nyaraka muhimu katika mauziano haya ya Acacia, ni ile ya Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick katika kumaliza mgogoro wa Makanikia na masuala ya Kodi. Nyaraka hiyo (ambayo Serikali imekuwa ikiificha baada ya Majadiliano yaliyofanywa na Prof. Palamagamba Kabudi) sasa imewekwa wazi kama Kiambatanisho namba 4 cha nyaraka za manunuzi ya Acacia.

Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na Barrick Gold Corporation mnamo tarehe 19 Mei, 2019. Makubaliano hayo ni MABAYA, ya HOVYO, yasiyo ya KIZALENDO na yanayoumiza nchi kuliko makubaliano yaliyokuwepo kwa Mujibu wa sheria ya Madini ya mwaka 2010. Kwa ufupi tu ni kuwa Rais John Pombe Joseph Magufuli na Waziri Palamagamba Kabudi WAMEUZA nchi kwa vipande vya dhahabu. Nitaeleza kama ifuatavyo.

Kiambatanisho namba 4 kimeweka muhtasari wa kinachoitwa ‘Material Terms’ katika Makubaliano ya awali kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold ambayo yamesainiwa (INITIALED) mwezi Mei mwaka huu. Kimsingi Barrick imelazimishwa na kanuni za masoko ya mitaji kuweka wazi makubaliano hayo. Ni masikitiko makubwa kuwa Serikali yetu haijathubutu hata kuliambia Bunge kuwa kuna makubaliano ya namna hiyo wakati wa Bunge la Bajeti, imesaini kwa siri kama ulivyosainiwa mkataba wa Buzwagi.

Ikumbukwe kuwa makubaliano hayo yamesainiwa wakati Bunge likiwa linaendelea na mkutano wake jijini Dodoma. Sisi kama wawakilishi wa Wananchi imebidi kusubiri masoko ya mitaji ya ‘MABEBERU’ wa London yaweke wazi masuala yanayohusu nchi yetu. Hii ni dharau kubwa ambayo Serikali ya Rais Magufuli imefanya kwa Wananchi na kwa Bunge. Sasa tutazame ni nini Serikali yetu imekubaliana na Barrick Gold katika maeneo matano tu.

1. Dola Milioni 300 za kumaliza mgogoro KIINI MACHO

Serikali imekubaliana na Barrick kuwa italipwa Dola milioni 300 (wastani wa TZS 700 Bilioni) kama malipo ya kumaliza mgogoro wote (full, final and complete settlement) na SIO kishika uchumba kama Serikali ilivyoeleza umma. Barrick watalipa fedha hizi kwa muda wa MIAKA 7 na zitakuwa ni baada ya kuondoa madai yote ya kodi ambayo Acacia inaidai Tanzania.

Itakumbukwa kuwa Acacia Group ina madai ya marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT refunds) inayofikia takribani Dola za Marekani milioni 240 (wastani wa 552 Bilioni). Hivyo katika malipo ya Dola za Marekani Milioni 300, zitakazobakia baada ya kutoa madai ya VAT refunds ni Dola Milioni 60 (wastani wa 138 Bilioni) tu. Kama tutakavyoona katika hoja ya pili hapa chini hata hizi Dola za Marekani Milioni 60 kimsingi hazitatolewa.

2. Barrick Gold Wamesamehewa Kodi ya Ongezeko la Mtaji USD 85.6M

Serikali ya Tanzania imetoa misamaha mbalimbali ya Kodi kwa Kampuni ya Barrick Gold katika makubaliano yaliyoingiwa ikiwemo kodi ya ‘Capital Gains’ ambayo inatokana na mauzo ya hisa za Acacia kwa Barrick. Itakumbukwa kuwa mwaka 2012 Bunge lilitunga sheria ya kutoa Kodi ya Ongezeko la Mtaji kwa mauzo ya mali zilizopo Tanzania ili kudhibiti ukwepaji wa Kodi.

Barrick inainunua Acacia kwa Hisa ambazo Barrick haikuwa inamiliki ambazo zimepewa thamani ya Dola Milioni 428. Capital Gains Tax ya 20% ilipaswa kulipwa lakini Rais Magufuli na Profesa Kabudi wametoa ‘waiver’ (Msamaha) na kupoteza Mapato halali na ya kisheria kwa nchi yetu ya Dola Milioni 85.6 (wastani wa TZS 200 Bilioni). Tukirejea hoja ya kwanza hapo juu utaona kuwa sio tu Tanzania kiuhalisia haitapata Dola Milioni 300, bali pia tunaipa zawadi Barrick ya Dola Milioni 25.6 (wastani wa TZS 59 Bilioni) za ziada.

3. Tanzania kupewa Hisa 16% za daraja B lakini Watanzania kunyimwa umiliki wa 30% kupitia Soko la Hisa la DSE

Ni kweli kuwa Serikali itapewa hisa za bure 16% kwenye Kampuni tanzu zote za Acacia hapa nchini kama tulivyoambiwa na Serikali. Lakini hisa hizo ni za Daraja la B ambazo ni hisa dhaifu kulinganisha na zile za Daraja la kwanza. Hisa hizo haziruhusiwi kuuzwa, hazina kura kwa masuala fulani fulani ya Kampuni na huwezi hata kuziweka kama dhamana ya mikopo. Hata mgawo wa gawio hisa hizi hupata baada ya wale wa daraja A kulipwa kwa ukamilifu.

Licha ya makubaliano haya ya hovyo na yasiyo na tija, Serikali yetu imetoa ‘waiver’ (msamaha) kwa Barrick kutoorodhesha hisa kwenye Soko la Hisa la Tanzania. Sheria ya Madini ya mwaka 2010 (Wakati wa Waziri William Ngeleja) na Kanuni zake iliweka sharti kwamba ni lazima makampuni ya madini yauze 30% ya hisa kwa Watanzania kwenye soko la Hisa la Tanzania.

Makubaliano ya Mei 2019 kati ya Barrick na Serikali ya Tanzania yametoa msamaha kwa Barrick kutekeleza sharti hilo la kisheria. Uamuzi huu unavunja sheria za nchi, ni hujuma kwa Watanzania kumiliki maliasili zao na ni ukosefu wa maarifa ya kiuchumi kwa kiwango kisichomithilika wala kuvumilika.

4. Bunge lafungwa mikono kubadili sheria yeyote

Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick wamekubaliana kuwa baada ya mkataba wao kukamilika Bunge la Tanzania haliwezi kutunga sheria yeyote ambayo itabadili makubaliano hayo na kodi zote zilizokuwa zinafanya kazi wakati wa kuingia makubaliano hazitaweza kubadilishwa kipindi chote ambacho Barrick watakuwa wanafanya kazi Tanzania (fiscal stabilisation).

Makubaliano ya namna hii ndiyo kitu kilicholeta Buzwagi mwaka 2007 ambapo Serikali za Rais Mkapa na Rais Kikwete ziliingia mikataba ya kulifunga Bunge kutimiza majukumu yake ya kikatiba kama Dola (sovereign). Sheria ya Madini yam waka 2010 iliondoa sharti hili kufuatia mapendekezo ya Kamati ya Bomani. Rais Magufuli na Waziri Kabudi wameturudisha kwenye unyonyaji wa kihayawani kabisa.

5. Barrick wameruhusiwa kufungua kesi ughaibuni kinyume na Sheria

Kwa mujibu wa sheria mpya za madini za mwaka 2017 makampuni yamezuiliwa kufungua mashauri yake nje ya Tanzania. Migogoro yote inapaswa kushughulikiwa na mahakama za ndani ya nchi. Serikali ya Tanzania imekubaliana na Barrick kuwa migogoro itafanyika kwa mujibu wa kanuni za UNICITRAL na Rais wa Kituo cha usuluhishi wa migogoro cha Singapore ndio atateua wasuluhishi ambao hapatakuwa na Mtanzania.

Serikali mara zote iliambiwa kuwa mabadiliko ya sheria kuhusu ‘arbitration’ hayakuwa halisi na ni ulaghai. Serikali yenyewe imekuwa ya kwanza kuvunja sheria yake yenyewe kwa kuingia makubaliano na Barrick Gold kuwa Mahakama zetu hazitahusika na kutatua mgogoro wowote kati ya Barrick na Tanzania.

Tanzania Imekosa Shilingi Trilioni 2 kwa Sababu ya Viongozi Kukosa Maarifa

Siku za mwanzo kabisa za mgogoro wa Makanikia nilieleza kuwa Serikali ya Rais Magufuli haina Maarifa ya kuwezesha nchi kupata ushindi katika suala hili, watu wengi walinitukana, lakini leo imedhihirika hivyo.

Wakati ule nilitoa mfano kuwa Acacia ilipotaka kununuliwa na Kampuni nyengine ya Canada kwa thamani ya Dola za Marekani 4.4 Bilioni (wastani wa TZS 10 Trilioni), Tanzania ingefaidika sana kwa kupata Kodi ya Ongezeko la Mtaji ya Dola za Marekani 880 Milioni (wastani wa TZS 2 Trilioni), Serikali haikufanya subira na ikazuia Makanikia na mpango ule wa Acacia kununuliwa ukavubjika.

Leo Serikali yetu imekwenda kuingia MAKUBALIANO YA AIBU kabisa ambayo kiuhalisia tunaishia kufuta kesi za Kodi ya Dola za Marekani 190 Bilioni (wastani wa TZS 400 Trilioni) na tunawalipa Barrick fedha badala ya sisi kupata Fedha. Ni jambo la fedheha mno, wanaojigamba kuwa ni wazalendo leo wametuuza.

Ingekuwa nchi nyengine, Makubaliano haya ya KIMANGUNGO kati ya Serikali ya Rais Magufuli na Kampuni ya Barrick, ingetosha kuiondoa Serikali madarakani. Rais John Magufuli na Waziri Palamagamba Kabudi wameuza nchi yetu kwa kipande cha dhahabu. Wamelihujumu Taifa.

Kabwe Z.Ruyagwa Zitto

Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo

Vuga, Zanzibar

Julai 20, 2019

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

ANGAZO: Unakaribishwa kuwa mwanachama wa #BaruaYaChahali yenye jumla ya vijarida vitano kwa wiki. Jinsi ya kujiunga: Uanachama kwa mwaka mzima ni sh100,00 au sh 10,000 kwa mwezi. Tuma mchango wako kwa m-pesa namba 0767632516 (jina Khadija Katule). Kwa walio nje ya Tanzania, unaweza kuchangia kwa KUBONYEZA HAPA.

Endapo unataka kuondolewa kwenye orodha ya wanaotumiwa #BaruaYaChahali JIONDOE HAPA.

Ndimi mtumishi wako

Evarist Chahali